Thursday, April 12, 2012

SHIRIKISHO LA FILAMU NCHINI "TAFF" WAPIGA MARUFUKU UUZAJI WA VIDEO ZA MAZISHI YA MAREHEMU STEVEN KANUMBA

Marehemu Steven Kanumba enzi za uhai wake
SHIRIKISHO  la Filamu Nchini(TAFF),limesema litamchukulia hatua za kisheria mtu yeyote atakayebainika kuuza CD za shughuli za mazishi ya marehemu Steven Kanumba bila ridhaa ya familia.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari nyumbani kwa marehemu Vatican Sinza, Rais wa shirikisho hilo Simon Mwakifamba alisema lengo la mkutano huo lilikuwa ni kutoa salamu za shukurani kwa wote waliohudhuria msiba huo na kutoa tahadhari hiyo.
Mwakifamba alisema tayari wameshapata taarifa za watu kuanza kuuza cd hizo kwa lengo la kujipatia fedha jambo ambalo sheria ya filamu hairuhusu.
Kwa mujibu wa Rais huyo,Kanumba alikuwa akitegemewa na familia yake kupitia kazi za filamu ambapo sasa hivi kutokana na kutokuwepo kwake familia hiyo itayumba.

Aliongeza kuwa endapo CD hizo zitaweza kusimamiwa vizuri pato lake litaingia kwenye familia na kuweza kuendesha maisha yao ya kila siku badala ya jasho hilo kufaidiwa na watu wengine.
Kwa upande mwingine Mwakifamba alisema msiba wa Kanumba ni pigo kwa tasnia ya filamu kutokana na namna msanii huyo alivyoweza kuitangaza  Tanzania kupitia kazi zake na kuongeza kuwa  TAFF itamkumbuka kwa mambo mengi,kwani mbali na kuwa mwanachama kupitia chama cha Waigizaji Kinondoni, pia alikuwa mjumbe wa kamati ya TAFF ya kuandaa mapendekezo ya marekebisho kanuni ya sheria za filamu za mwaka 2011.
Vilevile Kanumba alikuwa ni mmojawapo wa wafadhili wa Shirikisho hilo ambapo alikuwa mchango mkubwa katika kuleta umoja na mapinduzi ya kweli katika tasnia ya filamu.

No comments:

Post a Comment