Friday, August 9, 2013

Watalii waliomwagiwa tindikali Zenji warejea UK

Wanawake wawili waingereza waliochomwa kwa Acid nchini Zanzibar wanatarajiwa kuwasili nchini Uingereza baadaye leo

Kirstie Trup na Katie Gee, wote wenye umri wa miaka 18 kutoka London, walipelekwa hospitalini nchini Tanzania baada ya kushambuliwa Mashariki mwa kisiwa hicho.

Inaaminika kuwa walitoka Tanzania kuelekea Uingereza Alhamisi usiku.

Mama za wasichana hao, Rochelle Trup na Nicky Gee, walielezea kughadhabishwa mno na shambulizi hilo ambalo sababu yake haiwezi kujulikana na ambalo halikuchochewa kivyovyote. Walishambuliwa na wanaume wawili waliokuwa kwenye pikipiki.

Polisi walisema kuwa walirushiwa ACID kwenye nyuso zao, kifuani na kwenye mikono yao walipokuwa wanatembea mjini .

Mwandishi wa BBC anasema kuwa waliowashambulia walitoroka na polisi hawajui kwa nini wanawake hao walilengwa.

Mama za wasichana hao walisema kwenye taarifa yao kuwa walighadhabishwa mno na shambulizi hilo na hawaelewi kwa nini wasichana hao walishambuliwa ili hali walikwenda Zanzibar kwa nia njema.

''Tunashukuru kwa wale wanaotaka kujua kinachoendelea lakini tungeomba vyombo vya habari vituwache kwa sasa hadi tutakapokutana na watoto wetu,'' walisema akina mama hao.

Wasichana hao walikuwa wamekaa Zanzibar kwa muda wa wiki mbili ingawa walitarajiwa kuwa huko kwa wiki tatu, kupitia kwa kampuni ya usafiri ya i-to-i Travel, ambayo ilisema inafanya kila iwezalo kuwarejesha nyumbani Uingereza.

Kari Korhonen, mkurugenzi mwenza wa kampuni ambayo wasichana hao walikuwa wanafanyia kazi, alisema kuwa hali yao si mbaya ikizingatiwa athari za Acid kwa mwili na visa ambavyo vimewahi kushuhudiwa vya kuchomwa kwa ACID.

Msemaji mwingine aliongeza kuwa wasichana hao walikuwa njiani kuelekea kwa maankuli ya jioni wakati wa shambulizi hilo.

No comments:

Post a Comment