Friday, October 19, 2012

MASHUJAA WASOTEA JINA LA ALBUM

Baada ya kimya cha muda mrefu, wiki ijayo bendi ya Mashujaa Musica inatarajia kupata jina la albamu ya pili ambayo tayari nyimbo zake zimekuwa zikisikika redioni na kwenye vituo vya televisheni.

Kwa mujibu wa mmoja wa viongozi wa bendi hiyo Hamis Maero, uongozi wa Mashujaa Musica na wanamuziki utakutana ili kuchagua jina la albamu kabla ya kujiandaa na mikakati ya kuizindua.

"Nyimbo za albamu ya pili zilishamilika kilichobaki ni jina la albamu tu ambalo limechukua muda mrefu bila kupatikana, lakini wiki ijayo tutalipata baada kukutana na wanamuziki pamoja watu wetu wa karibu," alisema.
Rapa wa bendi ya Mashujaa Music, Saulo John 'Ferguson', akiwa kazini.
Alisema kuwa wanawashirikisha watu wao wa karibu katika kutafuta jina la albamu kama njia mojawapo ya kuonyesha jinsi wanavyowajali kwa mchango wao kwa bendi hiyo.

Kiongozi huyo alisema kuwa albamu ya pili imekamilishwa na wimbo wa Chaz Baba uliopewa jina la 'Usidharau Sifuri' ambao unatarajiwa kurekodiwa wiki ijayo na kisha kuingizwa kwenye video.

Aidha, alisema kuwa bendi hiyo inatarajia kuzinduzi albamu ya pili Desemba mwaka huu kwa kushirikisha makundi mbalimbali ya burudani ya jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa albamu ya kwanza ya 'Safari Yenye Vikwazo' waliizindua kwa kushirikiana na mwanamuziki kutoka Kongo lakini sasa kwa albamu ya pili wamepanga kushirikisha vikundi vya nyumbani.

No comments:

Post a Comment