Friday, May 31, 2013

MWILI WA MAREHEMU ALBERT MANGWEA UTAWASILI DAR ES SALAAM JUMAPILI BADALA JUMAMOSI

Mwili wa marehemu Albert Mangwea utawasili Jumapili badala ya Jumamosi kama ambavyo ilipangwa hapo awali.

Kwa mujibu wa kamati ya maandalizi ya msiba huo kupitia ,semaji wake Adam Juma ni kuwa, maamuzi hayo yametokana na maombi ya watanzania waishio nchini Afrika kusini kuomba kuuaga mwili wa marehemu hapo kesho.

Kufuatia mabadiliko hayo mwili wa marehemu utawasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwl. J.K Nyerere siku hiyo ya Jumapili majira ya saa 7.30 mchana ambapo mashabiki, ndugu, jamaa na marafiki wa Mangwea watapata nafasi ya kuuaga mwili Jumatatu kuanzia saa 2 asubuhi mpaka saa 6 mchana katika viwanja vya Leaders Club na baadae safari ya kuelekea Morogoro kwa mazishi itaanza ambapo atazikwa siku ya Jumanne.

Hivyo ndugu, jamaa, marafiki na mashabiki wa Mangwea mnaombwa kujitokeza kwa wingi uwanja wa ndege ili kuupokea mwili wa marehemu na katika viwanja Leaders Club ili kuuaga mwili wa ndugu yetu, kipenzi chetu Albert Mangwea.

KAA TAYARI KUIPOKEA VIDEO SURGERY ITAKAYOKUJIA HIVI KARIBUNI


VIDEO SURGERY, Show mpya ambayo itaanza kuwa published Youtube, Mpango na lengo lake kubwa likiwa ni kujenga na kuboresha kazi mbalimbali za videos zinazofanya na wasanii, hususan Music Videos, Kwa kushirikisha wataalam wa Video Production kwa karibu pamoja na maoni ya kwako wewe mkali wetu, tutakuwa tunachambua videos ambazo kwa mwanzo huu tutakuwa tunazichagua sisi na kuhighlight mambo yoote ambayo yamefanyika vizuri katika video hiyo na pia tutakuchana kinomanoma pale ambapo tutakuwa tumeona makosa dhahiri, lengo kubwa likiwa ni kuwachallenge wasanii kufanya kazi bora zaidi kwa mashabiki wao.

Presenters wa show ni Kennedy Frank Remedy [@KenedyFrank] na Fadhili Kiwia [Mo_Faze] chini ya Director mkali Edson Kato 2.5D [.....], Mpango ndio umekaa hivi na maoni na support yako ni muhimu sana katika kufanikisha hili.

Find and Like us on Facebook kupitia link hii https://www.facebook.com/VideoSurgery na pia twitter kupitia https://twitter.com/CreativemindsTZ na pia blogspot http://videosurgerytz.blogspot.com/.

Cheki hapa Episode ya kwanza kabisa ya show hii;

2


Kwa followup Subscribe youtube channel https://www.youtube.com/user/creativemindstz?feature=watch

SERIKALI KUWAWEZESHA WAGONJWA KUTAMBUA DAWA FEKI KWA KUTUMIA SIMU ZA MKONONI


Katika juhudi za kukabiliana na ongezeko la dawa feki za binadamu serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na kampuni ya kimataifa ya kutengeneza dawa baridi ya Glaxo Smith Kline imezindua mpango utakaowezesha wagonjwa kutambua ubora wa dawa kupitia simu za mkononi.
Akizungumza na wadau wa sekta ya Afya Naibu waziri wa Afya Mh. Seif Rashid (pichani), amesema mpango huo unalenga kuiongezea nguvu serikali katika jitihada za kufikiwa kwa malengo ya millennia pamoja na kuleta mageuzi katika utoaji wa huduma katika sekta ya afya na kuwawezesha wananchi kuwa na uhakika wa dawa wanazozitumia.
Mkurugenzi wa Udhibiti wa Nchi zinazoendelea wa kampuni ya Kimataifa ya Glaxo Smith Kline Dkt. William Mwatu amesema utafiti uliofanywa katika nchi za Kenya na Tanzania umeonyesha kuwa wagonjwa wengi wamekuwa na hofu wa dawa wanazotumia.
Mh. Seif Amesisitiza kuwa asilimia 30 ya dawa zilizo katika maduka ya dawa baridi ni feki, kiwango ambacho kinatarajiwa kuongezeka kwa asilimi 13 kwa mwaka.

BARAZA LA MITIHANI LATANGAZA MATOKEO KIDATO CHA 6


Baraza la mitihani Tanzania, leo limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha sita uliofanyika mwezi February mwaka huu..
Akitangaza matokeo hayo katika ofisi za baraza hilo Mikocheni jijini DSM, Naibu katibu mtendaji wa baraza hilo Dr. Charles Msonde amesema Jumla ya watahiniwa wa shule 40,242 kati ya watahiniwa 42,952 sawa na asilimia 93.92 wamefaulu kwa daraja la 1 hadi la nne.

Aidha Dr msonde ametaja shule 10 bora, zilizoongozwa na Marian Girls ya Pwani katika kundi la watahiniwa zaidi ya 30 ambazo ni Mzumbe Secondary school, Feza Boys, Ilboru, Kisimiri, St. Mary's Mazinde juu, Tabora Girls, Igowole, Kibaha Secondary school na Kifungilo Girls.

Pia ametaja watahiniwa waliofanya vizuri katika masomo mbalimbali, Kwa upande wa Sayansi aliyeongoza ni Erasmi Inyanse aliyekuwa akisoma PCM kutoka Ilboru shule ya Arusha, kwa masomo ya biashara wa kwanza ni Erick Robert Mulogo kutoka Tusiime ya DSM kombi ya ECA, na kwa masomo ya lugha na sayansi ya Jamii ni Asia Idd Mti kutoka Barbro-Johansson ya DSM alikuwa akisoma HGE.

Monday, May 27, 2013

FEZA KESSY NA NANDO WAWAKILISHI WA TANZANIA KATIKA SHINDANO LA BIG BROTHER 2013

Mwakilishi kutoka Tanzania Nando akihojiwa na Mtangazaji wa kipindi hicho Ik wakati wa uzinduzi wa show hiyo, Kushoto patna wa Nando Mshiriki kutoka Namibia Cleo.
Mwakilishi mwingine kutoka Tanzania Feza Kessy, akitambulishwa kwa patner wake kutoka Ghana Elikem wakati wa uzinduzi wa shinado hilo.
Feza Kessy akiwasalimia mashabiki waliojitokeza katika uzinduzi wa shindano hilo.

Kile kitendawili cha nani ataiwakilisha Tanzania katika shindano la Big Brother The chase 2013, kimeteguliwa jana katika uzinduzi wa shindano hilo uliofanyika jana jijini Johannesburg Afrika ya Kusini huku Tanzania ikiwakilishwa na Feza Kessy na Nando.

Wengi wameonyesha kustaajabu baada ya kuwaona washiriki hao kinyume cha matarajio ya wengi ambapo magazeti mbalimbali yaliripoti kuwa mastaa Wema Sepetu, Baby Madaha au Jackline Pentzel ndiyo wangeiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo mwaka huu ingawa wahusika wenyewe walipoulizwa walikanusha madai hayo.

Kila la kheri Feza na Nando tunaamini ushindi utarudi Tanzania.  

MICHEZO YA UMISETA YAZINDULIWA LEO HII MKOANI LINDI

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa Afisa elimu, Taaluma Mkoa wa Lindi Bwana Sarufu Kakama (pichani juu)
Sehemu ya wanamichezo 640 kutoka katika Halmashauri 6 za Wilaya zinazounda Mkoa wa Lindi.

Ufunguzi wa mashindano ya Umoja wa Michezo na Sanaa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) mkoani Lindi umefanyika rasmi leo katika Viwanja vya shule ya sekondari Lindi.

Uzinduzi huo wa michezo ya Umiseta iliyojumuisha wanamichezo 640 kutoka katika Halmashauri 6 za Wilaya zinazounda Mkoa wa Lindi ambapo mashindano hayo ya michezo hiyo yanafanyika kwa siku nne mfululizo huku yakitoa fursa ya kuchagua wanamichezo watakaoshiri katika michezo hiyo Kanda ya Kusini.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo Ambae pia ni afisa elimu Taaluma Mkoa wa Lindi,Sarufu Kakama amesisitiza wanamichezo wote kucheza na kushindana bila kuumizana na kucheza kwa upendo na kuzingatia nidhamu kama ambavyo wawapo mashuleni mwao ili kujenga mshikamano baina ya wao kwa wao ikiwemo na walimu wao.

Aidha Kakama alieleza mkoa wa Lindi ulivyojipanga katika michuano hiyo iliyoanza leo ngazi ya mkoa kuelekea kanda itakayofanyika Hivi karibuni mkoani humo
Nae Kaimu Afisa Utamaduni Manispaa ya Lindi,Mwl Alice Choaji licha ya kuelezea michezo kama masomo mengineyo na kwa kuzingatia somo hilo kwasababu michezo ni ajira, michezo hutatua migogoro katika jamii mbalimbali, michezo hudumisha utamaduni wa nchi na makabila mbalimbali ikiwemo kuibua vipaji vya watoto alieleza.

Katika  mashindano hayo kuna jumla ya michezo saba ikiwemo soka wavulana na wasichana, netiboli kwa wasichana, riadha wavulana na wasichana kuanzia mita 100 hadi 5000, basketiboli wavulana na wasichana, wavu wavulana na wasichan na tufe ambapo michezo hiyo itakuwa kifanyika kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi 11:30 jioni kwenye viwanja hivyo vya Lindi Sekondari na Mtanda kwa Mpira wa Miguu

SOURCE:Abdul Aziz video-Lindi

Friday, May 24, 2013

VURUGU ZA MTWARA YAIBUKA MAPYA, ASKARI POLISI WATUHUMIWA KUMUUA MJAMZITO KWA RISASI, KUWABAKA WANAWAKE, KUVAMIA MAKAZI YA WATU NA KUPORA MALI



Hali ya usalama katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara imezidi kuwa mbaya baada ya askari polisi kudaiwa kufanya unyama kwa kuwabaka wanawake na kumpiga risasi mjamzito.
Mbali na unyama huo polisi pia wanadaiwa kuchoma moto nyumba tatu za wananchi katika mtaa wa Magomeni na  maduka kadhaa na kupora vitu vilivyomo ndani ya maduka hayo.

Hata hivyo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa amesema hali ni shwari na kwamba wananchi watoke nje kuendelea na shughuli zao za kila siku kama kawaida naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Mohamedi Kodi amethibitisha kupokea mwili wa mjamzito ukiwa na tundu tumboni, zinazoaminika kuwa za risasi na hivyo kufanya idadi ya maiti zilizopokelewa hospitalini hapo kufikia mbili na majeruhi 18: 

“Ni kweli kwa leo( jana) tumepokea maiti moja ya mwanamke ambaye ni mjamzito wa miezi saba, amepigwa risasi tumboni pia tumepokea mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Chuno, amevunjwa miguu yote kwa risasi.” 

 Habari zinadai kuwa mjamzito huyo ameuawa akiwa nyumbani kwake baada ya polisi kuvamia makazi yake. Huduma za kijamii zimesimama, hakuna maduka yaliyo wazi, hakuna usafiri wa daladala wala pikipiki, mji upo kimya, sauti za milio ya mabomu na bunduki zimetawala, wanajeshi waliovalia sare wameuzingira mji wakiwa katika magari na pikipiki. 

Wakizungumza na Waandishi wa Habari kwa nyakati tofauti wakazi wa mji huo wamelalamikia kitendo cha askari wa jeshi la polisi kuingia katika makazi yao, kuwapiga, kuwabaka na kuwapora mali zao: 

“Wakazi waMagomeni A hatuna amani askari wanaingia majumbani mwetu wanatupiga na kutunyang’anya simu, yani huku Magomeni hatuna amani kabisa, tumepoteza watoto na hatujui hata waume zetu wako wapi”alisema Paulina Idd na kuongeza: “Majumba yetu yamechomwa moto , wanaofanya fujo ni polisi wenyewe halafu wanakuja wanatubaka na kuiba mali zetu halafu tunateseka sisi yaani tumechoka kabisa na serikali yenyewe,” aliongeza Paulina.



Habari zaidi zinasema kuwa wanawake na watoto wameyakimbia makazi yao na kukimbilia katika Hospitali ya Mkoa Ligula Mkoani Mtwara(kama unavyoona pichani) kwa ajili ya kuomba hifadhi wakihofia usalama wao.

Kamanda Sinzumwa alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa atapingana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi aliyewasili Mtwara leo(jana): Kuhusiana na suala hilo siwezi kulizungumzia kwa sasa kwani nitapingana na Waziri wangu kwani leo(jana) ametoa tamko bungeni na leo(jana) atawasili,” alieleza Sinzumwa.


Juhudi za kumtafuta Kamanda Sinzumwa ziliendelea asubuhi hii na alipotafutwa majira saa 4 kasorobo asubuhi alidai kuwa yupo kwenye kikao na WAZIRI wa mambo ya ndani, Mh. Emmanuel Nchimbi hivyo atafutwe baada ya kikao hicho ambacho hakusema kinamalizika saa ngapi..




Thursday, May 23, 2013

HALI MKOANI MTWARA YAENDELEA KUWA TETE, RAIS ATOA TAMKO, BUNGE LAAHIRISHWA TENA WATU 91 WATIWA MBARONI

Wakati hali ikizidi kuwa tete Mkaoni Mtwara kufutia vurugu ziliyoanza jana Mkoani hum,o Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ametoa amri  kwa Jeshi la olisi kuhakikisha wahusika wote wa vuugu hizo kusakwa na kutiwa nguvuni mara moja.
 Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa barabara kuu ya Iringa-Dodoma katika eneo la Kizota mkoani Dodoma  Rais Kikwete  alisema wote waliohusika na vurugu hizo watasakwa na kuchukuliwa hatua kali.
Rais Kikwete alisema rasilimali inayopatikana mahali popote pale nchini inatakiwa kutumiwa na Watanzania wote.
Wakati huo huo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Anna Makinda ameliahirisha tena bunge leo asubuhi baada ya jana jioni kuitaka Serikali ije na ripoti ya tukio hilo ambapo leo ameitaka kamati ya uongozi ya Bunge iendelee kukutana ili kutoa maamuzi na tamko kuhusu vurugu hizo zinazoendelea Mkoani humo na kusababisha kifo cha mtu mmoja na uharibifu wa mali ikiwemo kuchomwa moto kwa nyumba za viongozi wa serikali,chama cha mapinduzi na nyumba ya mwandishi wa habari wa TBC Kassim Mikongoro.
Hata hivyo mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini umesimamishwa kwa muda mpaka ufumbuzi wa tatizo la vurugu hizo utakapopatiwa ufumbuzi ambapo Kesho Bunge litajadili bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya Afrika Mashariki.
Aidha Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara ACP Linus Sinzumwa amesema Jeshi la polisi mkoani humo linawashikilia watu 91 kwa tuhuma za kuhusika na vurugu hizo na hatua itakayofuata ni kufanya nao mahojiano ili kubaini chanzo cha vurugu hizo na kuongeza kuwa Jeshi la Polisi limejipanga ili kudhibiti vurugu hizo na kurejesha hali ya amani.

Wednesday, May 22, 2013

HALI YA USALAMA MKOANI MTWARA IMEENDELEA KUWA MBAYA KUTOKANA NA VURUGU ZINAZOENDELEA MKOANI HUMO

MAPAMBANO kati ya Askari wa Jeshi la Polisi na Wananchi wa Mkoa wa Mtwara umefika katika hatua mbaya,kiasi cha mtu mmoja kudaiwa  kujeruhiwa vibaya baada ya kurushiwa bomu wakati wa mashambulizi hayo katika eneo la Magomeni.
Mbali na kujeruhiwa kwa mtu huyo aliyekuwa katika maandamano ya kupinga Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, Ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pia imechomwa moto. 
Taarifa zilizonaswa na Fahari ya Kusini hivi punde zinadai kwamba wananchi wa Mkoa wa Mtwara wamefungiwa majumbani tangu asubuhi, huku Jeshi la Polisi likifanya msako wa nyumba hadi nyumba kwa lengo la kuwanasa watuhumiwa wanaodaiwa kuchochea maandamano hayo kwa njia ya vipeperushi. 

Shuhuda wa wa tukio hilo ameitaarifu Fahari ya kusini  kwamba waandamanaji hao wameapa kufa endepo serikali itaendelea na mipango yake ya kusafirisha gesi hiyo hadi Jijini Dar es Salaam. "Hali hapa ni mbaya, tangu asubuhi wananchi wote wamefungiwa ndani ya majumba yao, hakuna anayeruhusiwa kutoka nje, Polisi wanapiga mabomu ya machozi kila mtaa huku wakiwasaka watuhumiwa waliosambaza vipeperushi na kuwatawanya wandamanaji waliozagaa katika mitaa  mbalimbali, mpaka hivi sasa kuna mtu mmoja ameripotiwa kujeruhiwa vibaya katika mashambulizi ya raia na Asakari Polisi wanaotumia mabomu ya machozi na silaha zigine za moto"alisema shuhuda wa tukio hilo. 
Hata hivyo imedaiwa kuwa hali hiyo imesababisha barabara zote kufungwa kiasi cha kuzuia mabasi yanayoingia na kutoka katika mji huo toka asubuhi, kuna baadhi ya mitaa matairi yamechomwa moto barabarani, magari ya FFU yametanda kila kona za mji, huku taarifa zaidi ikifafanua kwamba hakuna mawasiliano, milio ya mabomu inasikika kila kona na hali ya utulivu sio ya kuridhisha, Askari wa zima moto wamesambaa kuzima moto na kuna baadhi ya nyumba maeneno ya Shangani zimechomwa moto.  Nyumba ya mwandishi wa Habari wa TBC kassim Mikongoro inasemekana Imechomwa moto mchana huu.Hali ni tete Askari wawili na raia mmoja wanasadikika kuuawa.
Wakati huo huo Spika wa Bunge la Jmhuri wa Muungano wa Tanzani Anne Makinda ameahirisha Kikao cha Bunge mpaka kesho ambapo ameiagiza serikali kuja  taarifa kamili kuhusiana na vurugu zinazoendelea huko  Mtwara.

SOURCE:Lindiyetu.blogspot.com

Tuesday, May 21, 2013

PROFESSOR JAY AJIUNGA RASMI CHADEMA AKABIDHIWA KADI MUDA MFUPI ULIOPITA

Msanii mkongwe wa muziki wa kizazi kipya nchini, Joseph Haule (Professor Jay) amejiunga rasmi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA).

Pichani ni Mheshimiwa Joseph Mbilinyi(Sugu) Mbunge wa Mbeya mjini kupitia CHADEMA akimkabidhi msanii huyo kadi ya Chama hicho muda mfupi uliopita mjini Dodoma.

Mpaka sasa tunafanya jitihada za kuzungumza na Prodessor Jay mwenyewe ili kupata maelezo zaidi kuhusiana na hatua yake hii Endelea kutembelea Blog hii ili kufahamu alichokisema.

BAADHI YA PICHA ZA WALIOMUUNGA MKONO LADY JAYDEE SIKU YA LISTERNING PARTY YA ALBUM YAKE YA SITA

KAULI YA CCM BAADA YA TAARIFA KUWA MWENYEKITI WA CHAMA HICHO TAIFA, RAIS KIKWETE AMERUHUSU WANAOKUSUDIA KUGOMBEA URAIS 2015


Mei 19, 2013 Chama Cha Mapinduzi kilifanya kikao cha siku moja na wabunge wanaotokana na CCM, kikao hicho kilifanyika mjini Dodoma ambapo pamoja na viongozi wengine wa juu wa CCM kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Kikao hicho kilikuwa na lengo la wabunge wa CCM na viongozi wa CCM wakiongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM ambaye pia ni Rais na mtekelezaji mkuu wa Ilani ya uchaguzi ya CCM kubadilishana uzoefu wa namna ilani ilivyotekelezwa hasa kwenye majimbo kwa kipindi cha nusu ya muhula wa miaka mitano. Baada ya kubadilishana mawazo uliwekwa mwelekeo wa namna bora ya kutekeleza ilani na ahadi mbalimbali kwa kipindi kilichobaki.

Kwahiyo kwa kifupi lengo la kikao hicho ilikuwa ni kutathimini utekelezaji wa ilani majimboni na kuangalia namna bora ya kuweka msukumo mpya na mkubwa zaidi kwa kipindi kilichobaki cha utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa 2010/2015, lengo likiwa kuhakikisha ilani na ahadi za CCM na wagombea wake zinatekelezwa kwa kiwango kikubwa.

Hata hivyo baada ya semina hiyo baadhi ya vyombo vya habari vimenukuu kauli inayodaiwa kutolewa na Mwenyekiti wa CCM Dr. Jakaya Kikwete kuwa ameruhusu wanaokusudia kuomba ridhaa ya CCM kugombea Urais wa 2015 kufanya kampeni.

CCM imesikitishwa na nukuu hiyo ya kupotosha ukweli wa kilichojadiliwa na hivyo tumelazimika kutoa ukweli wa kilichojiri na kujadiliwa. Ni kweli kuwa mjadala juu ya watu mbalimbali wanaotajwa au wanaojitaja kuwa na nia ya kugombea nafasi mbalimbali hasa udiwani, ubunge na Urais ulikuwepo na ulikuwa mkali.

Hata hivyo hitimisho la kikao na majumuisho ya Mwenyekiti wa CCM Taifa lilikuwa ni kukemea kwa nguvu zote pirika hizo na uvunjifu huu wa makusudi wa kanuni za Chama chetu ambazo kimsingi pirika hizi zinakigawa Chama na kuvuruga mshikamano na umoja ndani ya Chama.

Nasisitiza nukuu hiyo ya baadhi ya vyombo vya habari si sahihi na ni ya kupotosha ukweli. Inaelekea kuna kikundi cha watu wanamgombea wao wa kuchonga ambaye bila shaka anapungukiwa na sifa, hivyo wanajaribu kumuongezea sifa kwa kumlisha Mwenyekiti maneno na kuwaapa baadhi ya waandishi, uhuni huo haukubaliki.

CCM ina kanuni na taratibu zake zinazoisimamia na kuiongoza katika kufanya shughuli zake mbalimbali zikiwemo za mchakato wa kuwapata wagombea wake katika ngazi mbalimbali kuanzia shina hadi taifa.

Kanuni hizo ni pamoja na kanuni za Uteuzi wa wagombea wa CCM kuingia katika vyombo vya dola toleo la Februari, 2010 na Kanuni za uchaguzi wa CCM, toleo la 2012.

Katika Kanuni za Uchaguzi wa CCM Toleo la 2012 kanuni za jumla Ibara ya 33 inazungumzia Miiko ya kuzingatiwa wakati wa shughuli za uteuzi na uchaguzi. nanukuu“ Maadili na nidhamu ya chama katika kusimamia na kutekeleza shughuli za uchaguzi wa chama lazima kuzingatiwa na wale wote wanaohusika. Hivyo yawapasa kuelewa na kutambua kuwa;-
(1). “….wanachama wenye nia ya kugombea hawaruhusiwi kufanya kampeni ya aina yoyote kabla ya majina yao kuteuliwa na kikao kinachohusika”.

(4). “Ni mwiko kwa kiongozi au mwanachama yeyote wa CCM kuunda vikundi visivyo rasmi ndani ya chama, au kushiriki katika kampeni za uchaguzi za chini chini kinyume na ratiba ya uchaguzi na taratibu rasmi zilizowekwa”.

Ibara hiyo ya 33 kifungu kidogo cha 1 na 4 vinaweka wazi msimamo wa kikanuni wa Chama. Hivyo basi kwa mujibu wa kanuni za Uteuzi wa wagombea wa CCM kuingia katika vyombo vya dola toleo la Februari, 2010 na Kanuni za uchaguzi wa CCM, toleo la 2012 na kwa mujibu wa maagizo yaliyotolewa na kupokelewa kwenye kikao cha Mwenyekiti wa CCM Taifa na wabunge wa CCM mjini Dodoma tarehe 19/05/2013;
Ni marufuku kwa mwanachama yeyote wa CCM anayetaka kuomba CCM impe nafasi ya kugombea kwenye uchaguzi wa dola kujipitishapitisha na kuita wapiga kura na kukutana nao kinyume na kanuni za Chama. Hatua kali zitachukuliwa kwa mwana CCM yeyote atakaye kiuka agizo hili.
Lakini pia ni marufuku kwa viongozi na watendaji wa Chama kujihusisha na kuwakusanyia wapiga kura watu hao wenye nia ya kugombea kupitia CCM kwenye uchaguzi wa dola. Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya viongozi na watendaji wote watakao kiuka agizo hili la Chama.

Tunawataka wote wenye nia, viongozi na watendaji wa CCM kuzingatia agizo hili, ili tusije laumiana mbele ya safari.

Imetolewa na;-

Nape Moses Nnauye
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi

SPIKA WA BUNGE AAMURU KUFUTWA KWA HOTUBA YA KAMBI YA UPINZANI ILIYOSABABISHA BUNGE LISITISHWE JANA ASUBUHI


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Anne Makinda, ameamuru kambi ya upinzani kuyaondoa maneno yote yaliyomo kuanzia ukurasa wa kwanza mpaka wa 14 katika hotuba rasmi ya Kambi ya upinzani iliyosmwa na mbunge wa Mbeya Mjini, Mh. Joseph Mbilinyi "Sugu" ambaye ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.

Mh. Makinda ametoa amri hiyo kufuatia kamati ya kanui ya Bunge kujadili hotuba hiyo na kubaini kuwa kauli za uchochezi na kusema kuwa Bunge siyo sehemu ya kugombanisha wananchi, hivyo maneno yote ya uchochezi hayaruhusiwi.
 
Katika hotuba hiyo, Mh. Mbilinyi aliishutumu serikali kuhusika na kuteka nyara waandishi wa habari, kauli iliyopelekea Spika Makinda kuahirisha Bunge.


Monday, May 20, 2013

WEMA SEPETU APATA DILI LA MAMILIONI KAMPUNI YA NYWELE "DARLING"

Miss Tanzania 2006 na muigizaji wa filamu Wema Sepetu amepata mchongo wenye pesa ndefu kutoka kampuni ya nywele ya Darling Hair Tanzania.
Kwa mujibu wa meneja wake, Martin Kadinda mkataba huo utamfanya Wema awe staa mwenye thamani kubwa zaidi Tanzania ingawa amesema si kawaida yao kutaja kiasi cha fedha
Deal hiyo itamuonesha Wema akiwa kama msemaji na sura wa Darling Hair Tanzania.
  
CHANZO : BONGO5.COM

MBUNGE WA IRINGA MJINI MCH. PETER MSIGWA AMEACHIWA KWA DHAMANA

Pichani juu ni Mchungaji Peter Msigwa akiikishwa mahakamani
Watuhumiwa wengine 60 wakishuka kwenye karandinga la Polisi kuelekea Mahakamani huku Polisi wakiimarisha ulinzi katika eneo hilo.

WATUHUMIWA 60 wa vurugu kati ya wamachinga na polisi mjini Iringa akiwemo Mbunge  wa  Jimbo  hilo, Mchungaji Peter Msigwa wameachiwa kwa dhamana baada ya walisomewa mashitaka matatu  huku mbunge  akisomewa shitaka la  kushawishi  watuhumiwa hao kufanya  vurugu.
  
Watuhumiwa  wote  wamekana mashitaka  dhidi yao na baadae utaratibu  wa dhamana  ukafanyika mbele  ya mahakama ya  hakimu mkazi  wa wilaya ya  Iringa, Mheshimiwa  Godfrey Isaya.
 
Mashitaka waliyosomewa watuhumiwa ni pamoja na shitaka la kwanza la mbunge ambalo ni kushawishi kufanya vurugu, huku  wengine  wote  makosa yao yakiwa ni kufanya mkutano bila kibali, kuharibu mali kinyume na sheria ni  kufanya  vurugu.

INDIA NA CHINA ZAAFIKIANA KUHUSU MPAKA

Waziri mkuu wa China (PICHANI KULIA) yupoNchini  India kwa ziara yake ya kwanza ya nje inayoonekana kugubikwa na mzozo wa muda mrefu wa mpaka kati ya nchi hizo mbili za bara la Asia.
Ziara ya waziri mkuu huyo wa China inajiri wiki kadhaa baada ya kuwepo malalamiko kutyoka kwa umma kufuatia India kukishutumu kikosi cha China kuingia ktika maeneo yake.

Zaidi ya miaka hamsini iliyopita tangu nchi hizo zilipopigana vita vya muda mfupi, bado nchi hizo hazijakubaliana kuhusu mipaka yao, na India inatuhumu China kwa kudhibiti sehemu kubwa ya ardhi yake.Mkwamo huo hatimaye ulitatuliwa kwa amani , lakini umezua mtazamo mwingine wa hatari inayotokana na mzozo kati ya nchi hizo mbili zenye idadi kubwa ya watu.
Waziri mkuu wa India alimpokea mwenzake wa China kwa tabasamu na waziri mkuu wa China akisisitiza kwamba lengo kuu la ziara yake ni kujenga imani kati ya nchi hizo mbili.
Aidha Li Keqiang amesema kuwa India na China lazima ziimarishe juhudi zake kutuliza mzozo wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili huku akiahidi kuunga mkono juhudi za amani na utulivu
SOURCE:BBC SWAHILI

FLAVIANA MATATA KUSHIRIKI KATIKA MISA YA KUMBUKUMBU YA MV BUKOBA

Mwanamitindo wa kimataifa wa Tanzania, Flaviana Matata(Pichani) kesho atashiriki katika misa maalum ya kuwakumbuka watanzania waliopoteza maisha katika ajali ya MV Bukoba mwaka 1996.
Misa hiyo itafanyika kwenye eneo la makaburi ya kumbukumbu ya MV Bukoba ambapo Flaviana alipoteza mama yake mzazi na kaka yake katika ajali hiyo.
Mwaka jana, mwanamitindo huyu kupitia shirika lake la Flaviana Matata Foundation alitoa msaada wa maboya yaani vyombo vya kuokoa maisha majini (life vests) 500 kwa mawakala wa meli ya serikali yaani Marine Services Ltd ikiwa ni njia moja ya kujaribu kusaidia usalama majini.
Mkurugenzi wa kampuni ya Compass Communications, Maria Sarungi alisema kuwa mbali ya kushiriki katika misa hiyo, pia mwana mitindo huyo atafanya mazungumzo na wadau mbali mbali kuhusu jinsi ya kuendeleza juhudi za kuimarisha usalama majini.
Flaviana amesema kuwa juhudi zake kubwa kwa hivi sasa ni kuhakikisha kuwa ajali za vyombo vya majini zinaepukika na ndiyo maana anapigana huku na kule katika sakata hilo.
Ameongeza kuwa lengo lake kubwa ni kuona vyombo vya kuokolea katika kila meli vinapatikana na hasa kwa kutafuta misaada kwa wadau mbali mbali.
“Suala la usalama majini bado haujatiliwa mkazo vya kutosha na jamii pamoja na serikali” alieleza mwanamitindo huyu na kuongeza kuwa “Muda umefika kwa wahusika wote kushirikiana kwa pamoja kuzungumzia na kukabiliana na changamoto hii” .

NGASSA AREJEA NYUMBANI YANGA ASAINI MKATABA WA MIAKA MIWILI

Mrisho Ngassa akizungumza na waandishi wa habari.
Pichani juu ni Mrisho Ngassa akikabidhiwa jezi ya Yanga na chini akibusu Jezi hiyo.
Habari zilizotufikia hivi punde zinasema Mchezaji wa zamani wa Young African sports Club (Yanga) Mrisho Khalfan Ngassa amerejea tena Yanga na tayari amesaini mkataba wa miaka miwili muda mfupi uliopita.

Ngassa ambae alihamia Simba August 2, mwaka jana kwa mkopo akitokea Azam FC baada ya timu hiyo kutangaza kuwa iko tayari kumuuza mchezaji huyo kwa timu yoyote itakayofikia dau la dola 50,000 ambapo Yanga ilikuwa tayari kumtwaa mchezaji huyo kwa dau la Tshs mil.20 huku watani wao Simba wakiwashinda kwa dau la mil.25 na kumtwaa mchezaji huyo.




MHESHIMIWA SUGU ACHAFUA HALI YA HEWA MJENGOZI

Spika wa bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Anna Makinda amesitisha kikao cha bunge na kuiruhusu kamati ya kanuni za bunge kuijadili hotuba ya bajeti ya kambi ya upinzani kuhusu wizara ya habari, utamaduni na michezo.

Hayo yametokea baada ya Mheshimiwa Joseph Mbilinyi (Pichani) kuanza kuwasilisha hotuba hiyo     ambayo imedaiwa kuwa na maneno ya uchochezi.

Bunge limeahirishwa mpaka saa 11 jioni ambapo kamati ya kanuni ya Bunge itakapoipitia hotuba ya bajeti ya kambi ya upinzani  na kujiridhisha kwamba haina maneno ya uchochezi.

Hii si mara ya kwanza  katika Bunge hili la mkutano wa 11 kusitisha hotuba za upinzani na kuitaka kamati ya kanuni ipitie upya.

Sunday, May 19, 2013

MBUNGE WA IRINGA MJINI ANATAFUTWA NA JESHI LA POLISI KWA TUHUMA KUSABABISHA VURUGU

Pichani ni Mbunge wa Iringa Mh. Peter Msigwa
Namna hali ilivyokuwa wakati vurugu zikiendelea mkoani Iringa

Jeshi la polisi mkoani Iringa linamtafutafuta Mbunge wa Iringa mjini kwa tiketi ya chama cha demokrasia na maendeleo(Chadema) Mh. Peter Msigwa kwa madai ya kuchochea vurugu kwa kuhamasisha wafanyabiashara ndogo ndogo mkoani humo maarufu kama wamachinga kufanya biashara katika eneo lisiloruhusiwa kwa shughuli hizo.

Watu zaidi ya 50 wanashikiliwa na polisi kwa kusababisha vurugu hizo ambazo pia  zimesababisha uharibifu wa gari la zimamoto.

Wednesday, May 15, 2013

D'BANJI APATA SHAVU LA KUWA BALOZI WA BENKI YA VIWANDA NIGERIA

Pichani ni mwanamuziki D'banji akiwa amesimama na Mkurugenzi mwendeshaji na Afisa mtendaji mkuu wa benki ya viwanda Nigeria bi. Evelyn Oputu.

Mwanamuziki nyota wa nchini Nigeria D'banj ameteuliwa kuwa balozi mpya wa benki ya viwanda huko Lagos, Nchini Nigeria.

Hii ni nafasi nyingine ya msanii huyo aliyepata umaarufu kwa ngoma zake kali kama vile Fall in Love, Oliver Twist na nyinginezo kula nafasi hiyo ambayo inamuweka katika nafasi nzuri zaidi kimataifa, ambapo baada ya kupata nafasi hiyo aliwajuza mashabiki wake kupitia account yake ya Twitter kuwa ametajwa kushika nafasi hiyo ya ubalozi wa benki hiyo.
 
Kila la kheri d'banji katika nafasi hiyo.

Tuesday, May 14, 2013

WANAFUNZI SHULE YA SEKONDARI MANZESE WAANGUKA NA KUPOTEZA FAHAMU

Mmoja kati ya wanafunzi walioanguka shuleni hapo 
Baadhi ya wanafunzi hao wakiwa katika hali mbaya.
Zaidi ya wanafunzi 40 wa shule ya sekondari Manzese jijini Dar Es Salaam, wameanguka na kupoteza fahamu wakiwa  shuleni  huku wengine wakitoka madarasani na kukimbia ovyo.

Tukio hilo limetokea leo majira ya saa nne asubuhi ambapo alianza mwanafunzi mmoja kupiga kelele na kuanguka wakati wakiendelea na masomo na baadae kutolewa nje ya darasa lakini jambo la kushangaza ghafla wanafunzi wengine zaidi ya 40 nao walianza kupiga kelele na kupigana kama watu waliorukwa na akili na kuanguka.

Hata hivyo wakati hayo yakiendelea uongozi wa shule hiyo uligoma kuzungumzia tukio hilo pale waandishi wa habari walipohitaji ufafanuzi wa tukio hilo.

WAREMBO 12 WAJITOKEZA KUWANIA MISS LINDI 2013, MEI 31

Zaidi ya warembo 12 wanatarajiwa kushiriki kwenye kinyang'anyiro cha kumsaka Malkia wa Mkoa wa Lindi ‘Miss Lindi 2013’ linalotarajia kufanyika Mei 31 mwaka huu katika ukumbi wa Hoteli ya Lindi Beach Resort (Lindi Oceanic Hotel).

Akizungumza na Blog hii kutoka mjini Lindi, Muandaaji wa Shindano hilo, Shaha Ramadhani kupitia kampuni ya Alliance Entertainment amesema warembo 12 wataingia Kambini Hotelini hapo chini ya Mkufunzi Zainab Mselemu ambaye alikuwa Miss Pwani 2010.

Maandalizi yote ya shindano hilo yanaendelea vyema na Milango iko wazi kwa Wadhamini kujitokeza.

Irene Veda (pichani juu) ndiye anashikilia taji hilo baada ya kulitwaa mwaka 2012. 

Monday, May 13, 2013

KIJANA WA MIAKA 21 AFIKISHWA MAHAKAMANI KESI YA BOMU ARUSHA

Mtuhumiwa mmoja kati ya tisa waliotiwa mbaroni na jeshi la polisi baada ya kutokea mlipuko wa bomu katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi amefikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka 21 ya mauaji na kujaribu kuua.

Victor Ambrose Calist (20) ambaye ni dereva wa bodaboda na mkazi wa eneo la Kwa Mromboo jijini Arushai amesomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu mkazi, Devotha Kamuzora.

Mtuhumiwa huyo anakabiliwa na mashtaka matatu ya mauaji ya watu watatu waliofariki dunia katika tukio ambalo lililotokea Mei 5, mwaka huu.

Mawakili wa serikali, Haruna Matagane na Zachariah Elisaria wanadai Calist pia anatuhumiwa kwa makosa 18 ya kujaribu kuua. Hata hivyo makosa mengine bado hayajatajwa..


Pia polisi imewaachia huru raia wanne wa kigeni waliokuwa wakishikiliwa kwa tuhuma za kuhusika katika tukio hilo baada ya uchunguzi uliofanywa na jeshi hilo kwa kushirikiana na FBI na polisi wa kimataifa (Interpol), kubaini hawakuhusika kurusha bomu katika kanisa hilo.