Sunday, February 17, 2013

PADRI EVARIST MUSHI WA KANISA KATOLIKI ZANZIBAR AUAWA KWA KUPIGWA RISASI KICHWANI



Padri Evarist Mushi wa kanisa Katoliki Parokia ya ST. Joseph, Shangani Unguja
 amefariki dunia baada ya kupigwa risasi saa 1.00 asubuhi na kufariki kabla ya kufikishwa hospitalini Mnazi Mmoja visiwani humo.

Padri huyo amepigwa risasi kichwani na kufa papo hapo na watu wasiojulikana wakati  akiwa kwenye gari yake akielekea kuendesha ibada ya saa 3.00 asubuhi ya leo katika kanisa la Mt. Theresia eneo la Mtoni Zanzibar.

Msemaji wa Jeshi Polisi Zanzibar Inspekta Mohamed Mhina amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na amesema kuwa padre huyo ameuawa wakati akijiandaa kuingia kanisani akitokea kwenye gari yake ambapo ndipo alipofikwa na umauti huo.

Jeshi la Polisi visiwani humo kupitia kwa Msemaji wake Mkaguzi wa Polisi, Mohamed Mhina limelaani mauaji hayo na kusisitiza kuwa Jeshi limeanza msako mkali ili kuwabaini wauaji hao.
Hili ni tukio la pili kutokea visiwani Zanzibar ambapo tukio la kwanza lilitokea kwa Padri Ambrose Mkenda kupigwa risasi na kujeruhiwa na watu wasiojulikana.

Mungu ailaze roho ya marehemu Padri Evarist Mushi, Amina.

No comments:

Post a Comment