Thursday, March 22, 2012

FM ACADEMIA KUPAMBA BONANZA LA WAANDISHI WA HABARI JUMAMOSI

Bendi ya muziki wa Dansi nchini FM Academia "Wazee wa ngwasuma" wanatarajiwa kutoa burudani ya kukata na shoka katika Bonanza la waandishi wa habari linalotarajiwa kufanyika Jumamosi hii ambapo wanahabari zaidi ya 1500 kutoka katika vyombo mbalimbali vya habari nchini wanatarajiwa kushiriki katika Bonanza hilo litakalofanyika katika ukumbi wa msasani Beach Club
Bonanza hilo hufanyika kila mwaka likiandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) na linajulikana kama Media Day Bonanza.

Lengo la bonanza ni kuwaweka pamoja waandishi wote wa habari bila kujali ni wa siasa, michezo, uchumi, afya na mambo mengine pamoja na wafanyakazi wa vyombo mbalimbali vya habari, ili kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja.
Maandalizi kuhusiana na bonanza hilo yapo hatua za mwisho, ambapo shughuli itaanza saa tatu asubuhi hadi saa mbili usiku.
Pamoja na FM Academia pia kutakuwa na wanamuziki wa Bongo Fleva ili kuongeza nguvu ya burudani
Mgeni rasmi katika bonanza hili atakuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki na aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta.Pamoja na mambo mengine, Sitta atakabidhi zawadi za vikombe na medali kwa washindi mbalimbali watakaoibuka siku hiyo, pia atapata fursa ya kuzungumza na washiriki wa bonanza hilo.
Aidha vyombo vya habari ambavyo havijathibitisha ushiriki wao kwa njia ya maandishi vimeombwa kufanya hivyo kama vilivyoagizwa kwenye barua zao za mialiko, vinginevyo ushiriki wao hautathaminika.

No comments:

Post a Comment