Monday, November 26, 2012

TAARIFA YA KIFO CHA MSANII SHARO MILIONEA KUTOKA KWA KAMANDA WA POLISI MKOA WA TANGA

Sharo Milionea enzi za uhai wake
Namkariri Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga Constantine Massawe akizungumza na East Africa Radio jana usiku akisema, “leo majira ya saa mbili usiku kwenye barabara ya Segera Muheza mtu mmoja alietambulika kwa jina la Hussein Ramadhani au Sharo Milionea akiwa anaendesha gari namba T478 BVR Toyota Harrier akitokea Dar es salaam kwenda Muheza alipofika eneo la Maguzonizonga wilayani Muheza hilo gari lake liliacha njia na kupinduka mara kadhaa na kusababisha kifo chake, mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye hospitali Teule ya wilaya ya Muheza”

Kamanda amesema hakuna kona kali sana wala ubovu wa barabara kwenye sehemu aliyopata ajali Sharo Milionea, katikati ya Segera na Muheza ambapo gari imehifadhiwa mahali salama kwa sababu haitembei.
Kwenye gari alikuwa mwenyewe hivyo hakuna taarifa kamili ya nini kilichotokea maana inaweza kuwa alisinzia.

R.I.P Sharo tulikupenda lakini mungu kakupenda zaidi, kazi zako tulizipenda na tutakukumbuka kwa mengi.

Friday, November 23, 2012

DJ CHOKA AFUNGUKA KUHUSU MTOTO WAKE

Mdau mkubwa wa muziki bongo, DJ Choka (pichani) amezungumza na ENEWS ya Eatv  kuhusu furaha aliyonayo baada ya kupata mtoto wake wa kwanza jana.

DJ Choka amesema amefurahi sana kupata mtoto huyo wa kiume kwani kiu yake kubwa ilikuwa ni kupata mtoto wa jinsia hiyo ambae atakuwa si mtoto tu kwake bali ni rafiki yake kwa kuwa yeye ni mtoto pekee wa kiume kwenye familia yao.

Hongera DJ Choka kwa kupata Jembe.

USIKOSE USIKU WA KHANGA ZA KALE LEO SERENA HOTEL

Thursday, November 22, 2012

MUUMINI AENDELEA KUTANGA TANGA, AIHAMA TENA TWANGA SASA AKIMBILIA VICTORIA SOUND

Muumin Mwinjuma(kulia) akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu kuhama  bendi ya African Stars(Twanga Pepeta) na kujiunga na Bendi ya Victoria Sound.  Kushoto ni Meneja wake, Abdulfarid Hussein na Mkurugenzi wa Victoria Sound Daniel Denga Mjema.
Mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi mwenye sifa kubwa ya kutotulia kwenye bendi moja kwa muda mrefu, Mwinjuma Muumini ambae alitamba miaka ya 90 na nyimbo kama Tunda akiwa na Tamtam sound iliyokuwa inamilikiwa na ASET, na baadae kuihama bendi hiyo na hatimaye kuzunguka kwenye bendi tofauti tofauti ambapo mwaka jana aliamua kurudi kwenye kampuni ya ASET na kujiunga na Bendi ya African Stars (Twanga pepeta), jana ametangaza tena kujiengua kwenye bendi hiyo na kujiunga na bendi changa ya Victoria Sound.

Akizungumza na blog hii jana, Muumini alisema ameamua kuihama bendi hiyo kubwa na kuhamia kwenye bendi hiyo changa ambayo haifahamiki na hata watu 20 ingawa imeanzishwa miaka mitano iliyopita kwa kuwa anaangalia zaidi maslahi na uhuru wa kufanya kazi kuliko kuwa kwenye bendi kubwa ambayo haijampa mkataba na maslahi madogo.

Aidha Muumini aliwataka mashabiki wake kumuelewa na kutomfikiria vibaya kwani kuhama kwake hakuathiri chochote kazi yake ila anaboresha zaidi kazi yake, hivyo mashabiki wakae mkao wa kula ili kupokea kazi zake mpya ambazo anatarajia kuzitoa mwakani akiwa na bendi hiyo ya victoria, ambapo hivi sasa yuko mapumzikoni kwa ajili ya kujipanga kwa mashambulizi mwakani.

Nakumbuka mara baada ya kurudi Twanga niliongea na Muumini kupitia kipindi changu(Afrobeat) ambapo alijigamba kuwa sasa amefika kweli kama ambavyo aliwahi kuimba miaka ya nyuma na kamwe hawezi kuihama bendi hiyo mpaka pale atakapostaafu muziki, nimeshangaa kusikia eti amehama tena, namshauri ajiangalie nafikiri hicho anachofanya ni kitendo cha kujimaliza mwenyewe kwa kuua kipaji chake na kujishushia heshima kwa mashabiki, sitoshangaa nikisikia baada ya miezi kadhaa anatangaza tena kuihama bendi hiyo kwa visingizio kibao visivyo na msingi.

MLOPELO AFARIKI DUNIA

Msanii wa maigizo wa siku nyingi aliyekuwa katika kundi la kaole na kutamba katika tamthilia mbalimbali zilizokuwa zikionyeshwa na kituo cha Televisheni cha ITV amefariki dunia leo baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Mlopelo alijipatia umaarufu mkubwa sana kutokana na aina ya uigizaji wake na nafasi alizokuwa akizicheza kama mganga wa kienyeji.

Mwenyezimungu aiweke roho ya marehemu mlopelo mahali pema peponi

KIJANA HUYU ANAHITAJI MSAADA WAKO


Kijana Swakimu Elius mwenye umri wa miaka 14 mkazi wa Mtwara anahitaji msaada wako wa hali na mali kutokana na maradhi ya uvimbe usoni yanayomkabili.
 
Akizungumza kwa shida katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikolazwa kijana huyo, Swakimu amesema
 
“Ugonjwa huu ambao sijui chanzo chake umekuwa ukinitesa sana na kunifanya nishindwe kuendelea na masomo katika Sekondari ya Libobe, Mtwara.

“Uvimbe unaonitesa ulianza kama kipele lakini kadiri siku zilivyokuwa zikisonga mbele uliongezeka ndipo nilikwenda Hospitali ya Mkoa wa Mtwara ambapo walinitibu kisha waliniambia nije hapa Muhimbili kwa matibabu zaidi.

“Kinachonihuzunisha sina msaada wowote kwani ndugu yangu aliyenipokea hana uwezo na ninatakiwa kutoa gharama za matibabu shilingi 90,000 na damu,” alisema mtoto huyo.

“Nawaomba Watanzania wanisaidie kiasi hicho cha fedha na damu ili nifanyiwe upasuaji ambao nimeelezwa na madaktari kwamba utaisha na kuwa na afya njema,” alieleza Swakimu kwa uchungu.

Afisa Ustawi wa Jamii Mwandamizi wa Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili, Mary Ochieng aliomba kijana huyo asaidiwe kwa kuwa hana ndugu wa kumsaidia.

Yeyote atakayeguswa na maradhi ya kijana huyu aende wodi namba 23 Sewa Haji, Muhimbili .
 
                                                            "Kutoa ni moyo si utajiri"

Wednesday, November 21, 2012

MAPOKEZI YA VIONGOZI WA CCM MTWARA

Maandamano ya pikipiki ya wanachama na wafuasi wa CCM Mkoani mtwara yakiongoza msafara wa Viongozi hao kuelekea Ofisi za CCM Mkoa wa Mtwara.
Viongozi wa Juu wa chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa wakiongozwa na Katibu Mkuu, Abdulrahaman Kinana, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na Katibu wa Oganizesheni, Dk. Mohamed Seif Khatib wamewasilili mkoani Mtwara leo kwa ziara maalum ya kuimarisha chama hicho. Pichani kulia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara,  Mohamed Sinani akiwapokea viongozi hao katika Uwanja wa ndege wa Mtwara.

NISHA AKANA KUTOKA KIMAPENZI NA NEY WA MITEGO

Nisha katika pozi
Moja kati ya picha za Ney na Nisha zilizovuja

Siku chache baada ya picha za kimahaba za msanii Ney wa Mitego na Nisha kuvuja Nisha ameamua kufunguka kuhusu uhusiano uliopo kati yao.

Akizungumza katika kipindi cha Hotmix cha EATV Nisha amefunguka kuwa hakuna uhusiano wa mapenzi kati yake na Ney ila picha hizo zimetokana na movie yao mpya ambayo walikuwa wakishoot na picha hizo walizipiga wakati wa maandalizi ya movie hiyo ambayo inatarajiwa kutoka mapema mwakani.

 Aidha Nisha ameongeza kuwa picha hizo zimevuja baada ya simu waliyotumia kwa kupiga picha hizo kupotea na mtu aliyeokota simu hiyo ndiye aliyezisambaza, hata hivyo amewatupia lawama baadhi ya waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari kwa kukurupuka na kuandika habari kuhusu picha hizo bila hata ya kuwauliza wahusika ili wapate ukweli wa picha hizo.

Wednesday, November 14, 2012

PUMZIKA KWA AMANI LULU WETU

Pichani juu na chini ni marehemu Lulu Oscar wakati wa uhai wake
Aliyekuwa mwandishi wa habari na mtangazaji wa kituo cha SIBUKA TV, aliekuwa akitangaza kipindi cha Pepeta afrika, Lulu Oscar (pichani)amefariki dunia jana nyumbani kwao Mbezi Kwa Yusufu.

Akizungumz na blog hii, mdogo wa marehemu, Ritha Oscar alisema kuwa Lulu alipatwa na mauti hayo majira ya usiku ambapo alizidiwa ghafla kufuatia kulalamikia kifua kumbana.

Siku chache zilizopita alikuwa amelazwa kwenye hospitali ya Masister ya Luguluni Mbezi, zaidi ya mara tatu, baadae aliruhusiwa kurudi nyumbani baada ya kuendelea vizuri lakini juzi usiku alilalamikia kifua kikimbana tulimuhangaikia mpaka hatua ya mwisho lakini ikashindikana na alipoteza maisha” alisema Ritha huku akilia.

Aidha, alisema kuwa, ndugu baada ya kukutana wamekubaliana kuuzika mwili wa marehemu siku ya Alhamisi(kesho) katika Makaburi ya Kinondoni na msafara utaanzia nyumbani Mbezi kwa Yusufu na kuelekea Makaburini.

Katika historia yake, Lulu alihitimu elimu yake ya msingi mwaka 1996 katika shule ya Upanga pia ana elimu ya uandishi wa habari aliyoipata chuo cha uandishi wa habari na utangazaji (Royal College of Tanzania) aliyohitimu mwaka 2009 ambapo mwaka 2003,  alihitimu kozi ya elimu ya juu katiika Taasisi ya uandishi wa habari na mawasiliano Institute of journalisim and mass communication DSM.

Nimesikitishwa sana na kifo cha Lulu kwani pamoja na kwamba nilisoma nae lakini tulikuwa tukiwasiliana mara kwa mara kwa kuwa tulikuwa tukifanya vipindi vinavyofanana na mara nyingi alikuwa akinipigia na kuniomba namba za wasanii mbalimbali wa muziki wa dansi, na mara ya mwisho tuliwasiliana wiki mbili zilizopita akiniomba namba ya mwanamuziki na Rais wa mashujaa musica Charles Baba.


Tulikupenda sana Lulu lakini mungu amekupenda zaidi, Pumzika kwa amani ndugu yangu, rafiki yangu  mbele wewe nyuma sisi.

Mwenyezimungu aiweke roho yako mahali pema peponi.. Amina.

Tuesday, November 13, 2012

TIGO WATOA VIFAA VYA NISHATI YA JUA KWA AJILI YA KUCHAJIA SIMU

Ofisa Masoko wa kampuni ya Tigo Jacqeuline Nnunduma (kushoto)  na Meneja Mradi wa Kampuni hiyo, Yaya N'dojere pamoja na Ofisa Uhusiano Msaidizi wa Tigo, Mariamu Mlangwa wakionyesha kifaa cha solar kinavyoweza kufanya kazi ya kuchaji simu kwa njia ya nishati ya jua.
Ofisa masoko wa kampuni ya Tigo Jacquline Nnunduma kushoto  na Meneja Mradi  wa Kampuni hiyo, Yaya N'dojere wakionyesha kifaa cha solar kinavyoweza kufanya kazi ya kuchaji simu kwa njia ya nishati ya jua.
Ofisa masoko wa kampuni ya Tigo Jacqueline Nnunduma kushoto akionesha jinsi  ya kifaa cha solar kinavyoweza kufanya kazi kulia ni Meneja Mradi wa Kampuni hiyo, Yaya N'dojere.

ALLY REMTULLAH, DIANA MAGESSA KUWASHA MOTO MITINDO NIGHT 3 WASHINGTON

TANZANIA'S TOP DESIGNERS -ALLY REHMTULLAH NA DIANA MAGESSA KUWASHA MOTO KATIKA MAONYESHO YA MAVAZI YA MITINDO NITE 3 USA YANAYO FANYIKA KILA MWAKA JUMAMOSI YA THANKS GIVING WASHINGTON DC YANAYOANDALIWA NA DESIGNER MA WINNY NA J &P.

MMOJA WA WARATIBU WA MAONYESHO HAYO YA MITINDO..MR DICKSON MKAMA ..a.k.a " DMK" AMETHIBITISHA KUWA MWAKA HUU WAMEJIANDAA KWA SHOW YA AINA YAKE AMBAYO MBALI NA TANZANIA  KUNA MADISIGNER KUTOKA NCHI MBALI MBALI ZA AFRICA  NA CARIBBEAN PAMOJA NA SUPER MODELS 16 KUTOKA KAMPUNI YA "IHI MODELING AGENCY",UKUMBI WA KISASA KABISA NA BURUDANI KABAMBE KUTOKA KWA MWANAMUZIKI MAHIRI WA KIKE " HAFSA KAZINJA ".

MAONYESHO HAYO YANALETWA KWENU NA MAKAMPUNI YA J&P ENT, DMK GLOBAL PROMOTIONS,NORTHERN ZONE ENT..NA YATARUSHWA LIVE NA VIJIMAMBO TV...MC WA USIKU HUO WA MITINDO ATAKUWA SUNDAY SHOMARI KUTOKA VOICE OF AMERICA!

MATOKEO YA UCHAGUZI WAJUMBE WA NEC YAVUJA

Wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM kutoka mkoani Mtwara
Mh. Wassira akiwa na baadhi ya wajumbe wa mkutano huo


MATOKEO  ya uchaguzi wa wajumbe wa NEC katika kura zilizopigwa juzi mjini Dodoma katika mkutano wa  nane wa Chama cha Mapinduzi (CCM) yamevuja.

Huku Mwenyekiti wa chama hicho kinachoiongoza Serikali, Rais Jakaya Kikwete akitangaza jana kuwa matokeo hayo yatatangazwa leo pamoja na matokeo ya nafasi za Makamu Mwenyekiti lakini tayari hadi jana mchana zaidi ya asiliamia 90 ya wajumbe walisha jua matokeo hayo na kuanza kupongezana huku yale ya wagombea wa bara yakiwekwa na idadi ya kura zao. 

Ingawa baadhi ya wajumbe wameoneshwa kushangazwa na idadi ya kura alizopata Katibu Mkuu wa Chama hicho Wilson Mukama kwa kushika nafasi ya 9 huku Steven Wasira akiwaongoza.

Wanaodaiwa kushinda nafasi 10 Zanzibar:
Mbunge wa Uzini, Mohamed Seif Khatib; Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Ali Mwinyi, Waziri wa Fedha Zanzibar, Omar Yussuf Mzee, Abdulhakim Chasama na  Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Shamsi Vuai Nahodha.

Wengine  ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Khadija Hassan Aboud, Bhaguanji Mansuria, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa na Khamis Mbeto.

Wanaodaiwa kushinda Bara

Majina ya wajumbe wa Nec walioshinda bara na kura walizopata katika mabano ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira aliyeongoza kundi hilo kwa kupata kura 2,135, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba (2,093), Mwekahazina wa CCM, Mwigulu Nchemba (1,967), na Katibu wa UVCCM, Martine Shigela (1,824).

Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi (1,805), Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard Membe (1,455), Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mathayo David Mathayo (1,414), Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Jackson Msome (1,207), Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama (1,174) pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana  na Michezo, Fenela Mukangara (984).

SOURCE:http://mrokim.blogspot.com

HAPPY MOMENT

SALAMA J NDANI YA BONGO 5

Friday, November 9, 2012

MKANGANYIKO SKENDO YA AUNT EZEKIEL, TUCHUKUE LIPI?

JE UNAFIKIRI HISTORIA KUJIRUDIA, MTOTO WA FAMILIA YA NKWABI KUTWAA TAJI LA EBSS KWA MARA NYINGINE?

Baada ya mchuano wa miezi mitatu wa kumtafuta mshindi atakayetwaa Taji la EBSS mwaka huu, hatimaye mshindi kujulikana leo, ambapo washiriki watano watachuana vikali huku kila mmoja akihakikisha ananyakua ushindi huo.

Washiriki hao watano wanochuana katika kinyang'anyiro hicho mwaka huu ni Walter Chilambo, Wababa Mtuka, Salma Abushiri, na watoto wa familia moja Nsami Nkwabi na Nshoma Ng'hangasamala.

Fainali hizo zitafanyika leo katika ukumbi wa Diamond Jubilee kwa viingilio vya VVIP Tshs 70,000, VIP Tshs 30,000 na kawaida Tshs 10,000 ambapo mshindi atajinyakulia kitita cha shilingi milioni hamsini pamoja na mkataba wa kurekodi nyimbo kutoka kwa
wadhamini wakuu wa shindano hilo, kampuni ya simu za mkononi Zantel

Wasanii watakaopamba kwa burudani katika fainali hizo ni Rich Mavoko, Ommy Dimpoz, Ben Paul, Linah, Amini, Mzee Yusuf na mkewe Leyla Rashid, mshindi wa shindano hilo mwaka jana(Haji Ramadhan) Mwasiti, Ditto, Linex na Barnaba. 

USIKU WA TWANGA DAR LIVE JUMAPILI HII


Thursday, November 8, 2012

VIONGOZI WA UAMSHO ZANZIBAR WAENDELEA KUSOTA RUMANDE

Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi Zanzibar
Viongozi wa Jumuiya mbili za Kiislam Kisiwani Zanzibar wanaotuhumiwa kwa makosa tofauti ya kutoa lugha za uchochezi na kusababisha ghasia na vitendo vya uvunjifu wa amani uliopelekea uharibifu wa miundombinu ya barabara ambao leo walifikishwa Mahakama Kuu ya Vuga mjini Zanzibar, wamerudishwa tena Rumande.
Kesi hiyo ambayo inawakabili Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar Sheikhe Faridi Hadi Ahmedi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Uamsho Sheikhe Mselem Ali Mselem, Mussa Juma Issa, Suleiman Juma Suleiman, Azan Khalid Hamdan, Khamis Ali Suleiman, Hassan Bakar Suleiman na  Ghalib Ahmada Omar iliitwa mahakama kuu kwa kutajwa baada ya kuahirishwa mwezi uliopita.
Hata hivyo, kabla ya kutajwa tena kwa kesi hiyo, huku kukiwa na ulinzi mkali wa Makachero wa Polisi na Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia, ndani ya Mahakama hiyo kulizuka mabishano makali ya kisheria huku kila upande ukionyesha ujuzi wao wa kisheria.

Kwa upande wa Mawakili wa Watuhumiwa Bw. Salum Toufik na Bw. Abdallah Juma Kaka, wakiwasilisha hoja mbalimbali za uvunjifu wa haki za watuhumiwa ikiwemo ya kunyolewa ndevu wakiwa Rumande katika Chuo cha Mafunzo jambo ambalo ni kinyume na uhuru wa kuabudu kwani wamesema ndevu kwa mashehe ni sehemu ya ibada.
Baada ya kuwasilisha hoja hizo, Mwanasheria wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bw. Ramadhani Nassibu, akinukuu vifungu vya sheria vilivyopo kwenye Katiba ya Zanzibar na kusema kuwa kama kuna haki zinazovunjwa na chombo chochote ama mtumishi wa Serikali kuna mahala pengine pa kupeleka malalamiko hayo.
Baada ya mabishano hayo, Mrajisi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar Mh. George Kazi, aliamuru watuhumiwa wote warudishwe tena rumande hadi Novemba 20, mwaka huu itakapokuja tena katika Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa kutajwa.

SERIKALI YA JAPAN YATIA SAINI MSAADA WA SHS MIL 380 KWA AJILI YA MIRADI MIPYA YA LINDI NA MTWARA

Balozi wa Japan nchini Tanzania, Masaki Okada akisoma hotuba yake kwa viongozi wa mkoa wa Lindi na Taasisi ya Women in Social Entrepreneurship (WISE) ya mkoani Lindi wakati wa utilianaji saini mkataba wa makubaliano kati ya Ubalozi wa Japan na Taasisi ya WISE msaada wa ujenzi wa bweni la wasichana sekondari ya Ng'apa ya Lindi utakaogharimu shilingi Milioni  188. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Ludovick Mwananzila na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Nassor Hamid Nassor.
Mkurugenzi wa taasisi Women in Social Entrepreneurship (WISE) ya mkoani Lindi, Astronaut Bagile (kushoto) akitiliana saini na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Masaki Okada (wa tatu kulia) msaada wa ujenzi wa bweni la wasichana sekondari ya Ng'apa ya Lindi utakaogharimu shilingi Milioni  188. Wengine wanaoshuhudia utiaji saini huo kutoka kushoto ni Meya wa Manispaa ya Lindi, Frank Maghali, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Ludovick Mwananzila, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Nassor Hamid Nassor na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi,  Ashimun Mnzava.Utiaji saini huo wa makubaliano hayo ya msaada ulifanyika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi Novemba 7, 2012.

KHANGA ZA KALE 2012


RUSSELL SIMMONS ATOA DOLA ELFU KUMI KUCHANGIA FLAVIANA MATATA FOUNDATION

Mfanyabiashara mkubwa nchini Marekani Russell Simmons ametoa Dola za kimarekani 10,000(zaidi ya mil. 15 za kitanzania) kwa ajili ya kusaidia mfuko wa Flaviana Matata (Flaviana Matata Foundation).

Katika mazungumzo yao kwenye mtandao wa kijamii (Twitter) Simmons amesema anajisikia furaha kumsaidia mtu ambae ameweza kusaidia wengine nchini Tanzania.

Russel Simmons si jina geni masikioni mwa wengi kwani hapo miaka ya nyuma iliripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa mfanyabiashara huyo anatoka kimapenzi na mwanamitindo huyo lakini baadae Flaviana alikanusha habari hiyo.
Hata hivyo Uncle Russell kama wenyewe wanavyomuita ni mmoja kati ya watu waliomtengenezea njia ya kupata mkataba wa uanamitindo na kuitangaza Tanzania nchini Marekani na kwingineko.

Flaviana Matata Foundation ilizinduliwa May 21,2011 kwa ajili ya kusaidia watu wasio na uwezo, wanawake na watoto.

Wednesday, November 7, 2012

MAMA MZAZI WA RAY C AFUNGUKA KUHUSU MWANAE, AOMBA MSAADA KWA WATANZANIA NA MASHABIKI WA RAY C

Siku chache baada ya vyombo vya habari kuripoti kuwa mwanamuziki Ray C (kiuno bila mfupa, pichani chini) ameathirika kwa kutumia madawa ya kulevya, mama mzazi wa msanii huyo (pichani juu)  amejitokeza na kuomba msaada kwa ajili ya matatizo ya mtoto wake.
Akizungumza na kipindi cha Hotmix kinachoruka kupitia Eatv mama huyo amefunguka kuwa ni kweli kuwa mtoto wake huyo ameathirika kutokana na matumizi ya dawa za kulevya na kuwataka waandishi wa habari kutoandika habari zitakazomkatisha tamaa msanii huyo, watu waliojitolea kumsaidia na familia yake kwa ujumla.
Aidha mama huyo ameongeza kuwa tatizo lililompata Ray C linaweza kumpata mtu yeyote hivyo amewaomba mashabiki wake kuelewa tatizo hilo na waendelee kumuombea na kumsaidia ili aweze kupona na kuondokana na matumizi ya dawa hizo kabisa.
Mama huyo amewaomba wasamaria wema na mashabiki wa msanii huyo wenye uwezo kujitokeza na kumsaidia mama huyo pesa kwa ajili ya kumuuguza mwanae kwa kuwa dawa anazotumia ni za gharama kubwa hivyo yeye peke yake hawezi kumudu kuzinunua.

Kwa mawasiliano zaidi na mchango waweza wasiliana na mama huyo kwa simu namba 0655 666700

HONGERA RAIS BARRACK OBAMA

Rais Barrack Obama akiwa na familia yake mara baada ya kutangazwa kuwa ni mshindi, akiwa tayari kwa kutoa Speech.
Rais wa Marekani Barrck Obama

Monday, November 5, 2012

DOGO ASLAY AWANIA TUZO ZA KORA MWAKA HUU

Akiwakilisha kundi la TMK wanaume Family Dogo Asley ametajwa na mtandao wa Kora All Africa Music Award kuwa ni mmoja kati ya wasanii watakauwepo kwenye kinyang'anyiro hicho mwaka huu akiwania tuzo ya Best New comer.

Hivyo wewe Mtanzania na shabiki wa muziki bongo unaombwa kutoa support yako kwa kumpigia kura dogo huyo ili aweze kujichukulia tuzo ambazo zinatarajia kutolewa December 29 mwaka huu nchini Ivory Coast.

Dogo Asley anawania Tuzo hiyo kupitia wimbo wake wa "Niwe nawe".

Sunday, November 4, 2012

REDD'S MISS TZ 2012 NI BRIGITTE ALFRED

Redd's Miss TZ 2012 Brigitte Alfred akia na furaha mara baada ya kutangazwa mshindi wa kinyang'anyiro hicho.
Redd's Miss Tz 2012 Brigitte Alfred (katikati) akiwa na mshindi wa pili Eugene Fabian (kushoto) na mshindi wa tatu Edda Sylvester (kulia) mara baada ya kutangazwa mshindi wa shindano hilo lililokuwa likiwaniwa na warembo 30.

Friday, November 2, 2012

JB MPIANA KUSINDIKIZA UZINDUZI WA RISASI KIDOLE DAR, MWISHO WA MWEZI

Mwanamuziki kuto DRC Congo JB Mpiana (pichani) anatarajia kufanya onyesho mwishoni mwa mwezi huu, katika viwanja vya Leaders Club Jijini Dar Es Salaam.

Waandaaji wa onyesho hilo wamesema itakuwa ni mara ya kwanza kwa JB kufanya onyesho Tanzania baada ya miaka 9 iliyopita na kuongeza kuwa lengo la onyesho hilo ni kuzindua Album mpya ya Mashujaa Musica iitwayo "Risasi Kidole" pamoja kwa kushirikiana na kampuni ya QS itakayokuwa ikijihusisha na masuala ya kukuza vipaji vya wasaniiwa muziki wa kizazi kpya hapa nchini.

HIVI NDIVYO GARI YA WOLPER ILIVYOCHOMWA MOTO

Gari hiyo inavyoonekana kwa mbele
Hii ndiyo sehemu ambayo imechomwa na ukiangalia kwa juu utaona Turubai nalo limechomwa moto na kwa maelezo ya Wolper mwenyewe anahisi mtu huyo aliyefanya tukio hilo alirusha kitambaa kilicholowanishwa mafuta na kukirusha kwenye turubai hilo kwa lengo la kuunguza gari hiyo aina ya Toyota Brevs.
Kwa nyuma gari hiyo inaonekana hivi
Kwa karibu zaidi jinsi gari hiyo ilivyochomwa.

Watu wasiojulikana wamechoma moto Gari ya Staa wa Filamu Tanzania Jackline Wolper aina ya Toyota Brevs.

Kwa mujibu wa Wolper mwenyewe tukio hilo limetokea usiku wa Oktoba 23, 2012 ambapo inahisiwa kuwa mtu huyo alitumia matambara yenye mafuta ya taa au petroli na kuyarusha ndani ya nyumba anayoishi Wolper kwa lengo la kuichoma gari hiyo.

Wolper amesema kuwa mpaka sasa hakuna mtu nayemhisi kuhusika na tukio hilo kwa kuwa katika kumbu kumbu zake hakumbuki kuwa na ugomvi na mtu yeyote ambao umepelekea tukio hilo ila anaamini kuwa mtu/watu waliohusika na tukio hilo ni wale wasiopenda maendeleo yake.
"Kiukweli siwezi kumuhisi mtu ila najua ni lazima atakua mtu asiependa maendeleo yangu ni mtu mbaya sana kwangu. Na inawezekana kabisa alipanga kuniua lakni kwa bahati nzuri siku hiyo sikua nyumbani nilikua nimesafiri." alisema Wolper.
Ameongeza kuwa amepeleka taarifa hizo katika kituo cha polisi Kawe kwa ajili ya msaada wa kiupelelezi.
Blog hii inampa pole Wolper kwa tukio hilo, vitendo kama hivi ni vitendo vya kinyama na havifai katika jamii na tunapaswa kuwa na wivu wa maendeleo na si wivu wa aina hii wa kurudishana nyuma.

Habari hii ni kwa mujibu wa Wolper mwenyewe na Blog yake ya www.jacklinewolper.blogspot.com

NANI KUNYAKUA TAJI LA REDD'S MISS TZ 2012?



Anaitwa EUGENE FABIAN Mbio za kulisaka taji la Miss Tanzania amezianzia Mkoani Mara na baadae kutwaa taji la Kanda ya Ziwa na anavalia namba 21 kambi ya taifa.
ANANDE RAPHAEL ni mshiriki namba 11 akitokea Mkoa wa Kilimanjaro akiwakilisha Kanda ya Kaskazini.

  Huyu ni VIRGINIA MOKIRI  ni mshiriki namba 1. Akitokea Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na akiwakilisha Elimu ya Juu.
BABYLOVE KALALA ni Mshiriki na 9 akitokea mkoa wa Kagera, akiwakilisha Kanda ya Ziwa.
BRIGITTE ALFRED ni Mshiriki namba 26 akitokea Kitongoji cha Sinza na anawakilisha Kanda ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Jina lake ni BELINDA MBOGO  ni mshiriki na 29 akitoka mkoa wa Dodoma akiwaklilisha Kanda ya Kati
J
CAREN  ELIAS mshiriki 23 anatokea Mbeya anawakilisha Nyanda za Juu Kusini
CATHERINE MASUMBIGANA ni mshiriki na 15 akitokea Kitongoji cha Chang'ombe anawakilisha kanda uya Temeke jijini Dar es Salaam.
DIANA HUSSEIN amepata namba ya ushirtiki 20, akitokea kitongoji cha Dar Indian Ocean, akiiwakilisha Kanda ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
FINA REVOCATUS anavaa namba 12 akitoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha IFM, akiwakilisha Kanda ya Vyuo Vya Elimu ya Juu.
Kutoka Kahama- Shinyanga ni HAPPINESS RWEYEMAMU ananamba 8 anawakilisha Kanda ya Ziwa.
EDDA SYLVESTER amepata namba 22, akitoka Kigamboni na anaiwakilisha Kanda ya Temeke jijini Dar es Salaam
ELIZABETH DIAMOND anavalia namba 2 akitokea mkoa wa singida, akiwakilisha kanda ya Kati.
FATMA RAMADHANI nambari yake 25 akitoka chuo cha Uandishi wa habari Arusha ASJ, anawakilisha Kanda ya Elimu ya Juu.
FLAVIAN MAEDA anavalia namba 10 akitokea kitongoji cha Kurasini mwakilishi wa kanda ya Temeke jijini Dar es Salaam.
KUDRA LUPATOni mshiriki 24 akitokea kitongoji cha Dar Indian Ocean, akiiwakilisha Kanda ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Huyu ni HAPPYNESS DANIEL namba yake ya ushiriki ni 19 anatokea jiji la Mwanza akiwakilisha Kanda ya Ziwa.
IRINE VEDA anatokea Lindi na kupata namba 16 akiuwakilisha Kanda ya Mashariki
JESCA HAULE ni mshiriki namba 14, akitoka kitongoji cha Chang'ombe anawakilisha Kanda ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Kutoka Mji kasoro Bahari-Morogoro ni JOYCE BALUHI akiwa ni mshiriki 13 anawakilisha Kanda ya Mashariki
MAGDALENA ROY mshiriki nambari 18, kutyoka mkoa wa Iringa akiwakilisha Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Huyu ni LIGHTNESS MICHAEL anavalia 5, akitokea Dodoma akiwakilisha Kanda ya Kati.
Kutoka mkoa wa Manyara ni LUCY STEPHANO mshiriki namba 4 akiwakilisha Kanda ya Kaskazini.
MAGDALENA ROY mshiriki namba 6, kutoka Kitongoji cha Dar City Centre akiwakilisha Kanda ya Ilala.
Anaitwa Mary Chizi akitokea kitongoji cha Ukonga, anavalia namba 17, akiwakilisha Kanda ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Anaitwa ZUWENA NASIB akiwa ni mwakilishi pekee wa chuo Kikuu Huria OUT.
Jinalake ni NOELA MICHAEL yupo na namba 27, anashikilia taji la kitongoji cha Tabata na ni mwakilishi tegemeo wa Kanda ya Ilala.
Rose Lucas ana namba 28 akitokea Mkoa wa Pwani akiwakilisha Kanda ya Mashariki
VENCY EDWARD  ni mshiriki nambari 7, akitoka Mkoa wa Rukwa akiwakilisha Kanda ya Nyanda za Juu Kusini
WARID FRANK huyu ni mshiriki namba 30 akitokea Arusha ana kuiwakilisha  Kanda ya Kaskazini.


 Unafikiri ni nani anaweza kutwaa Taji la REDD'S Miss Tanzania 2012?

Kitendawili hicho kitateguliwa kesho ambapo ndiyo siku ya
Fainali za kinyang'anyiro hicho zinazotarajia kufanyika katika ukumbi wa Blue Pearl Ubungo Plaza, ambapo warembo 30 hapo juu watachuana vikali ili kuonyesha kuwa anastahili kuibuka mshindi na kutwaa Taji hilo.
Picha na www.mrokim.blogspot.com