Friday, May 24, 2013

VURUGU ZA MTWARA YAIBUKA MAPYA, ASKARI POLISI WATUHUMIWA KUMUUA MJAMZITO KWA RISASI, KUWABAKA WANAWAKE, KUVAMIA MAKAZI YA WATU NA KUPORA MALI



Hali ya usalama katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara imezidi kuwa mbaya baada ya askari polisi kudaiwa kufanya unyama kwa kuwabaka wanawake na kumpiga risasi mjamzito.
Mbali na unyama huo polisi pia wanadaiwa kuchoma moto nyumba tatu za wananchi katika mtaa wa Magomeni na  maduka kadhaa na kupora vitu vilivyomo ndani ya maduka hayo.

Hata hivyo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa amesema hali ni shwari na kwamba wananchi watoke nje kuendelea na shughuli zao za kila siku kama kawaida naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Mohamedi Kodi amethibitisha kupokea mwili wa mjamzito ukiwa na tundu tumboni, zinazoaminika kuwa za risasi na hivyo kufanya idadi ya maiti zilizopokelewa hospitalini hapo kufikia mbili na majeruhi 18: 

“Ni kweli kwa leo( jana) tumepokea maiti moja ya mwanamke ambaye ni mjamzito wa miezi saba, amepigwa risasi tumboni pia tumepokea mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Chuno, amevunjwa miguu yote kwa risasi.” 

 Habari zinadai kuwa mjamzito huyo ameuawa akiwa nyumbani kwake baada ya polisi kuvamia makazi yake. Huduma za kijamii zimesimama, hakuna maduka yaliyo wazi, hakuna usafiri wa daladala wala pikipiki, mji upo kimya, sauti za milio ya mabomu na bunduki zimetawala, wanajeshi waliovalia sare wameuzingira mji wakiwa katika magari na pikipiki. 

Wakizungumza na Waandishi wa Habari kwa nyakati tofauti wakazi wa mji huo wamelalamikia kitendo cha askari wa jeshi la polisi kuingia katika makazi yao, kuwapiga, kuwabaka na kuwapora mali zao: 

“Wakazi waMagomeni A hatuna amani askari wanaingia majumbani mwetu wanatupiga na kutunyang’anya simu, yani huku Magomeni hatuna amani kabisa, tumepoteza watoto na hatujui hata waume zetu wako wapi”alisema Paulina Idd na kuongeza: “Majumba yetu yamechomwa moto , wanaofanya fujo ni polisi wenyewe halafu wanakuja wanatubaka na kuiba mali zetu halafu tunateseka sisi yaani tumechoka kabisa na serikali yenyewe,” aliongeza Paulina.



Habari zaidi zinasema kuwa wanawake na watoto wameyakimbia makazi yao na kukimbilia katika Hospitali ya Mkoa Ligula Mkoani Mtwara(kama unavyoona pichani) kwa ajili ya kuomba hifadhi wakihofia usalama wao.

Kamanda Sinzumwa alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa atapingana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi aliyewasili Mtwara leo(jana): Kuhusiana na suala hilo siwezi kulizungumzia kwa sasa kwani nitapingana na Waziri wangu kwani leo(jana) ametoa tamko bungeni na leo(jana) atawasili,” alieleza Sinzumwa.


Juhudi za kumtafuta Kamanda Sinzumwa ziliendelea asubuhi hii na alipotafutwa majira saa 4 kasorobo asubuhi alidai kuwa yupo kwenye kikao na WAZIRI wa mambo ya ndani, Mh. Emmanuel Nchimbi hivyo atafutwe baada ya kikao hicho ambacho hakusema kinamalizika saa ngapi..




No comments:

Post a Comment