Monday, June 17, 2013

WABUNGE WA CHADEMA WAGOMA KUINGIA BUNGENI KUFUATIA BOMU LA ARUSHA, IGP ATOA NAMBA YAKE KWA MTU YEYOTE MWENYE TAARIFA NA SERIKALI YATENGA MIL 100 KWA ATAKAEFANIKISHA KUKAMATWA KWA MAGAIDI

Wakati Jeshi la Polisi nchini limesema limepata taarifa za mwonekano wa mtu aliyetupa bomu katika mkutano wa kampeni wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Arusha,Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe amesema wabunge wake leo hawataingia bungeni.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mbowe alisema wabunge hao watawasili Arusha kwa ajili ya kuungana na wananchi pamoja na wanachama kwenye msiba huo.

Alisisitiza kwamba kuanzia leo mahema yatawekwa viwanja vya Soweto kwa ajili ya kuomboleza msiba huo na  mara polisi wakimaliza uchunguzi wao na kutoa majibu juu ya vifo hivyo, marehemu hao watasafirishwa.

Wakati Mbowe anatoa kauli hiyo Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi akizungumza jana mjini Arusha na waandishi wa habari, alisema taarifa za awali zinaonesha mlipuko huo ni bomu la kutupwa kwa mkono (grumeti)  na hivi sasa timu ya wataalamu  ikiongozwa na Kamishna wa Operesheni Maalumu wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
 
Naye  Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini,  Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema  katika taarifa yake kwa vyombo vya habari ameahidi kupambana na kuhakikisha wahusika wanapatikana.
 
Alitoa taarifa hiyo jana kwa waandishi wa habari Dar es Salaam na kusema hadi jana, watu waliothibitika kufa katika tukio hilo ni wawili na 68 ni majeruhi.
 
Waliokufa ni Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha) wa Chadema, Kata ya Sokoni 1, Judith Moshi (25) na mtoto aliyejulikana kwa jina moja la Justin.
 
"Mpaka hivi sasa  watu waliokufa ni wawili  na wengine 68 wamejeruhiwa na mlipuko huo, lakini naahidi kuwa tutapambana na kuhakikisha tunawapata wahusika," alisema Mwema.
 
Sanjari na kupatikana taarifa juu ya mtu aliyetupa bomu, Mwema alisema  timu ya jeshi hilo imetumwa kutoka makao makuu kwenda Arusha kuongeza nguvu katika upelelezi.

Hata hivyo, hakufafanua zaidi juu ya mtuhumiwa huyo kutokana na kile alichosema taarifa husika  zinafanyiwa uchunguzi  kabla ya  kuwakamata watu sahihi waliohusika na tukio hilo.

Kwa mujibu wa IGP Mwema, timu ya polisi kutoka Makao Makuu inayoongozwa na makamishna wawili, imeondoka  kwenda mkoani Arusha kuongeza nguvu katika operesheni na upelelezi.
 
Timu hiyo inaongozwa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja na Isaya Mngulu kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, wakishirikiana na vyombo vingine vya ulinzi.
 
Alisema polisi inafanya operesheni kali nchini kote kuhakikisha inawatia mbaroni watu wote waliowezesha, waliofadhili na waliotenda uhalifu huo.
 
"Kikubwa wananchi waendelee kuwa watulivu na waendelee kutoa ushirikiano kwa wakati wote uchunguzi ukiendelea," alisema.

IGP ametaka mtu yeyote atakayekuwa na taarifa za wahalifu hao, atoe taarifa kupitia namba yake ya simu ambayo ni 0754 785557 au kwenye kituo chochote cha polisi ili wakamatwe.

Wakati huo huo serikali kupitia bunge imetoa taarifa kuhusu tukio hilo la bomu na imetenga kiasi cha shilingi milioni 100 kwa yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya ugaidi.

No comments:

Post a Comment