Monday, February 4, 2013

WATU WANAODHANIWA KUWA NI MAJAMBAZI WAVAMIA NYUMBANI KWA MAKAMBA

Watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wamevamia nyumbani kwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Mh. January Makamba (pichani) kwa lengo la kufanya uhalifu. 
Hata hivyo majambazi hao ambao walimfunga kamba mlinzi wa nyumba hiyo na kuingia ndani, hawakufanikiwa kuiba chochote. Mh. Makamba amesema kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana wakati yeye akiwa safarini jimboni kwake Bumbuli ila familia yake ilikuwepo nyumbani hapo.
Makamba alisema baada ya majambazi hao kuingia ndani, walimfunga kamba na kumziba mdomo mlinzi.
“Ujambazi huo ulitaka kufanyika nyumbani kwangu Masaki karibu na Ubalozi wa Afrika Kusini, Mimi sikuwepo nyumbani. Walivamia chumbani mke wangu akabonyeza kengele iliyopiga kelele ndio wakakimbia, baada ya majirani kuwasili eneo la tukio, wakatokomea kusikojulikana,” alisema Makamba na kuongeza:
“Waliingia kwenye ofisi yangu ya pale nyumbani na kupekua lakini cha ajabu ni kwamba sebuleni kulikuwa na Ipad na laptop  lakini hawakuvichukua.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba watu hao walitaka kufanya ujambazi, lakini hawakufanikiwa.
Kamanda Kenyela alisema tukio hilo lilitokea saa 10 alfajiri ya kuamkia jana, lakini majambazi hao hawakufanikiwa kutimiza azima yao.
“Walimfunga kamba mlinzi na kufungua dirisha, kisha kuingia ndani. Lakini hawakufanikiwa kuchukua chochote,” alisema Kamanda Kenyella.
Kamanda Kenyella alieleza kuwa majambazi hao hawakufanikiwa kuiba chochote kwa kuwa wakazi wa eneo hilo, walisikia purukushani na kupiga kelele zilizosababisha watu hao kutokomea.
“Haijulikani walikuwa wangapi kwa kuwa hakuna mtu yeyote aliyewaona, lakini katika tukio hilo hakuna aliyejeruhiwa,” alisema Kamanda Kenyella.
Alisema baada ya tukio hilo Jeshi la Polisi Kinondoni, inaendesha msako wa kuwatafuta watu hao ili kuweza kuwatia nguvuni na kuwafikisha mahakamani.

No comments:

Post a Comment