Tuesday, June 18, 2013

CHADEMA YASEMA KITENDO CHA SERIKALI KUTANGAZA DAU LA MIL. 100 NI UTUMIAJI MBAYA WA RASILIMALI ZA TAIFA



Chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA kimesema kitendo cha serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, uratibu na Bunge Mh. William Lukuvi bungeni jana, kutangaza dau la Shilingi Mil 100 kwa yeyote atakayefichua taarifa za tukio la kihalifu lililotokea Arusha mwishoni mwa wiki si la kiungwana.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya chama hicho jijini Dar Es Salaam, Mkurugenzi wa habari na mawasiliano Mh. John Mnyika amesema kitendo cha serikali kutangaza dau hilo la shilingi mil. 100 ni utumiaji mbaya wa rasilimali za Taifa na kuitaka serikali kutumia pesa hizo kwa kusaidia famili za watu waliopoteza maisha bila hatia katika matukio mbalimbali akitolea mfano wa familia ya aliyekuwa mwandishi wa habari, marehemu Daud Mwangosi.

Akizungumzia kauli iliyotolewa na kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni na mwenyekiti wa chadema Mh. Feeman Mbowe, Mh. Mnyika amesema chama kimetoa Baraka zote kwa mwenyekiti huyo kutokana na kauli hiyo na kuanzia sasa Wabunge wote wa Chadema hawatoshiriki na hawaruhusiwi kushiriki vikao vya Bunge vinavyoendelea mpaka hapo taratibu za maombolezo zitakapokamilika.

Aidha Mh. Mnyika ameongeza kuwa chadema haijafurahishwa na kitendo cha Bunge kutositisha shughuli zake kutokana na tatizo la Arusha wakati majanga mengine kama hayo yanapotokea Bunge husitisha shughuli zake na taratibu zingine hufuata.

Wakati huo huo MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Mh. Freeman Mbowe amefichua siri kuhusu tukio la mlipuko wa bomu lililotokea jusi katika viwanja vya Soweto, jijini Arusha.

Katika kauli yake jana, Mbowe ameibua tuhuma nzito dhidi ya Jeshi la Polisi, ambapo alidai kuwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) ndiye aliyerusha bomu hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa,baada ya kutembelea majeruhi katika Hospitali ya Selian, Mbowe alisema chama chake kina ushahidi wa kutosha juu ya askari huyo kurusha bomu.

Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni,alisema wamefanikiwa kupata ushahidi wa kutosha juu ya tukio hilo baya linalochafua taswira ya nchi.

Alisema chama chake kipo tayari kuweka ushahidi huo hadharani, iwapo Serikali itaendelea kufanya siasa na kuficha ukweli.
 

No comments:

Post a Comment