Thursday, July 18, 2013

Siku ya Mandela leo kuadhimishwa na Yatima, Dar es Salaam

Ubalozi wa Afrika Kusini nchini, umepanga kuadhimisha Siku ya Mandela Duniani hii, kwa kushiriki shughuli mbalimbali za jamii katika kituo cha watoto yatima cha Maria Theresa Dar es Salaam.

Mshauri wa Balozi wa Masuala ya Siasa, Terry Govender, amesema watatumia dakika 67 kufanya kazi mbalimbali ndani ya kituo hicho kwa kushirikiana na watoto wanaolelewa mahali hapo.

Kwa mujibu wa Govender, Ofisi ya Habari na Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa ndio iliyopendekeza kituo hicho kwa mwaka huu.

Kwa maelezo ya mshauri huyo wa siasa, mwaka jana ubalozi huo uliadhimisha siku hiyo kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii katika Shule ya Msingi Tandale ya Dar es Salaam.

"Lengo letu ni kuwashawishi watu wote duniani wawe na utaratibu wa kujihusisha na shughuli za kijamii japo kwa dakika 67, ambazo tunaamini wanaweza kuzitenga na kufanya la maana katika maeneo watakayochagua.

"Siku ya Mandela haimaanishi kutoa msaada, bali kuwajibika kwa jamii katika shughuli mbalimbali. Tutaendelea kuitekeleza ili kuwavuta watu watenge muda wao kuwajibika katika shughuli za jamii," alisema na kuongeza kuwa wataanza kazi kwenye kituo hicho saa 3:30 asubuhi.

Alitaja kazi watakazozifanya kuwa ni kupasua kuni katika magogo yaliyohifadhiwa, ili zitumike kupika kwa urahisi, kukata mboga na kuandaa chakula (kupika), kufanya usafi wa eneo hilo na shughuli nyingine za jamii zitakazo kuwepo wakati huo.

Siku ya Mandela Duniani ilitangazwa rasmi Novemba 2009 na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN), ikilenga kushawishi  jamii duniani kutenga muda kwa kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii.

Kutangazwa huko kwa siku hiyo kulizingatia kujitoa kwa Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela katika shughuli za jamii, ambapo, kwa miaka 67 mfululizo amekuwa akizifanya bila kuchoka.

No comments:

Post a Comment