Tuesday, January 29, 2013

CCM WAITAKA SERIKALI IWASIKILIZE WANANCHI WA MTWARA

Viongozi wa CCM wakizungumza na wananchi wa Uvinza-Kigoma

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM), kimesema kuwa wananchi wa Mtwara wanayo hoja hivyo Serikali inatakiwa kuwasikiliza na kutoa majibu sahihi.

Pamoja na hayo chama hicho kimesema kuwa kinachoonekana hivi sasa nyuma ya sakata hilo kuna watu wanafanya uhaini, uhalifu na kila aina ya hujumu jambo ambalo wanaitaka Serikali kuchukua hatua kali za kuhakikisha wote wanojihusisha na uhalifu huo wanachukuliwa hatua.

Kauli hiyo ilitolewa jana mjini kigoma na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana ikiwa ni msimamo wa chama chao katika sakata hilo.

Mjadala wa gesi ya Mtwara kutoka mkoani humo kwenda Dar es Salaam umekuwa gumzo kubwa huku wananchi wakiitaka Serikali kuwaeleza watanufaika vipi na gesi hiyo kabla ya kunufaisha maeneo mengine.

Kinana alisema kuwa kuna haja kwa Serikali kuhakikisha inatumia nafasi yake kuzungumza na wananchi wa Mtwara katika kupata suluhu ya suala hilo kwani wana hoja za msingi ambazo zinataka majibu.

“Msimamo wetu kama chama, tunataka Serikali kukaa na wananchi hao na kuwasikiliza.Tunahitaji kuona Serikali inatoa majibu ambayo yatakuwa sahihi na kumaliza tofauti iliyopo sasa,”alisema Kinana.

Pamoja na hayo alisema kuwa kinachoshangaza ni kuona hali ya uvunjifu wa amani inayofanywa na baadhi ya watu ambao wameamua kuingia mtaani na kuiba, kupora mali na kuharibu nyumba za watu kwa kuzichoma moto.

Alisema kuwa CCM inaona ni wakati mzuri kwa Serikali kuwadhibiti wote ambao wanatumia mwanya huo kufanya uhalifu huo ambao haukubaliki huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kusikilizwa.

Alisema mtazamo wa chama chao ni kwamba kuna jambo ndani ya suala hilo maana gesi inatakiwa kujadiliwa kwa njia ya amani kupata suluhu kuliko mali za watu kuharibiwa na kufanywa kwa uhalifu ambao hauvumiliki.

No comments:

Post a Comment