Kiongozi wa Bendi Kalunde Bob Rubala |
Uongozi wa Kalunde Band hiyo umesema kwamba wataanza kuandaa mipini yenye ladha mbalimbali za asili kwa dhumuni la kudumisha utamaduni wa makabila mbalimbali ya hapa Tanzania.
Hayo yalisemwa na kiongozi wa bendi hiyo Bob Rubala na kuongeza kuwa hatua hiyo inalenga kuifanya Kalunde iweze kupata soko la muziki la ndani na hata nje ya Tanzania.
Bendi hiyo ambayo kwa sasa, inaendelea kuitangaza albamu yake ya pili ya 'Imebaki Stori' mbali na hilo kwa sasa inajipanga kwa ajili ya kuvaa mavazi ya asili kila itakapoporomosha maonyesho yake ya burudani.
"Tunajiandaa kuja kiasili zaidi hasa kwa kuzingatia kuwa bendi yetu inaundwa na wanamuziki wenye vipaji zaidi ya kimoja, hivyo nina uhakika tutafanikiwa," alisema Bob Rudala.
Alisema kuwa wanajiandaa kuanza kutumia mavazi ya asili kwenye onyesho lao la kila Jumatano la 'Usiku wa Mtanzania' ambalo hufanyika ndani ya ukumbi wa Peacock Hotel jijijini Dar es Salaam.
Ameongeza kuwa katika onyesho hilo wamekuwa wakishirikiana na kundi la Wane Star ambalo hutoa burudani ya ngoma za asili, hivyo bendi yao pia haina budi kuwaonjesha mashabiki vionjo vya asili.
"Huo ndio mkakati wetu kwamba albamu ya tatu tutakayoiandaa itakuwa na nyimbo nyingi za vionjo vya asili hasa kwa kuzingatia kwamba uwezo wa kutunga nyimbo za aina hiyo tunao," alisema Rudala.
Kalunde imekuwa ikiendelea kunadi albamu yake ya 'Imebaki Stori' kwenye mikoa mbalimbali nchini ambayo nyimbo zake ni 'Nilie na Nani','Mama Yangu', 'Cisse', 'Fungua', 'Ndoto', 'Uliniependea Nini' na Njoo 'Tucheze'.
No comments:
Post a Comment