Dk. Joyce Ndalichako
BARAZA
la Mtihani la Tanzania (Necta), limetangaza matokeo ya mitihani ya
kidato cha sita iliyofanyika Februari mwaka huu yakionyesha kuongezeka
kidogo kwa kiwango cha ufaulu kwa ujumla huku wavulana waliofaulu
wakiwaacha mbali wasichana.
Katika
matokeo hayo yaliyotangazwa jana na Katibu Mtendaji wa Baraza la
Mitihani la Tanzania (Necta), Dk Joyce Ndalichako (pichani), kati ya
watahiniwa 46,499 waliofanya mtihani huo, wavulana waliofaulu ni 30,466
wakati wasichana ni 16,033. Hata hivyo, kumekuwa na mchuano mkali katika
ufaulu kwa asilimia ambao wasichana walipata 87.37 na wavulana 87.69.
Sekondari
ya Wasichana ya Marian, Bagamoyo ndiyo iliyoongoza kitaifa na
mwanafunzi wake, Faith Assenga ndiye aliyeshika namba moja katika masomo
ya Sayansi.
“Katika
masomo ya Biashara, aliyeshika nafasi ya kwanza ni Alex Isdor wa
Sekondari ya Kibaha na Lugha ni Faridi Abdallah wa Sekondari ya
Mpwapwa,” alisema Dk Ndalichako.
Dk
Ndalichako alisema kiwango cha kufaulu kwa watahiniwa 46,499; wakiwemo
wale wa kujitegemea, kimeongezeka kutoka asilimia 87.24 mwaka jana hadi
87.58 mwaka huu.
|