Monday, October 29, 2012

Twanga Pepeta yakubali matokeo

 
Wanenguaji wa Bendi ya  Twanga Pepeta

Ni zaidi ya wiki mbili sasa tangu mwimbaji wa bendi ya Twanga Pepeta, Uncle Vena aingie mitini, uongozi wa  kampuni ya ASET inayomiliki bendi hiyo umesema kuwa hauhangaiki kumtafuta.

Kwa mujibu wa meneja wa kampuni hiyo Hassan Rehan, awali walikuwa wakimtafuta mwimbaji huyo lakini sasa wameona hakuja haja ya kufanya hivyo na badala yake wanaendelea na kazi kama kawaida.

"Tunajua kwamba ameondoka kwenye bendi akiwa na mkataba wa miaka mitatu, lakini hata hivyo hatuna budi kuachana naye kwani tumejitahidi kumpigia simu, lakini alikuwa hapokei na sasa haipatikani kabisa," alisema Rehan.

Meneja huyo alisema kuwa Twanga Pepeta ina wanamuziki wengi na wenye uwezo mkubwa wanaoendelea kufanya kazi kama kawaida lakini akaongeza kuwa iwapo mwimbaji huyo akijitokeza watamdaka kwa sababu ameondoka akiwa na mkataba wa miaka mitatu ya kuitumikia bendi hiyo ambao aliusaini mwanzoni mwa mwaka huu.

Mwimbaji huyo aliyeibuliwa na Mwinjuma Muumin akiwa naye kwenye bendi yake ya Bwagamoyo Sound, alijiunga Twanga Pepeta mwaka juzi baada ya bendi hiyo kufa.

Uncle Vena ambaye hadi sasa haijafahamika alikotimkia, ameshiriki kikamilifu kurekodi nyimbo za albamu ya 12 ya bendi hiyo ambazo ni 'Mapambano ya Kipato', 'Nyumbani ni Nyumbani',  'Ngumu Kumeza', 'Mwenda Pole Hajikwai', 'Shamba la Twanga' na 'Walimwengu Hawana Jema'.

No comments:

Post a Comment