Thursday, September 5, 2013

Daktari feki akamatwa hospitali ya KCMC, moshi



HALI ya wasiwasi imetanda kwa baadhi ya wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya mjini Moshi baada ya uongozi wa hospitali hiyo kumkamata mtu mmoja anayedaiwa kujifanya ni daktari wa watoto akiwa kwenye wodi ya upasuaji.

 Daktari huyo feki aliyefahamika kwa jina la , Alex Sumni Massawe alikamatwa jana majira ya saa 5 asubuhi na kuwekwa chini ya ulinzi mkali wa makachero wa Jeshi la Polisi waliokuwa wamevalia nguo za kiraia baada ya kukutana na mmoja wa wagonjwa ambaye alimuahidi kumfanyia mwanae wa kiume upasuaji wa ngozi.

 Kabla ya kukamatwa kwa Alex, mama mzazi wa kijana aliyekuwa akitakiwa kufanyiwa upasuaji, Pamvelina Shirima alikutana na daktari huyo katika baa moja maarufu mjini hapa iliyopo eneo la Dar Street (jina limehifadhiwa) na kumtoza sh.200,000 akidai zitatumika kuharakisha mwanae afanyiwe vipimo vya upasuaji.

Alex anadaiwa alitaka kumfanyia upasuaji kijana, Makasi Tipesa, mkazi wa Manispaa ya Moshi ambaye amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya ngozi kwa muda mrefu sasa.

 Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya KCMC, Bw. Gabriel Chisseo alisema daktari huyo aliwekewa mtego na uongozi wa hospitali ya KCMC kutokana na baadhi ya wagonjwa kuripoti kutapeliwa na mmoja wa madaktari ambaye amekuwa akijinasibu kwamba anafanya huduma hiyo kutokana na wito alionao katika fani hiyo.

 “Leo asubuhi(jana) mteja wetu ambaye amekuwa akitibiwa hapa alitapeliwa na huyu Alex , tulimkamata akiwa wodi ya upasuaji baada ya kupokea kiasi cha sh.200,000 kutoka kwa Pamvelina Shirima ambaye alimleta mwanae afanyiwe upasuaji wa ngozi”, alisema Chisseo.

Uongozi wa Hospitali ya KCMC umethibitisha kwamba mtu huyo aliyekamatwa ndani ya Hospitali hiyo, si mwajiriwa wao na wala hakukutwa na sare wala kitambulisho kinachomtambulisha kitengo chake cha kazi.

 Hivi karibu kumeibuka matukio ya watu kadhaa kujivika kuwa na taaluma mbalimbali ambazo si za kweli huku jeshi la polisi likifanikiwa kuwakamata wengine wakijifanya kuwa ni maofisa wa jeshi hilo ,wengine usalama wa taifa huku wengine wakijifanya asakri wa kikosi cha usalama barabarani.

No comments:

Post a Comment