Tuesday, March 26, 2013

WEMA ASITISHA KUZUNGUMZIA KUHUSU KUMLIPIA FAINI KAJALA


Wema akiwa na Kajala mara baada ya kuachiwa huru kwa Kajala
Baada ya mlimbwende Wema Sepetu kumnusuru msanii mwenzake Kajala kifungo cha miaka saba kwa kumlipia Faini ya Tshs Milioni 13 na vyombo mbalimbali vya habari hapa Nchini kuiripoti taarifa hiyo, Mwanadada huyo ambae ni Staa wa Filamu hapa Bongo amesema ameshaufunga mjadala huo na hayuko tayari kuendelea kulizungumzia suala hilo.

Akizungumza na Blog hii msanii huyo amesema aliamua kumsaidia Kajala kwa moyo wake na kama rafiki yake lakini hakuwa na nia ya kufanya Publicity kama inavyofanywa na vyombo vya habari na kuongeza kuwa kwa ambao tayari wameshafanya hivyo sasa imetosha na binafsi hayuko tayari kuendelea kulizungumzia suala hilo kwani kwa kufanya hivyo atakuwa kama anamsimanga rafiki yake huyo au anajisifu kwa kile alichokifanya kitu ambacho anaona hakitaleta picha nzuri na kitazusha mjadala mwingine kwa jamii.
Kajala alishikiliwa na Polisi na kuwekwa mahabusu mwaka jana kwa kudaiwa kuwa yeye na mumewe Faraja Chambo walikula njama ya kuhamisha umiliki wa nyumba iliyopo Kunduchi Salasala jijini Dar es Salaam,  kinyume na kifungu cha 34 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007,
Pia ilidaiwa kuwa Aprili 14, 2010, walihamisha umiliki wa nyumba kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na katika shitaka la tatu kuwa Kajala na mumewe walidaiwa kuwa  Aprili 14, 2010, wakijua kuwa ni kinyume na sheria, walifanya kosa la kutakatisha fedha haramu.

Friday, March 22, 2013

DEVOTHA NYARUSI MPIGA GITAA WA KWANZA WA KIKE KALUNDE BAND

Mwanamuziki Devotha Nyarusi amekuwa kivutio kikubwa cha Mashabiki wa Kalunde Band kutokana na umahiri wake katika kazi hasa katika upigaji wa Gitaa.

Mwanamuziki huyo alikonga nyoyo za mashabiki pale alipopanda jukwaani na kuanza kulikung'uta Gitaa katika show yao ya jumapili iliyopita ambapo katika Hotel ya Giraffe.

Akizungumzia kitendo hicho cha mwanadada huyo kukung'uta Gitaa na kufanya kuwa kivutio kwa mashabiki waliokuwa ukumbini hapo na kumshangilia kwa nguvu sana, Rais wa Bendi hiyo Deo Mwanambilimbi alisema umahiri wa mwanadada huyo umewadhihirishia mashabiki kuwa Bendi hiyo inaundwa na wanamuziki wenye vipaji vingi na vya hali ya juu na kuongeza kuwa Bendi hiyo pia inakuza vipaji vilivyojificha na havifahamiki katika ulimwengu wa muziki.

Usikose kusikiliza kipindi cha Afrosunday cha East Africa Radio kinachoruka kila Jumapili saa 1 jioni mpaka saa 4 usiku, wiki hii ili kupata mambo mengi zaidi yanayomhusu mwanadada huyo na Kalunde Band kwa ujumla.

MASHUJAA MUSICA WAKANUSHA UVUMI WA CHARLES BABA KUTIMKIA TWANGA


Uongozi wa Mashujaa Band, umesema uvumi ulioenea mtaani kuwa mwanamuziki Charles Baba (pichani) ambae pia ni Rais wa Bendi hiyo ameihama Bendi hiyo na kurudi Twanga alikokuwa akifanya kazi kabla ya kujiunga na Mashujaa si wa kweli ni wa uzushi.

Mkurugenzi wa Bendi hiyo Sakina Mbange maarufu kama Mamaa Sakina alisema kuwa maneno hayo yaliyoenea mitaani ni ya kizushi na kufunguka kuwa ni kweli mwanamuziki huyo pamoja na mwanamuziki mwingine mpiga Tumba maarufu wa bendi hiyo(Mashujaa)  MCD waliwahi kupanda katika jukwaa la Twanga pepeta lakini haimaanishi kuwa wanamuziki hao wamejiunga na Bendi hiyo.

Akizungumza na Blog hii mwanamuziki Charles Baba nae alikanusha vikali uvumi huo na kuwataka mashabiki wake waondoe shaka na kuwahakikishia kuwa bado yeye ni mwanamuziki wa Mashujaa na ana mkataba wa kuitumikia Bendi hiyo na hana mpango wa kuhamia Bendi yoyote nyingine.

Hata hivyo wiki chache zilizopita Charles Baba alizungumzia pia uvumi huo wa yeye kuhamia Twanga Pepeta na kukiri kuwa ni kweli alionekana kwenye jukwaa la Twanga Pepeta kwa ajili ya kujikumbusha na kuonyesha mashabiki kuwa hana Bifu na mkurugenzi wa Bendi hiyo Asha Baraka wala wanamuziki wa Bendi hiyo kama ambavyo wadau wa muziki wanafikiria.

Tuesday, March 19, 2013

ZAIDI YA ASILIMIA 75 YA WAKAZI WA DSM HAWAANGALII TV TANGU ULIPOANZA MFUMO WA DIGITAL


Tangu Tanzania ilipohamia katika mfumo wa Digital mapema mwaka huu ni zaidi ya asilimia 75(75%) ya wakazi wa Dar Es Salaam hawaangalii Televisheni kutokana na kukosa uwezo wa kugharamia ving'amuzi.

Utafiti uliofanywa na wamiliki wa vyombo vya habari Nchini(MOAT) umeonyesha kuwa kwa Mkoa wa Dar es salaam pekee, zaidi ya asilimia 75 ya  wakazi wa jiji hilo hawaangalii channel za TV majumbani kwao tamhu ulipozimwa mtambo wa analog na kuanza kutumika mtambo wa digital na kusababisha umoja huo kuitaka serikali kuangalia upya uwezekano wa kurudisha matangazo ya analog kwanza mpaka Watanzania watakapozoea Digital.

Akizungumza jijini DSM mwenyekiti wa MOAT Dr. Reginald Mengi alisema, “Watanzania wapewe muda kujiandaa ili kutoka analog kwenda digital ifanyike vizuri na kwa mafanikio makubwa, pendekezo letu lilikua ni kwamba analog na digital ziende sambamba mpaka tufike mahali tuone kwamba watu wengi kama sio wote wana vyombo vya kuwawezesha kwenda digital, hilo lifanyike kabla ya tarehe 17 june 2015 ambayo ndio siku ya mwisho ya kutumia analog”

Saturday, March 9, 2013

UHURU KENYATTA ASHINDA URAIS KENYA


Pichani juu na chini ni Uhuru Kenyatta akipiga kura siku ya uchaguzi huo Machi 4,2013
MTOTO wa Rais wa kwanza wa Kenya, Marehemu Jomo Kenyatta, ambaye alikuwa anagombea Urais kwa tiketi ya Chama cha TNA, Uhuru Kenyata ameshinda nafasi hiyo baada ya kumwangusha mpinzani wake Raila Odinga.

Mpaka sasa  Uhuru alikuwa mbele kwa kura 6,173,433 dhidi ya mpinzani wake Raila Odinga aliyekuwa na kura 5, 340,546 ikiwa ni tofauti ya kura 832,887 na majimbo yaliyo kwisha kutangazwa ni 291/291.

Jumla ya kura zote zilizopigwa na kuhesabiwa  kwa nafasi ya Urais ni kura 12,338, 667 kutoka katika majimbo yote ya Uchaguzi 291 huku kura zilizoharibika zikiwa 108975 na kura halali zikibaki 12,222,980.

Katika kinyang’anyiro hicho Wycliffe Musalia Mudavadi anashika nafasi ya tatu akiwa amejikusanyia kura  483,981 nafasi ya nne ikienda kwa Peter Kenneth mwenye kura 72,786.

Mgombea wa Alliance for Real Change,Mohamud Abduba Dida anashika nafasi ya tano akiwa na kura  52,848 akifuatiwa na Mwana mama Martha Karua wa National Rainbow Coalition mwenye kura 43,881 hadi sasa.

Nafasi ya saba katika wagombea hao Urais inakwenda kwa James ole Kiyiapi wa Chama cha Restore and Build Kenya ambaye ana kura 40,998 huku nafasi ya ya nane na mwisho ikishikwa na Paul Kibugi Muite wa chama cha Safina.

Matokeo hayo yatatangazwa rasmi leo saa 5 asubuhi.

Wednesday, March 6, 2013

MWENYEKITI JUKWAA LA WAHARIRI AVAMIWA, AJERUHIWA VIBAYA

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya New Habari wachapishaji wa magazeti ya Mtanzania, Dimba, Bingwa na Dimba, Absalom Kibanda amevamiwa na watu wasiojulikana akiwa ndani ya gari lake wakati akiingia nyumbani kwake Mbezi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Kibanda alivamiwa majira ya saa sita usiku wa kumkia leo Tar March 6 2013, akitokea kwenye majukumu yake ya kila siku. Inadaiwa kuwa alichomolewa kwene gari, akapigwa na vitu vyenye ncha kali kichwani, ametobolewa jicho lake la kushoto pamoja na kunyofolewa kucha na baadhi ya vidole na hatimaye kutupwa mbali kidogo kutoka nyumbani kwake.


Baada ya hapo wasamalia wema walijitokeza na kumkimbiza katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ambako alipokelewa vizuri na madaktari na kumpatia tiba ya awali na baadaye kumhamishia Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI) ambako mpaka sasa anaendelea na matibabu.


Watu waliomfanyia madhara hayo, hawakuweza kuchukua kitu chochote kwenye gari ambapo kulikuwemo Laptop, simu na nyaraka zingine.