Thursday, January 24, 2013

WANANCHI WILAYANI RUFIJI WAVAMIA KITUO CHA POLISI NA KUCHOMA NYUMBA MOTO


Habari zilizotufikia hivi punde zinaeleza kuwa wananchi wenye hasira kali Kibiti Wilayani Rufiji mkoa wa Pwani leo, wamevamia kituo cha Polisi Kibiti na kuanzisha vurugu kubwa kufuatia mwananchi mmoja mkazi wa kijiji hicho kufariki dunia kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kutokana na kipigo cha Polisi.

Habari kutoka Kibiti zinasemakuwa, kijana huyo aliyefariki kutokana na kipigo hicho amefahamika Khamis Mpondi ambaye amepoteza maisha wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam, ambapo taarifa hiyo ilipowafikia wananchi wa kijiji hicho wakachukua uamuzi wa kwenda kituoni hapo na kuanzisha vurugu hizo.

Habari zaidi zinaeleza kuwa,baada ya kufanya vurugu katika kituo hicho cha polisi wakaendeleza vurugu zao kwa  kuteketeza nyumba za Askari Polisi zilizopo jirani kabisa na kituo hicho, licha ya juhudi za Polisi kuwatawanya kwa mabomu kuendelea kufanyika.

Mpaka taarifa hizi zinafika kwa blog hii wananchi hao walikuwa wamefunga barabara kuu ya Kilwa iendayo Mikoa ya Kusini, (Lindi na Mtwara) kwa mawe, magogo na kuchoma matairi ikiwa ni umbali unaokadiriwa kuwa ni wa kilometa moja kutoka kituo cha Polisi Kibiti.

Inaelezwa kuwa hali imezidi kuwa tete katika eneo hilo huku Polisi wa Kibiti wakiendelea na jitihada za kudhibiti hali hiyo kwa kufyatua mabomu ya machozi hewani kujaribu kutawanya umati huo wa watu.

tutaendelea kupeana taarifa zaidi kadri zitakavyokuwa zikitufikia.

No comments:

Post a Comment