Tuesday, July 2, 2013

WATANZANIA WALIVYOJITOKEZA KUMLAKI OBAMA BARABARANI

Rais Jakaya Mrisho kikwete akimsindikiza mgeni wake baada ya kumpatia mapokezi ya kihistoria leo Ikulu.

Na chini ni picha zinazoonyesha wananchi wa jiji la Dar Es Salaam walivyojitokeza kumlaki Rais huyo wa Marekani katika maeneo tofauti ya jiji ambapo msafara wa Rais huyo ulipita.



Ziara ya Rais wa Marekani Barack Obama barani Afrika imehitimishwa leo, baada ya kuwasili nchini Tanzania hapo jana akitokea Afrika kusini.

Obama ambae aliambatana na mkewe Michelle Obama pamoja na mabinti zao alipokelewa na mwenyeji wake Rais Jakaya Mrisho Kikwete  na mkewe  Mama Salma Kikwete katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere na kisha kuelekea Ikulukisha ambapo alifanya mazungumzo na waandishi wa habari kabla ya kushiriki dhifa ya pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali hapo hapo Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais Obama amekamilisha ziara yake kwa kutembelea kituo cha kuzalisha umeme cha Symbion kilichopo Ubungo jijini Dar Es Salaam, baada ya nchi yake kuahidi kutoa dola za Marekani bilioni saba kusaidia mradi wa umeme Barani Afrika.

Katika ziara yake Barani Afrika iliyoanzia nchini Senegal, Afrika kusini na hatimaye nchini Tanzania Obama amekuwa akisisitiza suala la demokrasia ambapo ameeleza kuwa Afrika itakuwa na mustakabali mzuri kwa kuwa na viongozi wanaopambana kuhakikisha raia wao wanakuwa na maisha bora.

Katika ziara yake nchini Afrika Kusini , Rais Obama hakusita kusifu jitihada za kiongozi wa zamani na baba wa taifa hilo Nelson Mandela ambaye ameeleza kuwa jitihada zake za ukombozi kwa raia wa taifa hilo zilimsukuma kuingia katika siasa na hatimaye kuwa Rais wa kwanza mweusi nchini Marekani.

Hata hivyo wakati wa ziara yake Nchini Tanzania, Rais Obama hapo jana alikutana na Rais aliyemwachia madaraka George .W. Bush na kwenda kuweka mashada kwenye ubalozi wa zamani wa marekani uliolipuliwa mwaka 1998.

Bwana Bush yupo Tanzania na mkewe Laura Bush kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa wake wa Marais wa Afrika unaofanyika leo kwa kudhaminiwa na Taasisi ya Bush Foundation.


No comments:

Post a Comment