Friday, June 28, 2013

Rama Dee na Lady JD, hatimaye!

Wanamuziki wakongwe toka nchi Tanzania, Lady Jay dee na Rama Dee wamejipanga kutoa wimbo wa pamoja hivi karibuni, wakali hawa wanaaminika kuwa wanaweza sana miondoko ya R&B kwahiyo huo moto wake nahisi utakuwa balaa.

Rama Dee ambaye kimakazi anaishi nchini Australia kwa sasa amesema wimbo hoo ni kwaajili ya mashabiki wake pamoja na mwanadada Lady Jay Dee hivyo amesema anaomba sapoti yao maana bila mashabiki anaamini kuwa msanii hawezi fika kokote.

"Wimbo tumefanya mimi la Lady Jay dee na utatoka muda si mrefu, mashabiki wakae mkao wa kula maana tumejitahidi kadiri ya uwezo wetu ili kuhakikisha tunatoa wimbo ambao utawafurahisha mashabiki wetu na kuongeza ukaribu zaidi kwetu na wao".

Basi sawa, wananchi wanasubiri kwa hamu maana wengi walikuwa wana hamu ya kuona wawili hawa wakifanya kolabo, naamini maombi ya wengi sasa yamesikilizwa.

Thursday, June 27, 2013

MWENYEKITI WA CHADEMA JOHN HECHE ASEMA NI AIBU KWA NCHI KUFANYA USAFI KWA SABABU YA WAGENI

Mwenyekiti wa Baraza la vijana Chadema (BAVICHA) John Heche (pichani)amesema, kitendo cha Serikali kuamuru usafi ufanyike katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar Es Salaam pamoja na kuwahamisha wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao kandokando ya barabara kwa sababu ya ujio wa Rais wa Marekani ni aibu kwa Taifa.

Akizungumza leo jioni kwenye kipindi cha Hot Mix kinachoruka kupitia EATV, Heche alisema pamoja na sababu zinazodaiwa na viongozi wa serikali kuhusu kuhamishwa kwa wafanyabiashara hao, lakini moja ya sababu kubwa ni ujio wa Rais Obama anayetarajia kufika Nchini Julai 1 kwa ziara ya kikazi ya siku tatu na kusisistiza kuwa ni aibu kubwa kwa Taifa kwa maana hatuwezi kufanya usafi mpaka tusikie kuna wageni.

Akijibu swali la Mtangazaji wa kipindi hicho Adrian Hilary Stepp kuwa kwa nini vurugu hizo zinazotokea mara kwa mara wakati wa mikutano ya chama chao(CHADEMA) pekee na si vyama vingine vya upinzani, Heche alisema kwa sababu chama chao ndicho chenye nguvu na kinaipa Presha chama Tawala hivyo hufanya mipango hiyo ya vurugu ili kuwatisha wananchi wasihudhurie mikutano yao akitolea mfano wa vurugu za Arusha zilizosababishwa na kurushwa kwa bomu na kuongeza kuwa bomu hilo lilikuwa na mkono wa serikali.

Kaseja, Sunzu kwaheri Simba.


Uongozi wa Simba kuamua kumtema mchezaji wao Juma Kaseja wamesema imetokana na maneno ya watu yanayoendelea huko mitaani, hali inayosababisha wao kuamua kumuacha Juma Kaseja aende akajaribu sehemu nyingine.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, mwenyekiti wa Simba kamati ya usajili , Zakaria Hanspope alikuwa na haya ya kusema

“Unajua Juma Kaseja amechezea timu ya Simba kwa miaka mingi sana, laikini hivi karibuni kumezuka maneno ya ajabu kuhusu Juma Kaseja kuuza mechi anapokuwa uwanjani, kwahiyo kama uongozi tumeoa hali hii haitoleta picha nzuri kwa timu yetu.

Kiongozi huyo alidai kuwa sababu zingine hawatopenda kuziweka wazi ila kubwa ni kuhusiana Juma Kaseja kutoaminiwa na baadhi ya mashabiki na kudai kuwa , kwa sasa anapocheza uwanjani na timu zingine basi huwa anaamua kuuza mechi na kufungwa ili wapinzani waweze kushinda.

“Kwahiyo kama viongozi wa simba tumeona hali hii ya mashabiki kumsema kuwa Juma Kaseja anauza mechi kwa wapinzani, itapunguza kiwango chake cha uchezaji, hata yeye anaposikia haya maneno ile munkari ya kucheza inaisha kabisa sababu watu ambao anacheza kwaajili yao hawamuamini tena” Alisema Zakaria Hanspope

Aidha Zakaria Hanspope akielezea kuhusiana na mchezaji Felix Sunzu alisema kuwa masuala ya malipo ndiyo yameleta utata kati yao

“Felix Sunzu anataka tumlipe pesa kubwa zaidi ambayo ni dola 3500, ukingalia bajeti yetu kwa sasa hicho kiwango cha pesa ni kikubwa na itakuwa kazi kumlipa , kwahiyo tumeakuwa tukibishana katika malipo, yeye amesimamia kiwango hicho na sisi hatuna uwezo wa kumlipa hicho kiwango kwa sasa”. Alisema mwenyekiti wa Simba kamatii ya usajili, Zakaria Hanspope

Wednesday, June 26, 2013

BAKHRESA AIOKOA BANDARI


Huu ndio muonekano mpya wa bandari ya Zanzibar, eneo la bandari ya malindi hasa lile eneo la boti ndogo ziendazo kwa kasi.

Kutokana na Serikali kutokuwa na uwezo hali iliyopelekea kushindwa kuliendeleza iliamua kumkabidhi mfanya biashara mzalendo, Bw Said Bakhresa.

Eneo hilo wakati lilipokuwa chini ya serikali lilikuwa kama gofu tu maana halikuwa na hadhi hata ya kuitwa bandari, lakini baada ya kumkabidhi Said Bakhresa mabadiliko yalianza kuonekana kwa muda mfupi na sasa jengo limependeza na naweza thubutu sema hakuna jengo la bandari linalofanana na hilo Tanzania.

Serikali iliweza kufanya jambo la maana kwa kumkabidhi Bwana Said Bakhresa kulifanyia marekebisho hilo jengo, na pia hata kwa maeneo mengine ambayo serikali inaona haiwezi kuyakarabati, basi ikabidhi wazalendo wa hapa nchini wanaoweza kuyarekebisha.

TENDWA ATATANISHA WANANCHI


Msajili wa Vyama vya Siasa nchini John Tendwa,  amedai kuwa ikibainika kuwa CHADEMA ndio waliohusika katika kulipua bomu katika mkutano wao wa 15/06/2013 atakifuta.
Tendwa  ameyasema   hayo alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Hot Mix cha East Africa Television akijibu swali la mtangazaji wa kipindi Adrian Stepp  kuhusu  hatua  zitakazochukuliwa...
Alipoulizwa kama itathibitika kuwa CCM ndio walihusika kulipua bomu hilo amedai kuwa hawezi kukifuta kwakuwa kwa kufanya hivyo itakuwa ni kufanya mapinduzi ya kalamu na jeshi linaweza kutawala nchi.
Pia  jaji Tendwa akiwa kwenye mjadala, amekanusha kuwa mhe Mizengo Pinda hakusema askari wapige wananchi, ni upotoshaji tu wa wanahabari na kuongeza kuwa wanahabari wanapaswa kumtafuta mhusika pale anapotoa habari ili kupata ufafanuzi zaidi wa habari hiyo.

KAMA MIPAKANI WANAFANYA UKAGUZI, MADAWA YA KULEVYA YANATOKA WAPI?



Leo ni siku ya kupambana na madawa ya kulevya kitaifa, na takwimu zinaonesha kuwa mkoa wa Dar Es Salaam unaongoza kwa kuwa na watumiaji pia waathirika wengi wa madawa ya kulevya, hii inatokana na mkoa huu kuwa na starehe karibia zote.
Mkoa  wa pili kwa biashara za madawa ya kulevya nchini Tanzania, unatajwa kuwa ni mkoa wa Tanga na hii inatokana na bandari ya Tanga, hivyo kusababisha shughuli za uingizaji wa madawa kutoka nje kufanyika katika eneo hilo kwa wingi, hali inayofanya wakazi wengi wa Tanga kupata madawa hayo kwa urahisi zaidi.
Madawa ya kulevya yanatajwa kuwa chanzo kikuu cha kuharibu akili ya mtu kwa kushindwa kujielewa na kufanya maamuzi yasiyo sahihi, hali hi husababisha mtu kushindwa kufanya kazi kwa usahihi na hali ya umaskini kumvaa kwa wingi.
Madawa ya kulevya yanasababisha tumkumbuke shujaa marehemu Amina Chifupa, aliyejitolea kupambana na madawa ya kulevya enzi za uhai wake ila harakati hizo zilisizi baada ya mh. Huyu kufariki dunia, hadi sasa bado hajatokea  mwenye harakati kama zake za kupambana na madawa ya kulevya.
Wanamuziki wengi wa hapa nchini Tanzania wamekumbwa na tatizo hili, tunakumbuka hata enzi za uhai wake mwanamuziki Langa Kileo aliwahi kukiri kutumia madawa ya kulevya na alisema kuwa ameacha kutumia madawa hayo baada ya kuona yanamharibia maisha yake.
Hii pia inatukumbusha kuwa vijana wengi kwa sasa madawa yanawaharibu sana, wapo wachache ambao ni watu maarufu tu ndio tunajua kuwa wanatumia, lakini kwa upande wa pili wapo watu wengi nchini Tanzania ambao sio maarufu na wanatumia haya madawa na wengi wao yanawaua na kusababisha taifa kupata hasara kubwa kila siku.
WITO KWA SERIKALI:
Katika hali ya kushangaza nchini Tanzania eti wanasema mipakani kuna watu wa kukagua madawa ya kulevya na kasoro zingine, uwanja wa ndege na hata bandarini kuna askari kibao wa kitengo cha madawa ya kulevya, swali linakuja.


 Je, huwa wanapokagua hao watu hawayaoni hayo madawa ya kulevya maana watu wanapita na hakuna anayekamwatwa lakini mwisho wa siku madawa unakuta yamesambaa kwa wingi nchini.
Imefikia wakati sasa serikali iache kucheza na akili za watanzania, mtu akiwa na madawa akamatwe na aadhibiwe masuala ya baadhi ya polisi kupokea rushwa na kuruhusu watu wa madawa ya kulevya kuyaingiza, yamepitwa na wakati, tunahitaji mabadiliko toka serikalini ili kufikia malengo ya millennia.

SAY NO TO DRUGS

Monday, June 24, 2013

OMMY DIMPOZ ALIVYOPIGWA MAKOPO DODOMA AIITA 'MAKOPO STYLE'

Msanii Ommy Dimpoz ambaye alipondwa na makopo ya vinywaji mjini Dodoma juzi katika show ya KILI MUSIC TOUR 2013, tayari ameipa jina staili hiyo kupitia ukurasa wake wa Twitter

"ha ha ha hiyo ni Makopo style ukirusha Nakwepa nikilidaka nakupa nalo la uso", hayo ni maneno aliyotweet Ommy Dimpoz leo asubuhi wakati akichat na baadhi ya watu.

Pia akiendelea kutweet amesema kuwa sasa amejipanga kamili kwa mashabiki wote watakaorusha hizo vitu akiwa stejini.

"hahahahaha kuna moja nililirudisha na teke nikasikia shabiki kapiga yowee YALAAAA nikajua litakuwa la kichwa hilo".

Dah, hii kali sasa, patamu hapo. Na wadau wengine wameipa staili hiyo jina la 'Rusha nikwepe Ooo me n you'
.

Friday, June 21, 2013

MHESHIMIWA MACHALI AMELAZWA KATIKA HOSPITALI YA RUFAA DODOMA BAADA YA KUVAMIWA NA MUPIGWA JANA JIONI

Mbunge wa Kasulu mjini Mh. Moses Machali amelazwa katika Hospitali ya Rufaa mjini Dodoma kufuatia kuvamiwa na kujeruhiwa na watu wasiojulikana katika maeneo ya Ipagala mkoani Dodoma.

Tukio hilo lilitokea jana jioni wakati Mh. Machalli akiwa kwenye gari lake baada ya kuwapigia honi vijana kadhaa waliokuwa katikati ya barabara ili wasogee pembeni ili naye aweze kupita .

  Vijana hao walioonekana kuchukizwa na kitendo hicho cha kupigiwa honi hivyo walianza kuishambulia gari hiyo ya Mh. Machali kwa kuigonga kwa nguvu jambo ambalo lilimfanya Machalli kusimamisha gari na kushuka ili kuzungumza na vijana hao waweze kufikia muafaka.

Baada ya Machali kushuka,  vijana hao walianza kumshambulia kwa matusi ya nguoni na ndipo Machalli aliamua kuwajibu kwa hasira kitendo kilichasababisha vijana hao waanze kumsahambulia kwa kumpiga.

Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo ni kwamba vijana hao waliompiga Mh. Machali walikuwa zaidi ya nane na ndiyo sababu ya yeye kushindwa kumsaidia Mheshimiwa huyo kwa kuhofia kuunganishwa katika kipigo.

Chanzo makini cha Blog hii kimemtembelea Mh. Machali Hospitalini hapo na kwamba wakati yeye akiwasili katiak Wodi namba 18 alimkuta akiwa amelala hivyo hakuweza kuzungumza nae chochote na kuzungumza na muuguzi wa zamu aliyefahamika kwa jina la Zainab na kusema kuwa walimpokea Mh. Machali majira ya saa 5 usiku jana ambapo alifikishwa na askari Polisi ambao walifika katika eneo la Ipagala alipovamiwa Mheshimiwa ili kumpa msaada na kufanikiwa kumkimbiza hospitalini hapo.

Aidha awali Mheshimiwa Machali mwenyewe alikiri kuwa anaamini kuwa watu hao waliomfanyia kitendo hicho ni wahuni tu kwa kuwa hana ugomvi na mtu yeyote kwa sasa hivyo hafikirii kama ni njama za watu fulani ila ni wahuni tu.

Hata hivyo taarifa zaidi zinasema kuwa eneo hilo la Ipagala si salama sana kwa sasa kwa sababu kuna vibaka wengi ambao hufanya matukio kama hayo ya uhalifu mara kwa mara.

Blog hii inamtakia kheri Mheshimiwa Machali aweze kupona ili arejee katika shughuli zake za ujenzi wa Taifa.




Tuesday, June 18, 2013

CHADEMA YASEMA KITENDO CHA SERIKALI KUTANGAZA DAU LA MIL. 100 NI UTUMIAJI MBAYA WA RASILIMALI ZA TAIFA



Chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA kimesema kitendo cha serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, uratibu na Bunge Mh. William Lukuvi bungeni jana, kutangaza dau la Shilingi Mil 100 kwa yeyote atakayefichua taarifa za tukio la kihalifu lililotokea Arusha mwishoni mwa wiki si la kiungwana.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya chama hicho jijini Dar Es Salaam, Mkurugenzi wa habari na mawasiliano Mh. John Mnyika amesema kitendo cha serikali kutangaza dau hilo la shilingi mil. 100 ni utumiaji mbaya wa rasilimali za Taifa na kuitaka serikali kutumia pesa hizo kwa kusaidia famili za watu waliopoteza maisha bila hatia katika matukio mbalimbali akitolea mfano wa familia ya aliyekuwa mwandishi wa habari, marehemu Daud Mwangosi.

Akizungumzia kauli iliyotolewa na kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni na mwenyekiti wa chadema Mh. Feeman Mbowe, Mh. Mnyika amesema chama kimetoa Baraka zote kwa mwenyekiti huyo kutokana na kauli hiyo na kuanzia sasa Wabunge wote wa Chadema hawatoshiriki na hawaruhusiwi kushiriki vikao vya Bunge vinavyoendelea mpaka hapo taratibu za maombolezo zitakapokamilika.

Aidha Mh. Mnyika ameongeza kuwa chadema haijafurahishwa na kitendo cha Bunge kutositisha shughuli zake kutokana na tatizo la Arusha wakati majanga mengine kama hayo yanapotokea Bunge husitisha shughuli zake na taratibu zingine hufuata.

Wakati huo huo MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Mh. Freeman Mbowe amefichua siri kuhusu tukio la mlipuko wa bomu lililotokea jusi katika viwanja vya Soweto, jijini Arusha.

Katika kauli yake jana, Mbowe ameibua tuhuma nzito dhidi ya Jeshi la Polisi, ambapo alidai kuwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) ndiye aliyerusha bomu hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa,baada ya kutembelea majeruhi katika Hospitali ya Selian, Mbowe alisema chama chake kina ushahidi wa kutosha juu ya askari huyo kurusha bomu.

Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni,alisema wamefanikiwa kupata ushahidi wa kutosha juu ya tukio hilo baya linalochafua taswira ya nchi.

Alisema chama chake kipo tayari kuweka ushahidi huo hadharani, iwapo Serikali itaendelea kufanya siasa na kuficha ukweli.
 

Monday, June 17, 2013

MWILI WA MSANII LANGA KUAGWA NA KUZIKWA LEO KATIKA MAKABURI YA KINONDONI

Mwili wa aliyekuwa msanii wa muziki wa Bongo Fleva Langa Kileo(Langa) aliyefariki Alhamis ya wiki iliyopita, unatarajiwa kuagwa na kutolewa heshima za mwisho leo majira ya mchana nyumbani kwao Mikocheni jijini Dar Es Salaam na safari ya kuelekea katika makaburi ya kinondoni ambapo ndipo mwili wake utahifadhiwa itaanza majira ya saa 8 mchana.
Tunatoa pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na mashabiki wa mwanamuziki huo na Mwenyezimungu aiweke roho ya marehemu Langa mahali pema peponi, Amina.

WABUNGE WA CHADEMA WAGOMA KUINGIA BUNGENI KUFUATIA BOMU LA ARUSHA, IGP ATOA NAMBA YAKE KWA MTU YEYOTE MWENYE TAARIFA NA SERIKALI YATENGA MIL 100 KWA ATAKAEFANIKISHA KUKAMATWA KWA MAGAIDI

Wakati Jeshi la Polisi nchini limesema limepata taarifa za mwonekano wa mtu aliyetupa bomu katika mkutano wa kampeni wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Arusha,Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe amesema wabunge wake leo hawataingia bungeni.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mbowe alisema wabunge hao watawasili Arusha kwa ajili ya kuungana na wananchi pamoja na wanachama kwenye msiba huo.

Alisisitiza kwamba kuanzia leo mahema yatawekwa viwanja vya Soweto kwa ajili ya kuomboleza msiba huo na  mara polisi wakimaliza uchunguzi wao na kutoa majibu juu ya vifo hivyo, marehemu hao watasafirishwa.

Wakati Mbowe anatoa kauli hiyo Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi akizungumza jana mjini Arusha na waandishi wa habari, alisema taarifa za awali zinaonesha mlipuko huo ni bomu la kutupwa kwa mkono (grumeti)  na hivi sasa timu ya wataalamu  ikiongozwa na Kamishna wa Operesheni Maalumu wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
 
Naye  Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini,  Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema  katika taarifa yake kwa vyombo vya habari ameahidi kupambana na kuhakikisha wahusika wanapatikana.
 
Alitoa taarifa hiyo jana kwa waandishi wa habari Dar es Salaam na kusema hadi jana, watu waliothibitika kufa katika tukio hilo ni wawili na 68 ni majeruhi.
 
Waliokufa ni Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha) wa Chadema, Kata ya Sokoni 1, Judith Moshi (25) na mtoto aliyejulikana kwa jina moja la Justin.
 
"Mpaka hivi sasa  watu waliokufa ni wawili  na wengine 68 wamejeruhiwa na mlipuko huo, lakini naahidi kuwa tutapambana na kuhakikisha tunawapata wahusika," alisema Mwema.
 
Sanjari na kupatikana taarifa juu ya mtu aliyetupa bomu, Mwema alisema  timu ya jeshi hilo imetumwa kutoka makao makuu kwenda Arusha kuongeza nguvu katika upelelezi.

Hata hivyo, hakufafanua zaidi juu ya mtuhumiwa huyo kutokana na kile alichosema taarifa husika  zinafanyiwa uchunguzi  kabla ya  kuwakamata watu sahihi waliohusika na tukio hilo.

Kwa mujibu wa IGP Mwema, timu ya polisi kutoka Makao Makuu inayoongozwa na makamishna wawili, imeondoka  kwenda mkoani Arusha kuongeza nguvu katika operesheni na upelelezi.
 
Timu hiyo inaongozwa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja na Isaya Mngulu kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, wakishirikiana na vyombo vingine vya ulinzi.
 
Alisema polisi inafanya operesheni kali nchini kote kuhakikisha inawatia mbaroni watu wote waliowezesha, waliofadhili na waliotenda uhalifu huo.
 
"Kikubwa wananchi waendelee kuwa watulivu na waendelee kutoa ushirikiano kwa wakati wote uchunguzi ukiendelea," alisema.

IGP ametaka mtu yeyote atakayekuwa na taarifa za wahalifu hao, atoe taarifa kupitia namba yake ya simu ambayo ni 0754 785557 au kwenye kituo chochote cha polisi ili wakamatwe.

Wakati huo huo serikali kupitia bunge imetoa taarifa kuhusu tukio hilo la bomu na imetenga kiasi cha shilingi milioni 100 kwa yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya ugaidi.

STEPS ENTERTAINMENT YATOA TUZO KWA WASANII WALIOFANYA NAO KAZI KWA MWAKA 2012/13

Baadhi ya wasanii wa kiume wa Bongo movie wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kukabidhiwa tuzo zao za mwaka 2012 zilizoandaliwa na Steps Entertainment na kudhaminiwa na kampuni ya steps Solar
Mkurugenzi wa Kampuni ya Steps Entertainment bwana Dilesh Solanki akifafanua jambo kabla ya kumkabidhi tuzo ya mwogozaji bora wa filamu nchini kwa mwaka 2012 tuzo iliyochukuliwa na Mkurugenzi wa RJ Company bwana Vincent Kigosi(Ray) wakati wa utoaji wa tuzo hizo zilizofanyika usiku wa June 15 katika ukumbi wa Blue Pearl Hotel Ubungo jijini DSM na kuhudhuliwa na wasanii na wadau wa Filamu nchini.
Ridhiwani Kikwete (wa tatu kushoto) akiwapongeza baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya Kanumba the great iliyokuwa inamilikiwa na marehemu Steven Kanumba baada ya kuwakabidhi Tuzo ya Movie iliyofanya vizuri sokoni 2012/2013
Ridhiwani Kikwete (kushoto) akimkabidhi tuzo msanii Haji Adamu(Baba Haji) kwa niaba ya Jimmy Mponda aliyeshinda tuzo ya msanii bora wa Filamu za Action wakati wa utoaji wa tuzo hizo.
Riyama Ally akipokea Tuzo yake
Jacob Steven alichukua tuzo ya msanii bora wa kiume 2012/2013 wakati kwa upande wa wanawake tuzo hiyo ilinyakuliwa na mrembo Irene Uwoya
Mtoto Jenipher nae akipokea tuzo yake, ambapo aliliza wengi baada ya kushindwa kutoa neno la shukrani na alipofika sehemu ya kumshukuru Uncle JJ(Marehemu Kanumba) alishindwa kuendelea na kuanza kulia.
Msanii Nice Mohamed a.k.a Mtunisi akipokea tuzo yake ya filamu yenye ujumbe
Amri Athumani a.k.a Mzee Majuto nae akipokea Tuzo yake ya msanii bora wa vichekesho