Wednesday, April 11, 2012

TAARIFA YA POLISI KUHUSU WATU KUPOTEZA MAISHA WAKATI WA MAZISHI YA STEVEN KANUMBA

Kutokana na taarifa zilizoenea mtaani kuwa kuna watu kadhaa wamepoteza maisha wakati wa mazishi ya mpendwa wetu marehemu Steven Kanumba, Jeshi la polisi limekanusha taarifa hizo.

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa kipolisi Kinondoni Charles Kenyela amesema hakuna ukweli wowote wa taarifa hizo na kuwa huo ni uvumi tu uliotokana na watu wengi kudondoka, lakini ukweli ni kwamba hakuna aliyepoteza maisha.

Kenyela alibainisha kuwa wengi kati ya watu waliodondoka walipewa huduma papohapo na watoa huduma wa chama cha msalaba mwekundu(Redcross) na kupata nafuu ingawa kuna wengine walipata nafuu wakati wakiwa njiani wakipelekwa hospitali wakati watu wapatao 10 walifikishwawa Hospitali na kati yao watu 9 walipelekwa Hospitali ya mwananyamala na mmoja alipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na wote waliruhusiwa baada ya muda.

Kwa upande mwingine Kamanda Kenyela ameeleza kuwa pamoja na taarifa hizo pia hawajapata taarifa za watu kuibiwa ingawa idadi ya watu ilikuwa kubwa kuliko ilivyotegemewa ambapo alisema hawezi kukadiria idadi ya watu waliofika lakini kwa haraka haraka walikuwa watu zaidi ya 25,000(Elfu ishirini na tano).

No comments:

Post a Comment