Monday, May 20, 2013

FLAVIANA MATATA KUSHIRIKI KATIKA MISA YA KUMBUKUMBU YA MV BUKOBA

Mwanamitindo wa kimataifa wa Tanzania, Flaviana Matata(Pichani) kesho atashiriki katika misa maalum ya kuwakumbuka watanzania waliopoteza maisha katika ajali ya MV Bukoba mwaka 1996.
Misa hiyo itafanyika kwenye eneo la makaburi ya kumbukumbu ya MV Bukoba ambapo Flaviana alipoteza mama yake mzazi na kaka yake katika ajali hiyo.
Mwaka jana, mwanamitindo huyu kupitia shirika lake la Flaviana Matata Foundation alitoa msaada wa maboya yaani vyombo vya kuokoa maisha majini (life vests) 500 kwa mawakala wa meli ya serikali yaani Marine Services Ltd ikiwa ni njia moja ya kujaribu kusaidia usalama majini.
Mkurugenzi wa kampuni ya Compass Communications, Maria Sarungi alisema kuwa mbali ya kushiriki katika misa hiyo, pia mwana mitindo huyo atafanya mazungumzo na wadau mbali mbali kuhusu jinsi ya kuendeleza juhudi za kuimarisha usalama majini.
Flaviana amesema kuwa juhudi zake kubwa kwa hivi sasa ni kuhakikisha kuwa ajali za vyombo vya majini zinaepukika na ndiyo maana anapigana huku na kule katika sakata hilo.
Ameongeza kuwa lengo lake kubwa ni kuona vyombo vya kuokolea katika kila meli vinapatikana na hasa kwa kutafuta misaada kwa wadau mbali mbali.
“Suala la usalama majini bado haujatiliwa mkazo vya kutosha na jamii pamoja na serikali” alieleza mwanamitindo huyu na kuongeza kuwa “Muda umefika kwa wahusika wote kushirikiana kwa pamoja kuzungumzia na kukabiliana na changamoto hii” .

No comments:

Post a Comment