Thursday, November 22, 2012

MUUMINI AENDELEA KUTANGA TANGA, AIHAMA TENA TWANGA SASA AKIMBILIA VICTORIA SOUND

Muumin Mwinjuma(kulia) akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu kuhama  bendi ya African Stars(Twanga Pepeta) na kujiunga na Bendi ya Victoria Sound.  Kushoto ni Meneja wake, Abdulfarid Hussein na Mkurugenzi wa Victoria Sound Daniel Denga Mjema.
Mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi mwenye sifa kubwa ya kutotulia kwenye bendi moja kwa muda mrefu, Mwinjuma Muumini ambae alitamba miaka ya 90 na nyimbo kama Tunda akiwa na Tamtam sound iliyokuwa inamilikiwa na ASET, na baadae kuihama bendi hiyo na hatimaye kuzunguka kwenye bendi tofauti tofauti ambapo mwaka jana aliamua kurudi kwenye kampuni ya ASET na kujiunga na Bendi ya African Stars (Twanga pepeta), jana ametangaza tena kujiengua kwenye bendi hiyo na kujiunga na bendi changa ya Victoria Sound.

Akizungumza na blog hii jana, Muumini alisema ameamua kuihama bendi hiyo kubwa na kuhamia kwenye bendi hiyo changa ambayo haifahamiki na hata watu 20 ingawa imeanzishwa miaka mitano iliyopita kwa kuwa anaangalia zaidi maslahi na uhuru wa kufanya kazi kuliko kuwa kwenye bendi kubwa ambayo haijampa mkataba na maslahi madogo.

Aidha Muumini aliwataka mashabiki wake kumuelewa na kutomfikiria vibaya kwani kuhama kwake hakuathiri chochote kazi yake ila anaboresha zaidi kazi yake, hivyo mashabiki wakae mkao wa kula ili kupokea kazi zake mpya ambazo anatarajia kuzitoa mwakani akiwa na bendi hiyo ya victoria, ambapo hivi sasa yuko mapumzikoni kwa ajili ya kujipanga kwa mashambulizi mwakani.

Nakumbuka mara baada ya kurudi Twanga niliongea na Muumini kupitia kipindi changu(Afrobeat) ambapo alijigamba kuwa sasa amefika kweli kama ambavyo aliwahi kuimba miaka ya nyuma na kamwe hawezi kuihama bendi hiyo mpaka pale atakapostaafu muziki, nimeshangaa kusikia eti amehama tena, namshauri ajiangalie nafikiri hicho anachofanya ni kitendo cha kujimaliza mwenyewe kwa kuua kipaji chake na kujishushia heshima kwa mashabiki, sitoshangaa nikisikia baada ya miezi kadhaa anatangaza tena kuihama bendi hiyo kwa visingizio kibao visivyo na msingi.

No comments:

Post a Comment