Thursday, September 8, 2011

MHINA PANDUKA AINGIA MATATANI KWA UDANGANYIFU

Mhina panduka
Panduka kushoto na Mangustino wa K- Mondo Sound
MWIMBAJI maarufu nchini Tanzania, Mhina Panduka ‘Toto Tundu’ ameingia matatani baada ya uongozi wa Bendi ya K-Mondo Sound kuamua kumfungulia kesi ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, baada ya kusaini mkataba wa kufanya kazi na Bendi hiyo kwa muda wa mwaka mmoja kuanzia Oktoba mwaka jana na badala yake alifanya kwa muda wa mwezi mmoja tu na kutimkia Visiwani Zanzibar na baadae kurejea Dar Es Salaam na kufanya kazi na TOT Band.
Taarifa iliyotolewa na Uongozi wa K-Mondo Sound imesema kuwa, wamefikia hatua hiyo ya kumshitaki Panduka baada ya kujaribu kumuita mara kadhaa tangu Aprili mwaka huu ili kumaliza suala lake lakini mwanamuziki huyo hakuonekana kujali.
“Tulimwita Panduka Aprili mwaka huu wakati wa sikukuu ya Pasaka aje kumaliza suala la mkataba wake,  tulipozungumza nae alisema hajasaini mkataba na TOT na atarudi, lakini akaomba afanye show ya Jumapili ya Pasaka pale Mango na TOT halafu atarudi K-Mondo lakini mpaka leo hajatokea,
Baada ya hapo tulimwandikia barua kupitia kampuni ya uwakili ya JM Attorney na akatakiwa kumaliza suala hili lakini mpaka leo hakuna alichojibu zaidi ya kuwatumia meseji viongozi kuwa watapambana mahakamani,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema wanamuziki wengine watatu ambao walikuwa wamechukua pesa na kukimbia wote waliamua kurudi kumalizia mikataba yao na mwingine ambaye ni mpiga rythim Fadhili aliamua kurudisha hela. Wengine waliokuwa wameondoka baada ya kuchukua hela lakini wakaamua kurudi kumalizia mikataba yao ni Joshua Bass ambaye alitimkia THT na Husein Said Tumba aliyekuwa Royal Band.
Taarifa hiyo  iliongeza kuwa baada ya kushauriana na wanasheria uamuzi uliofikiwa ni kumfungulia kesi hiyo ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu ili sheria ichukue mkondo wake kwani nyaraka zote za kusaini mkataba na jinsi alivyochukua pesa zipo.
Mbali na kuchukua pesa hizo Panduka pia ameitia K-Mondo Sound Band  hasara ya zaidi ya shilingi Milioni tatu kutokana na gharama ilizotumia kurekodi nyimbo tatu ambazo sauti yake ipo pamoja na Video hali iliyofanya nyimbo hizo zishindwe kurushwa hewani. Panduka alirekodi wimbo uitwao Kaumia, U Still Mine na Mpenzi Issa huku Video za Kaumia na U Still Mine zikiwa zimetengenezwa.

No comments:

Post a Comment