Tuesday, January 15, 2013

WALEMAVU WA NGOZI WALIA NA SERIKALI, WAITAKA IBAINI NJIA MPYA ZA MAUAJI DHIDI YAO


Chama cha Walemavu wa ngozi nchini kimelalamikia uendeshwaji wa kesi za watu wanaokamatwa kwa kuwadhuru, pamoja na kutokamatwa kwa kundi la waagizaji wakubwa wa viungo vya walemavu hali inayowapa mashaka juu ya usalama wao
.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ukumbi wa habari maelezo jijini Dar es salaam, Afisa Mahusiano na utetezi wa Chama cha Albino Nchini Bw. Joseph Torner amesema kwa uchungu kuwa, Kutokamatwa kwa kundi la tatu ambao ndio wanunuzi au waagizaji wa viungo vya Albino ni ishara kuwa tatizo hilo halitomalizika nchini


"Kesi ambazo zipo mahakamani mpaka sasa ni tano tu, wakati Albino waliouawa ni 70 na waliokamatwa ni waganga na wale wanaotekeleza matukio ya mauaji, je kundi ambalo ni waagizaji wa viungo hivi wako wapi wakati nchi yetu inasifiwa kwa upelelezi?" alisema bwana Torner


Aliongeza kuwa wanaiomba serikali iweke mikakati mipya, kwani hivi sasa wauaji wana mbinu zingine kiasi kwamba unaweza kuhisi mauaji hayapo lakini mauaji bado yanaendelea.
Aidha, Touner alilalamikia kitendo cha wanafunzi zaidi ya 139 wenye ulemavu wa ngozi katika shule ya Msingi Buhangija iliyopo manispaa ya Shinyanga kutorudi nyumbani wakati wa likizo kwa kuhofia usalama wao, ikiwa haijulikani ni lini watarudi kukutana na familia zao
.

" Wanafunzi wengi wenye ulemavu wa ngozi wamejikuta wakiwa kwenye kambi kila inapofika kipindi cha likizo kitendo ambacho kinaleta simanzi kwa familia za watoto hao, kwani hawajui ni lini watakutana na familia zao" Alisema Touner


Tangu mwaka 2006 mpaka hivi kumekuwa na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi hapa nchini licha ya serikali kuweka usalama kwa watu hao.

No comments:

Post a Comment