Friday, October 19, 2012

MR. NICE ASIMAMA UPYA KILIMANJARO

Msanii anayejaribu kurejesha makali yake ya zamani, Nice Lucas Mkenda 'Mr Nice', amefyatua wimbo mwingine mpya uitwao 'Imesimama'.

Wimbo huo ni kati ya mfululizo wa nyimbo zinazotolewa na msanii huyo zitakazokuwa katika albamu yake itakayofahamika kwa jina la 'Tabia Gani'.

Mr Nice alisema wimbo huo ameufyatulia nyumbani kwao Moshi-Kilimanjaro katika studio za prodyuza aiwate Tibe, na kwa sasa anafanya mipango ya kurekodi video yake pia mkoani humo
.
Mr Nice alisema wimbo huo unaozungumzia masuala ya usaliti ambao wanadamu wanafanyiana hata kama wana undugu na urafiki wa karibu kiasi gani, unatarajiwa kuachiwa hewani leo (Ijumaa).

"Natarajia kuachia hadharani wimbo wangu mpya uitwao 'Imesimama', ambao nimeurekodia hapa kwetu Moshi, ambako niko kwa sasa kwa mapumziko nikijiandaa pia kuitoa video yake huku huku," alisema Mr Nice.
Nice Lucas Mkenda 'Mr Nice'


Wimbo huo ni mfululizo wa 'ngoma' mpya alizoibuka nazo msanii huyo aliyewahi kutamba nchini akitambulika kama 'Mfalme wa Takeu' baada ya kimya cha miaka saba.

Nyimbo nyingine zinazoendelea kutamba kwenye vituo vya redio na runinga kwa sasa ni 'Tabia Gani' 'Nionje Kidogo' na 'Mfalme' maarufu kama Le Ray aliyoimba na wasanii wa kimataifa kutoka Hispania.



No comments:

Post a Comment