Tuesday, January 29, 2013

YALIYOJIRI KATIKA KIKAO CHA KUTAFUTA SULUHU KILICHOENDESHWA NA WAZIRI MKUU HUKO MTWARA


Waziri Mkuu Mizengo Pinda akisisitiza jambo wakati wa kikao chake na Baadhi ya Viongozi wa Vyama vya siasa na viongozi wa Asasi mbalimbali kuhusu mgogoro wa gesi kwenye ukumbi wa VETA mjini Mtwara Januari 27, 2013
 
 
Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda yupo Mkoani Mtwara akikutana na makundi ya wadau mbalimbali wa mkoa huo ili kusikia kutoka kwao mawazo, michango na dukuduku zao kuhusu mradi wa gesi asilia.

Imeripotiwa kuwa Waziri Mkuu angekutana na wanahabari jana saa 9 alasiri ili kutoa mjumuisho wa maongezi yake...
 
 UPDATES/TAARIFA MPYA za ziara ya Waziri Mkuu
Waziri Mkuu alikuwa akutane na Waandishi jana saa tisa alasiri. Kutokana na kikao kirefu cha madiwani wa Manispaa ya Mtwara/Mikindani na Mtwara vijijini pamoja na kikao cha wafanyabiashara, majumuisho ya ziara ya Mtwara atayatolea ufafanuzi kesho.

Dondoo muhimu:

  • Kwa ufupi wajumbe wengi wamekataa bomba la gesi lisiende Dar
  • Wamemkataa Mkuu wa Mkoa na kumtaka Waziri Mkuu aondoke naye
  • Wajumbe (Madiwani ) kumpinga kwa kauli moja  Hawa Ghasia kwa kile kilichosemwa kutumia mamlaka  kutoa kauli za uongo kuhusu Mtwara Vijijini kuunga mkono suala la gesi iende Dar madiwani waMtwara vijijini. Wamesema hawakushirikishwa.
  • Mzozo wa viwanja baina ya Madiwani na Mkuu wa Wilaya
  • Waziri Mkuu ametumia mbinu ya kisiasa kuwashawishi Wadau kuwa bomba liende Dar
  • Wajumbe wameondoka kwa shingo upande kwa kukubali kutokubaliana na Waziri Mkuu
  • Kikao kinafanyika chini ya ulinzi Mkali wa FFU, JWTZ na UwT (Usalama wa Taifa)
  • Hawa Ghasia arudishwa Uwanja wa Ndege, JKNIA asije Mtwara kwani anaweza kuchafua hali ya hewa
  • Polisi wanadai Meya anataka kuwachonganisha na jamii/wananchi kutokana na kauli yake ya kusema wao ndio chanzo cha vurugu

MAITI YA KICHANGA YAGEUKA KUWA KUKU HOSPITALI YA MWANANYAMALA

BADO tupo mwanzoni mwa mwaka lakini tukio la maiti ya kichanga kugeuka jogoo ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti kwenye Hospitali ya Mwananyamala, jijini Dar es Salaam linaweza kuongoza mengine yote ya ajabu yanayoweza kujiri ndani ya 2013.


Mwananyama ni hospitali yenye hadhi ya mkoa kitabibu, ina rekodi za kuwa na matukio ya ajabu, ila hili siyo tu kwamba linaingia miongoni mwa hayo bali pia linaweza kutia fora.
Asubuhi ya Jumatano iliyopita, ilikuwa kizaazaa pale jokofu lililotumika kuhifadhi maiti ya kichanga cha mtoto, kukutwa kuna jogoo.


Mshangao zaidi ni kwamba ndani ya lile jokofu, pembeni ya yule jogoo, kulikuwa na hirizi pamoja na tunguri.



Habari kutoka vyanzo vyetu, zimewekwa wazi kuwa Jumanne iliyopita, saa 7 mchana, polisi walipigiwa simu, wakataarifiwa kuhusu maiti ya mtoto iliyokuwa imetelekezwa eneo la Kigogo, Mbuyuni, Dar es Salaam.


Vyanzo vyetu vimebainisha kuwa polisi baada ya kupata taarifa hizo walifika eneo la tukio na kukuta maiti hiyo ya kichanga ikiwa imefunikwa kwa kuzungushiwa sanda.



Kwa mujibu wa Moses Madilu, mkazi wa Kigogo, aliyedai kushuhudia tukio hilo, polisi walipofika eneo la tukio waliikagua maiti hiyo na kubaini kwamba ni ya kike.


Chanzo chetu kikaeleza kuwa baadhi ya mashuhuda, hususan wanawake, walitokwa na machozi kwa masikitiko kwamba itakuwa mtu alijifungua halafu akakinyonga kichanga hicho kabla ya kukitelekeza eneo hilo.


“Baada ya kujiridhisha kwa kazi yao, polisi waliichukua maiti hiyo ya kichanga, wakaipakia kwenye ‘difenda’, wakaipeleka Hospitali ya Mwananyamala,” kilieleza chanzo chetu.


HOSPITALI YA MWANANYAMALA
Ndani ya hospitali hiyo, mwandishi wetu alielezwa kuwa polisi walipofika, walishusha maiti hiyo na kumkabidhi mganga wa zamu aliyejulikana kwa jina moja la Dk. Liwa.




 “Dk. Liwa aliwaambia wale polisi wapeleke maiti hiyo mochwari.


“Polisi walifanya hivyo lakini kule mochwari walimkuta msimamizi mkuu, Omar Buyoya aliyekataa kuipokea kwa vile daktari hakuthibitisha kama kile kichanga kilikufa au kilikuwa hai.


“Polisi na Buyoya walivutana kwa muda mrefu, alitokea mhudumu mwingine wa mochwari aliyekuwa akijuana na polisi mmoja aliyebeba ile maiti, alikubali kuupokea mwili huo na kuingiza ndani kwenye jokofu la kuhifadhia maiti.”


Muuguzi huyo aliendelea kusema kuwa siku iliyofuata, Dk. Liwa alifika mochwari na alipofungua jokofu na kufunua sanda, badala ya kukuta maiti ya kichanga, alikuta jogoo, tunguri na hirizi.


“Dk.Liwa alipatwa  na mshangao mkubwa huku jasho likimtoka kutokana na uoga, aliwaita wafanyakazi ambao walijazana hapo  mochwari kushuhudia.


“Baadhi ya wafanyakazi walipigwa na butwaa huku wengine wakicheka hadi kudondoka chini na wakawa wanajiuliza kama kweli polisi wanaweza kupeleka jogoo hospitali au ni mambo ya kishirikina,” alisema muuguzi huyo.


Dk. Liwa na wafanyakazi wenzake waliondoka mochwari na kuacha hilo jogoo katika chumba cha maiti huku wakishindwa la kufanya.


KAULI YA MGANGA MKUU.....

Uwazi  ilimtafuta Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk. Sophinias Ngonyani ambaye alikiri  kuonekana kwa jogoo badala ya maiti ya kichanga.


“Polisi walituletea kifurushi wakiamini kuwa ni maiti ya kitoto kichanga ambapo tulikipokea lakini ilipotazamwa na daktari, tulikuta jogoo, hirizi na tunguri, tuliamua kumchoma moto kwa sababu kile ni chumba cha kuhifadhi maiti siyo cha kuhifadhia mizoga ya kuku, ng’ombe au mbwa,” alisema Dk. Ngonyani.


KAULI YA POLISI ...
Naye Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Charles Kenyela alipoulizwa juu ya sakata hilo alisema kwamba wao kama jeshi la polisi walipigiwa simu na raia mwema kuwa  kuna maiti ya kichanga ambapo askari waliondoka hadi eneo la tukio na kuichukua mpaka Hospitali ya Mwananyamala.


“Polisi waliichukua hadi Hospitali ya Mwananyamala kwa wataalamu na baada ya kuikabidhi waliondoka na kuendelea na shughuli nyingine, nami nashangaa kusikia kwamba madaktari walikuta  jogoo,” alisema Kenyela.


MASWALI MATANO
Je, ni kweli polisi waliikagua maiti na kugundua ni kichanga cha kike?


Kama ndiyo, ilikuwaje kikageuka jogoo?


Kwa nini daktari hakuipima ile maiti, badala yake akaelekeza ipelekwe mochwari?


Je, au polisi walibeba mzoga wa jogoo, wakampakia kwenye difenda wakidhani ni maiti ya kichanga?


Mkweli nani, polisi wanaodai kupeleka maiti ya kichanga, au hospitali wanaosema walipelekewa mzoga wa kuku, tunguri na hirizi?


SOURCE: GPL

CCM WAITAKA SERIKALI IWASIKILIZE WANANCHI WA MTWARA

Viongozi wa CCM wakizungumza na wananchi wa Uvinza-Kigoma

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM), kimesema kuwa wananchi wa Mtwara wanayo hoja hivyo Serikali inatakiwa kuwasikiliza na kutoa majibu sahihi.

Pamoja na hayo chama hicho kimesema kuwa kinachoonekana hivi sasa nyuma ya sakata hilo kuna watu wanafanya uhaini, uhalifu na kila aina ya hujumu jambo ambalo wanaitaka Serikali kuchukua hatua kali za kuhakikisha wote wanojihusisha na uhalifu huo wanachukuliwa hatua.

Kauli hiyo ilitolewa jana mjini kigoma na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana ikiwa ni msimamo wa chama chao katika sakata hilo.

Mjadala wa gesi ya Mtwara kutoka mkoani humo kwenda Dar es Salaam umekuwa gumzo kubwa huku wananchi wakiitaka Serikali kuwaeleza watanufaika vipi na gesi hiyo kabla ya kunufaisha maeneo mengine.

Kinana alisema kuwa kuna haja kwa Serikali kuhakikisha inatumia nafasi yake kuzungumza na wananchi wa Mtwara katika kupata suluhu ya suala hilo kwani wana hoja za msingi ambazo zinataka majibu.

“Msimamo wetu kama chama, tunataka Serikali kukaa na wananchi hao na kuwasikiliza.Tunahitaji kuona Serikali inatoa majibu ambayo yatakuwa sahihi na kumaliza tofauti iliyopo sasa,”alisema Kinana.

Pamoja na hayo alisema kuwa kinachoshangaza ni kuona hali ya uvunjifu wa amani inayofanywa na baadhi ya watu ambao wameamua kuingia mtaani na kuiba, kupora mali na kuharibu nyumba za watu kwa kuzichoma moto.

Alisema kuwa CCM inaona ni wakati mzuri kwa Serikali kuwadhibiti wote ambao wanatumia mwanya huo kufanya uhalifu huo ambao haukubaliki huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kusikilizwa.

Alisema mtazamo wa chama chao ni kwamba kuna jambo ndani ya suala hilo maana gesi inatakiwa kujadiliwa kwa njia ya amani kupata suluhu kuliko mali za watu kuharibiwa na kufanywa kwa uhalifu ambao hauvumiliki.

Sunday, January 27, 2013

TAARIFA YA NDG ZITTO KABWE (MB) KUHUSU YANAYOENDELEA MTWARA NA MRADI WA BOMBA LA GESI ASILIA


Taarifa ya NDUGU ZITTO KABWE (MB) kuhusu yanayoendelea MTWARA na Mradi wa Bomba la GESI asilia

Sunday, January 27, 2013 · Posted in 
Serikali iache kutafuta mchawi, iende Mtwara   


Katika kipindi cha wiki nne sasa kumekuwa na maandamamo, malumbano na vurugu kuhusu mradi wa kujenga bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Mradi huu wa kutandaza bomba la urefu wa kilometa 542 ni mkubwa sana hapa nchini, na una thamani kubwa zaidi kuliko miradi mingine yote  ya miundombinu iliyopata kutokea hapa nchini. Mradi huu utajengwa kwa mkopo wa dola za Kimarekani 1.2 bilioni kutoka Benki ya Exim ya China.  
Wananchi wa Mtwara kupitia maandamano ya tarehe 27 Desemba 2012 wametaka kujua hatma ya maendeleo ya mikoa wa kusini kutokana na mradi huu wa bomba la gesi. Serikali imewajibu wananchi hawa kwa kuwaita wahaini, watu hatari na wasio elewa. Imefika mahali inapotosha madai yao kwamba hawataki gesi itoke Mtwara.   

Kimsingi Serikali haijajibu hoja yeyote ya msingi ya wananchi wa Mtwara kuhusu mradi wa kusafirisha gesi. Badala yake imekuwa ikijaribu kupotosha madai ya watu wa Mtwara kupitia mikutano na vyombo vya habari.   

Tangu maandamano haya yatokee, na baadaye mikutano ya hadhara nahatimaye matukio ya kusikitisha ya kuharibu mali za watu, mauaji ya watu na majeruhi mbalimbli, Serikali na hasa Wizara yenye dhamana ya mradi huu, imekuwa ikitoa matamko kwenye vyombo vya habari badala ya kwenda Mtwara kuzungumza na wananchi, kusikiliza madai yao na kuona namna ya kutekeleza madai hayo. Kutokana na Serikali kutofanya hivyo, kusikiliza na kuzungumza na wananchi wa Mtwara, vurugu mbaya sana zimeendelea mkoani humo. 

Mwezi uliopita, Desemba 2012, tatizo lilionekana kuwa ndogo na lenye kuhusiana zaidi na ukosefu wa kushirikishwa kwa wananchi. Badala ya kushughulikia tatizo likiwa bado ndogo, Serikali imeona njia pekee ya kushughulikia suala hili ni kutafuta mchawi na kwa wiki zote hizi imekuwa ikisemakuwa wanasiasa na makampuni ya uwekezaji ya nje yanachochea mgogoro huu.   

Leo hali iliyopo mkoani Mtwara inasikitisha sana, maana mali za wananchi zinaharibiwa, nyumba zinachomwa moto na watu wanapoteza maisha. Tunalaani matukio haya kwa nguvu zetu zote, maana kinachotokea Mtwara si Utanzania. Tusipowasikiliza wananchi na kutatua mgogoro huu kwa kuwashirikisha, hali itazidi kuzorota wakati tukitupiana lawama.   Hivi sasa serikali imeona njia pekee ya kushughulikia suala hili ni kutafuta mchawi na kwa wiki zote hizi imekuwa ikisema kuwa wanasiasa na makampuni ya uwekezaji ya nje yanachochea mgogoro huu.  

Kwanza, Serikali imekuwa ikiaminisha umma kwanza suala hili limechukuliwa kisiasa. Pili, Serikali imekuwa ikirudia kusema kuwa baadhi ya makampuni ya uwekezaji nchini na mataifa ya Magharibi yamekuwa yakichochea wananchi wa Mtwara.   

Katika mwendelezo wa mtindo wa Serikali wa ‘management by press conferences’ jana Jumamosi Naibu Waziri wa Nishati na Madini ndugu George Simbachawene aliwaambia wahariri kwamba mimi Zitto Kabwe ninachochea wananchi wa Mtwara, ninatumiwa, na si mzalendo. Vile vile alitoa vielelezo kadhaa kuonyesha kuwa mradi wa kujenga bomba la gesi ni gharama sawasawa. Akasisitiza kwamba mimi ni mwongo.   

Katika kipindi chote cha mgogoro wa Gesi Mtwara, sijafika Mtwara. Sijafanya mkutano wowote na waandishi zaidi ya kuandika mawazo yangu, kama Mtanzania kuhusu suala hili.   Nimeandika makala nne na zimechapishwa katika magazeti kadhaa hapa nchini na kwenye blogu yangu (www.zittokabwe.com).   

Sitaki kubishana na Naibu Waziri ama Kiongozi yeyote ya Serikali kwa sasa. Hatuwezi kuendelea kulumbana, kuzozana, kuzodoana na kurushiana maneno wakati nchi yetu inaungua. Huu sio wakati wa kutafuta mchawi bali kutafuta majawabu ya changamoto zilizopo mbele yetu.   Yanayotokea Mtwara ni fundisho kwetu kwa Taifa namna ya kukabili changamoto za utajiri wa rasilimali, ili kuweka mkakati, mambo haya yanayotokea Mtwara yasitokee tena Tanzania. Tutaweza kuzuia maafa haya iwapo tutaweka uwazi katika mikataba, tutashirikisha wananchi kwenye unyonyaji wa maliasili za nchi, na iwapo tutaweka uwajibikaji.     

Rais Kikwete Kikwete ana majibu; ayatoe sasa kwa wana Mtwara   

Kwa mujibu wa Mpango Kabambe wa Umeme nchini (Power System Master Plan), kulikuwa na mradi wa kufua umeme MnaziBay, ambao Rais Jakaya Kikwete aliagiza utekelezwe mara moja. Serikali ieleze umma kuhusu mradi huo wa kujenga kituo cha kufua umeme 300MW MnaziBay Mtwara na kujenga msongo wa umeme wa 300KV mpaka Singida. Umeishia wapi? Ikumbukwe kuwa mnamo tarehe 12 Oktoba 2012, Rais Jakaya Kikwete alipokea ripoti ya ujenzi wa mradi huu kutoka makampuni ya China National Machinery & Equipment Import & Export Corporation (CMEC) ya China na Siemens ya Ujerumani, ambayo kwa pamoja yalitarajia kujenga kituo kikubwa cha kuzalisha umeme kutokana na gesi katika eneo la Mnazi Bay, mjini Mtwara na pia kujenga njia ya kusafirisha umeme ya kilomita 1,100 kutoka Mtwara hadi Singida. Mradi huu ungegarimu dola za kimarekani milioni 684 na Rais aliagiza utekelezwe haraka sana. Huu mradi uliishia wapi? Kwa nini Serikali ipo kimya kuhusu mradi huu ambao ungejibu kabisa maswali ya watu wa Mtwara? Taarifa ya Ikulu kuhusu mradi huu imeambatanishwa hapa.   

Tufanyeje?   

Hapa tulipofikia ni lazima kwanza kabisa kusikia kilio cha wananchi wa Mtwara ikiwemo kuelewa madai yao. Swali kubwa kubwa la watu wa Mtwara na Kusini kwa ujumla ni ‘tunanufaikaje’? Jibu la swali hili si ahadi za miradi bali ni vitendo. Hapa ndipo serikali inaposhindwa kushughulikia suala hili, kutoelewa madai ya wananchi na kuyapotosha.Viongozi wa kisiasa wenye ushawishi kutoka pande zote, chama tawala na vyama vya upinzani, waende Mtwara kuzungumza na wananchi, lakini wawasikilize kwanza.   
  1. Lazima viongozi tujenge utamaduni wa kusikiliza wananchi na si kuwahutubia tu. Wananchi wa Mtwara wana madai ambayo lazima viongozi tukae kitako kuwasikiliza kisha kufanya nao majadiliano ambayo yatatoa mwafaka. Rais mstaafu, Ndugu Benjamin Mkapa ameshatoa kauli kuhusu suala hili. Ni wakati mwafaka sasa kwa viogozi wengine kumuunga mkono kwa kwenda Mtwara na kukaa na wananchi wa Wilaya zote za Mtwara, kusikiliza hoja zao na kuona namna ya kupata ufumbuzi wa suala hili. Wakati hatua hii inachukuliwa, wananchi waombwe kutulia na kuacha vurugu za aina yeyote ile, na Serikali isimamishe mradi mpaka hapo suluhu na wananchi itakapopatikana.  
  2. Wakati juhudi hizo zinaendelea Serikali iweke wazi mkataba wa ujenzi wa bomba, kwani ni dhahiri gharama za mradi huu ni kubwa mno kulingana na uhalisia wa miradi ya namna hii duniani kote. Katika taarifa zote kwa umma Serikali imekuwa ikisema kwamba mradi utagharimu jumla ya dola za kimarekani 1.2 bilioni, lakini katika taarifa ambayo Wizara ya Nishati na Madini imesambaza jana kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini imesema mradi utagharimu dola za kimarekani milioni 875. Usiri katika mkataba huu unaashiria kwamba Serikali inaficha kitu. Hivyo njia pekee ni kutaka mkataba uwe wazi kwa wananchi.  
  3. Wakati tunawataka wananchi wa Mtwara kuruhusu utulivu, ni vema Serikali ijiandae kutoa majawabu ya madai ya wananchi hao. Majawabu ya Serikali yajikite kueleza wananchi wa Mtwara wanafaidikaje na rasilimali ya gesi asilia kwa maendeleo yao. Wananchi wa Mtwara wanataka uwajibikaji wa Serikali kwenye utajiri wa nchi, na wamechoka na porojo za orodha ya miradi isiyotekelezwa.

Viongozi twendeni Mtwara kusikiliza wananchi wetu. Nchi inaungua na hatuwezi kuendelea kuzozana badala ya kuzima moto huu hatari kama vita vya MajiMaji. Mimi nakwenda Mtwara haraka na mara baada ya viongozi wangu wa chama kutoa ridhaa.     

ZITTO KABWE 
Mbunge, Kigoma Kaskazini (CHADEMA) 
Waziri Kivuli wa Fedha 
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni


SISTER MARY YA RAY YAPIGWA STOP

STAA wa filamu za Bongo, Vincent Kigosi ‘Ray’ yamemkuta baada ya ile ishu yake ya kutengeneza filamu inayoitwa Sister Marry ambapo mapadri wamemtaka asiipeleke sokoni milele. 

Ishu hiyo ilitokea kwenye kikao kizito cha saa 5 kilichofanyika Jumanne iliyopita katika Ofisi za Utamaduni jijini Dar es Salaam.
 

Washiriki wa kikao hicho walikuwa Ray, Mkurugenzi Mtendaji wa Utamaduni aliyetajwa kwa jina moja la Mwansoke, mapadri wanne na mtu mmoja aliyedaiwa kuwa ni wa kutoka Ofisi za Usalama wa Taifa.
 

Kikao hicho kilikuja baada ya hivi karibuni viongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam kumtaka msanii huyo ajieleze kimaandishi ni kwa nini mtawa Sister Marry (Irene Uwoya pichani) alikuwa akifanya matendo ambayo kiuhalisia, Wakatoliki wenyewe huwa hawayafanyi.
 

Kabla Ray hajajieleza kwa maandishi ndipo alipoitwa huko na kukubaliana ana kwa ana  na jopo hilo huku mashinikizo kadhaa yakielekezwa kwake.
 

Awali, wajumbe wote wakiwa wamekaa kwenye viti, filamu hiyo yenye saa 3 iliwekwa mwanzo mwisho huku mapadri hao wakiguna kila wakati, hasa wakati Sister Marry akiwa anafanya mambo yake mabaya.
 

Baada ya kumalizika kwa filamu hiyo, hoja zikaanza. Mwansoke akasema vipande vyote vichafu vinyofolewe na kubaki vile ambavyo wajumbe hawakuvigunia.

  
Baada ya bosi huyo kusema hayo, mapadri wakasema ‘noooo’. Filamu hiyo isiende mitaani hata kidogo kwani imejaa udhalilishaji wa Wakatoliki.
 

Inasemekana Paroko wa Kanisa la Mtakatifu Maximilian Kolbe lililopo Mwenge Kijijini (jina halikupatikana mara moja) yeye alipigilia msumari wa mwisho kwa maneno aliyoyatoa.
 

Alisema kwa kuwa filamu hiyo ilirekodiwa kwenye kanisa lake hilo, anataka vipande vyote vya kanisa hilo vitolewe ndipo iingie mtaani, jambo ambalo lilimtoa machozi Ray.
 

Ray sasa! Siku ya Alhamisi iliyopita, Ray alizungumza na Amani  na kukiri kuwepo kwa kikao hicho. Akasema itakuwa vigumu kuviondoa vipande vya kanisa hilo kwa sababu asilimia 85 ya filamu nzima imerekodiwa Maximilian Kolbe.
 

“Asilimia 85 ya filamu imerekodiwa Maximilian Kolbe, sasa wanaposema niviondoe ni kuimaliza filamu yote. Filamu ni ya saa 3, ukivitoa vipande vya kanisa si itabaki dakika 5 tu,”alisema Ray.
 

Alisema kikao kiliisha kwa maamuzi hayo, kwamba mtu wa utamaduni alisema vipande vichafu vinyofolewe huku mapadri wakitaka muvi nzima isiende sokoni na paroko wa Maximilian Kolbe akitaka kanisa lake lisionekane kwenye filamu hiyo.
 

Mwandishi: “Je, wewe  Ray umeamuaje?”
 

Ray: “Sijaamua chochote kwa kweli. Niponipo tu, nimetumia fedha nyingi sana.” 

SOURCE:http://www.freebongo.blogspot.com

PICHA TISA ZINAZOONYESHA ATHARI ZA VURUGU MKOANI MTWARA

Ofisi ya Elimu wilaya ya masasi ikiteketea kwa moto kufuatia vurugu za wananchi zilizotokea jana wilayani humo kwa kile kilichodaiwa askari kumpiga mwendesha bodaboda na kusababisha kifo chake.
Baadhi ya magari ya Halmashauri ya wilaya masasi yakiteketea kwa moto
Gari la wagonjwa la wilaya ya masasi nalo likiteketea kwa moto
Jenereta la Halmashauri hiyo poa likiteketea kwa moto
Nyumba ya Waziri wa Tamisemi Mh. Hawa Ghasia, iliyopo maeneo ya stand mtaa wa Sinani mkoani Mtwara jinsi ilivyoteketezwa kwa moto sambamba na kuvunjwa kwa vioo vya madirisha na milango kama inavyoonekana pichani.
Pichani ni jinsi mahakama ya mwanzo iliyopo mtaa wa stand kata ya Chikongola ilipokuwa inaanza kuteketea kwa moto, inasemekana kuwa eneo hilo lililopo mahakamani hapo limeuzwa na kuuziwa mtoto wa Rais Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Ridhiwan Kikwete.
Mabaki ya mahakama ya mwanzo ilivyoteketezwa na wananchi wenye hasira kali wilayani Mtwara.
Moja tu kati ya mabango wakati wa maandamano kabla hawajaamua kuanzisha vurugu
Mkazi wa Magomeni mkoani Mtwara Mohamed Rashid akiwa amejeruhiwa kutokana na vurugu hizo.

 

















HABARI KAMILI
WATU Saba akiwemo askari polisi mmoja wameuawa katika vurugu zilizotokea jana wilayani Masasi mkoani Mtwara, zikiwa zimebeba sura ya kupinga gesi kwenda Dar es Salaam.

Muuguzi wa zamu hospitali ya wilaya ya Masasi, Mkomaindo Fatuma Timbu amethibitisha kupokea maiti za watu saba.

Majeruhi ambao idadi yao haijajulikana wamekimbizwa hospitali ya misheni ya Ndanda kwa matibabu na hali bado ni tete, Vurugu kubwa zilianza majira ya saa 4 asubuhi jana baada ya polisi waliokuwa wakiendesha pikipiki kumgonga mtu na kukataa kutoa ushirikiano, Hata hivyo hoja hiyo ilihamia kwenye suala la gesi na kundi la vijana mara moja walivamia nyumba ya mbunge wa Masasi, Mariam kasembe na kuiwasha moto, pamoja na magari mawili.

Aidha vijana hao walivamia nyumba ya Anna Abdallah na kuiteketeza kwa moto kabla ya kuivania ofisi ya CCM wilaya na kuichoma moto pamoja na magari matatu, Hasira za wananchi hao zilifika kituo kidogo cha polisi kilichopo Mkuti wilayani humo na kukichoma moto ambapo baadae walichoma moto magari matano ya halmashauri ya wilaya.

Pia walichoma moto ofisi ya elimu ya halmshauri ya wilaya Masasi vijijini, kabla ya kuichoma ofisi ya maliasili.

Polisi kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya mkoa wa Mtwara inadaiwa walitumia risasi za moto na kusababisha vifo vya watu Sita huku polisi akidaiwa kuuawa kwa kupigwa na wananchi.

Picha na Happy Severine Mtwara, habari Abdulaziz video Masasi

Thursday, January 24, 2013

DIAMOND NDANI YA PENZI ZITO LA VJ PENNY WA DTV


Nyota wa Bongo Fleva anayemake headlines kila kukicha, Diamond Platnumz sasa ameibuka na story mpya kuwa anatoka kimapenzi na mtangazaji wa DTV VJ Penny na hivi sasa mapenzi yao ni moto moto kama unavyoona pichani juu.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari ni kuwa mapenzi yao yalianza siku ambayo Platinums alialikwa kwenye kipindi kinachoendeshwa na mwana dada huyo kwenye Luninga ya DTV kama hiyo picha inavyoonyesha (hiyo picha ilipigwa siku hiyo) na baada ya show hiyo wawili hao walikwenda kujiachia na ndiyo ukawa mwanzo wa mapenzi yao ambayo mpaka sasa yako hot na mwana dada huyo hakauki nyumbani kwa Diamond.
                                         
Picha hizo zote mbili zimeonekana kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook na ndipo story za mapenzi ya wawili hao zilipoanza kuzagaa.

WANANCHI WILAYANI RUFIJI WAVAMIA KITUO CHA POLISI NA KUCHOMA NYUMBA MOTO


Habari zilizotufikia hivi punde zinaeleza kuwa wananchi wenye hasira kali Kibiti Wilayani Rufiji mkoa wa Pwani leo, wamevamia kituo cha Polisi Kibiti na kuanzisha vurugu kubwa kufuatia mwananchi mmoja mkazi wa kijiji hicho kufariki dunia kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kutokana na kipigo cha Polisi.

Habari kutoka Kibiti zinasemakuwa, kijana huyo aliyefariki kutokana na kipigo hicho amefahamika Khamis Mpondi ambaye amepoteza maisha wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam, ambapo taarifa hiyo ilipowafikia wananchi wa kijiji hicho wakachukua uamuzi wa kwenda kituoni hapo na kuanzisha vurugu hizo.

Habari zaidi zinaeleza kuwa,baada ya kufanya vurugu katika kituo hicho cha polisi wakaendeleza vurugu zao kwa  kuteketeza nyumba za Askari Polisi zilizopo jirani kabisa na kituo hicho, licha ya juhudi za Polisi kuwatawanya kwa mabomu kuendelea kufanyika.

Mpaka taarifa hizi zinafika kwa blog hii wananchi hao walikuwa wamefunga barabara kuu ya Kilwa iendayo Mikoa ya Kusini, (Lindi na Mtwara) kwa mawe, magogo na kuchoma matairi ikiwa ni umbali unaokadiriwa kuwa ni wa kilometa moja kutoka kituo cha Polisi Kibiti.

Inaelezwa kuwa hali imezidi kuwa tete katika eneo hilo huku Polisi wa Kibiti wakiendelea na jitihada za kudhibiti hali hiyo kwa kufyatua mabomu ya machozi hewani kujaribu kutawanya umati huo wa watu.

tutaendelea kupeana taarifa zaidi kadri zitakavyokuwa zikitufikia.

Wednesday, January 23, 2013

FLAVIANA MATATA ANYAKUA TUZO YA MWANAMITINDO BORA AFRIKA


MWANAMITINDO wa kimataifa wa Tanzania, Flaviana Matata ameendelea kung’ara kimataifa baaada ya kushinda tuzo ya Nigeria’s Next Super model na kuwa mwanamitindo bora barani Afrika wa mwaka 2012 (Africa’s Most Outstanding Model 2012).

Tuzo hiyo hutolewa kwa wanamitindo ambao bado wanailetea sifa Afrika kimataifa na Flaviana amekuwa katika chati ya juu. Mwaka jana Desemba,  Flaviana alishinda tuzo nyingine  ya uwanamintindo bora kutoka kwa diaspora ya Waafrika.

Flaviana ambaye kwa sasa  anaishi na kufanya kazi ya uanamitindo New York nchini Marekani kupitia shirika la Wilhelmina Models, mpaka sasa ameweza kuitangaza Tanzania kimataifa kutokana na umahiri wake katika maonyesho ya mavazi.

Tangu ashinde taji la Miss Universe Tanzania mwaka 2007, Flaviana amekuwa aking’ara katika kona zote za dunia na hasa baada ya kumaliza katika nafasi ya sita katika mashindano ya kimataifa ya Miss Universe, huku Tanzania ikishiriki kwa mara ya kwanza.

Ameweza kushiriki katika maonyesho ya mavazi mengi Ulaya na Amerika huku akitoa misaada mingi kwa Watanzania wenzake ambao wamekuwa na ndoto ya kufika mbali katika fani hiyo.

Kwa sasa Flaviana anaendesha taasisi yake, Flaviana Matata Foundation ambayo inasomesha watoto wa kike 16 na mwaka jana alitoa msaada wa vifaa vya kuokoa maisha kama sehemu ya kumbukumbu ya kuzama kwa meli ya MV Bukoba huku ikiwa kumbukumbu ya kifo cha mama yake mzazi katika ajali hiyo ya mwaka 1996.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Compass Communication Tanzania Limited, Maria Sarungi Tsehai alisema kuwa wamejisikia faraja sana kwa kumvumbua mwanamitindo huyo ambaye kwa sasa anashika chati ya juu Tanzania na nje ya nchi.

Maria alisema kuwa Flaviana amedhihirisha ubora wake na mpaka sasa amepitiliza kiwango cha kuitangaza Tanzania nje ya mipaka yake, ndoto ambayo alikuwa nayo muda mrefu.

FID Q ATUNUKIWA CHETI MAALUMU NA "UNDER THE SAME SUN"

Mkali wa mashairi na flow kutoka Mwanza Fareed Kubanda a.k.a Fid Q ametunukiwa cheti maalum cha shukurani na shirika linalosaidia watu wenye ulemavu wa ngozi(albino) linalojulikana ma Under The Same Sun kwa mchango wake mkubwa katika kusapoti kampeni ya shirika hilo.
Ngosha amepost picha akiwa na mwanzilishi na mwenyekiti wa shirika hilo la Canada,Peter Ash, na kuisindikiza picha hiyo na maandishi yanayosomeka

 "Just received CERTIFICATE OF APPRECIATION from the one and only Mr. Peter Ash (CEO of Under The Same Sun)."

Mwaka jana Fid Q akiwa na wasanii wengine wa muziki wa kizazi kipya na walizungukia mikoa ya kanda ya ziwa na kuwahamasisha watu kupinga mauaji ya albino wakiwa na shirika hilo.


baada ya miezi kadhaa walirudi tena kanda ya ziwa kuwarudishia shukurani wakaazi wa kanda ya ziwa kwa sababu mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) yalipungua sana hivyo kampeni yao kwa kushirikiana na wakaazi wa kanda ya ziwa ilifanikiwa.

SHAKIRA AJIFUNGUA MTOTO WA KIUME

Nyota wa Pop wa nchini Colombia, Shakira amejifungua mtoto wa kiume jana mjini Barcelona, Hispania. Shakira ametoa taarifa hizo kupitia website yake ambayo iliandikwa kwa Kiingereza, Spanish na Catalán:


“We are happy to announce the birth of Milan Piqué Mebarak, son of Shakira Mebarak and Gerard Piqué, born January 22nd at 9:36pm, in Barcelona, Spain.The name Milan (pronounced MEE-lahn), means dear, loving and gracious in Slavic; in Ancient Roman, eager and laborious; and in Sanskrit, unification.”

Baba wa mtoto huyo ni mchezaji wa FC Barcelona, Gerard Piqué.

Friday, January 18, 2013

NASEMA UKWELI SIJUI KIINGEREZA AFUNGUKA CLOUD



Staa wa filamu nchini Issa Mussa(Cloud) pichani, aliwaacha watu midomo wazi pale alipoamua kufunguka mbele ya hadhara ya watu kuwa hajui kiingereza

Tukio hilo lililowashangaza wengi wakiwemo wasanii wenyewe limetokea jana katika ofisi za Finance Solutions wakati wa mkutano wa Mkururugenzi Mtendaji kampuni hiyo(Finance Solutions) Bw. Isaack Kassanga, Mkurugrnzi wa Mad Mad Entertainment Yasmine Razack walipokuwa wakitambulisha mpango wao wa kuwapeleka wasanii nje ya Nchi kufanya Filamu na wasanii wa kimataifa

Wakati wa mkutano huo mkurugenzi wa mad mad Entertainment alisema kuwa kigezo kikubwa kati ya vigezo wanavyotakiwa kuwa navyo wasanii ni kufahamu Lugha ya kiingereza ili iwarahisishie mazungumzo, ndipo msanii huyo alipofunguka kuwa kigezo hicho kisiwe muhimu kwa kuwa wasanii wengi akiwemo yeye hajui kiingereza.

"Nasema ukweli wasanii wengi hatujui kiingereza, nasema ukweli mbele ya waandishi wa habari hata mimi mwenyewe sijui kiingereza kwa hiyo kigezo hicho kisiwe muhimu  kwa sababu wasanii wengi tutakosa nafasi hiyo". Alisema msanii huyo.

WASANII WA BONGO MOVIE KUTANGAZWA KIMATAIFA, WAAHIDIWA KUPELEKWA KUPELEKWA NIGERIA KUCHEZA FILAMU

 Mkurugenzi wa Mad Mad Entertainment, Yasmin Razak (katikati) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu kampuni yake kuingia mikataba na wasanii wa filamu wa Tanzania na kuwapeleka Nigeria na Jmahuri  ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa ajili ya kutengeza filamu. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Superior Solutions, Issack Kasanga na (kulia) Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Simon Mwakifamba. 

Msanii wa filamu, Steve Nyerere (kulia) akifafanua jambo wakati wa mkutano huo.Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Superior Solutions, Issack Kasanga(kushoto) na Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Simon Mwakifamba(katikati)

KAMPUNI ya Mad Mad Entertainment iliyopo jijini London nchini Uingereza, 
imeanzisha program maalum ya kupeleka wasanii wa filamu za bongo nje ya nchi kwa lengo la kukuza sanaa hiyo hapa nchini.
 Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Yasmin Razak alisema ameamua kufanya kazi na wasanii  hao ili kuleta mabadiliko na kuwakwamua kiuchumi wasanii wa filamu hapa nchini baada ya kuona sanaa ya Tanzania haikui.

 “Kwa muda mrefu niliokaa London nimeona sanaa ya Tanzania haikui wala haibadiliki, nikafikiria kitu gani nifanye ili  kukuza tasnia hii ndipo nikaamua kuanzisha mpango huu, katika mkataba na kampuni msanii atakayetengeneza filamu na wasanii wa nje atalipwa kiasi cha sh 50 milioni pamoja na malipo mengine yatakayokuwepo kwenye mkataba, ikiwa ni pamoja na asilimia fulani kwa kila kazi itakayouzwa hapa nchini.

“Nimekuwa nikifanya kazi hiyo na wasanii wengi kutoka Nigeria wakiwemo kina Omotola, Two Face na wengineo na pia Ghana, Congo na hata Uingereza, hivyo nimeonelea kuwa itakuwa vema Tanzania nao kuingia katika mchakato huo,”alisema Razak.

Razak ambaye amesema pamoja na kusimamia kazi za muziki za Fally Ipupa lakini sasa wameanza project ya filamu ambapo tayari Fally ameshafanya filamu moja na 2Face Idibia na sasa ameamua kuangalia nyumbani na alitaja vigezo vya msanii atakayechaguliwa ikiwa ni pamoja umaarufu,  kuijua lugha ya kiingereza, uwezo wa kuigiza na kuuvaa uhusika wowote pamoja na mavazi.

Naye rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Simon Mwakifwamba aliwataka wasanii hao kujipanga kimataifa zaidi katika kuhakikisha wanaingia kwenye ushindani huo na kuwataka wale watakaochaguliwa kujituma na kutuwakilisha vema kwa kuonyesha nidhamu ya uhakika.

“Hapa kuna kuinua vipaji, soko la kimataifa na mengineyo, hivyo ni vema kufanya kazi kikamilifu kwa wale watakaochaguliwa na si kujisahau, wanatakiwa wasanii watatu na tupo katika hatua za awali za mchujo,” alisema
Mwakifamba.

Wednesday, January 16, 2013

ZAIDI YA ABIRIA 100 WANUSURIKA KUFA BAADA YA KIVUKO KUZIMA INJINI BAHARINI


ZAIDI ya watu 100 wamenusurika kufa maji baada ya Kivuko cha MV Magogoni kuzima injini na kupoteza mwelekeo baharini ambapo habari zinasema kuwa Kivuko hicho kilizima baada ya kupishana na meli kubwa ya Azam iliyokuwa imebeba mizigo na hata nahodha wa meli hiyo ya mizigo alifanya kazi kubwa ya kukikwepa kivuko hicho.


Akizungumza na blog hii jana, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo Halima Fred ambaye ni mkazi wa Kigamboni aliyekuwa ndani ya kivuko hicho alisema, baada ya injini za Mv Mgogoni kuzima, nahodha alishindwa kuizuia isisukumwe na upepo.


MV Magogoni ilikuwa ikitoka Kigamboni kuelekea upande wa pili (ferry) huku ikiwa na abiria zaidi ya 100 na kusababisha hofu kwa abiria na kusababisha baadhi ya abiria hao kukimbilia vifaa vya kuogelea hata hivyo mainjinia waliokuwa ndani ya kivuko hicho walifanya jitihada za kuwasha injini moja ya kivuko hicho na hatimayekuendelea na safari.

Tuesday, January 15, 2013

WALEMAVU WA NGOZI WALIA NA SERIKALI, WAITAKA IBAINI NJIA MPYA ZA MAUAJI DHIDI YAO


Chama cha Walemavu wa ngozi nchini kimelalamikia uendeshwaji wa kesi za watu wanaokamatwa kwa kuwadhuru, pamoja na kutokamatwa kwa kundi la waagizaji wakubwa wa viungo vya walemavu hali inayowapa mashaka juu ya usalama wao
.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ukumbi wa habari maelezo jijini Dar es salaam, Afisa Mahusiano na utetezi wa Chama cha Albino Nchini Bw. Joseph Torner amesema kwa uchungu kuwa, Kutokamatwa kwa kundi la tatu ambao ndio wanunuzi au waagizaji wa viungo vya Albino ni ishara kuwa tatizo hilo halitomalizika nchini


"Kesi ambazo zipo mahakamani mpaka sasa ni tano tu, wakati Albino waliouawa ni 70 na waliokamatwa ni waganga na wale wanaotekeleza matukio ya mauaji, je kundi ambalo ni waagizaji wa viungo hivi wako wapi wakati nchi yetu inasifiwa kwa upelelezi?" alisema bwana Torner


Aliongeza kuwa wanaiomba serikali iweke mikakati mipya, kwani hivi sasa wauaji wana mbinu zingine kiasi kwamba unaweza kuhisi mauaji hayapo lakini mauaji bado yanaendelea.
Aidha, Touner alilalamikia kitendo cha wanafunzi zaidi ya 139 wenye ulemavu wa ngozi katika shule ya Msingi Buhangija iliyopo manispaa ya Shinyanga kutorudi nyumbani wakati wa likizo kwa kuhofia usalama wao, ikiwa haijulikani ni lini watarudi kukutana na familia zao
.

" Wanafunzi wengi wenye ulemavu wa ngozi wamejikuta wakiwa kwenye kambi kila inapofika kipindi cha likizo kitendo ambacho kinaleta simanzi kwa familia za watoto hao, kwani hawajui ni lini watakutana na familia zao" Alisema Touner


Tangu mwaka 2006 mpaka hivi kumekuwa na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi hapa nchini licha ya serikali kuweka usalama kwa watu hao.