Thursday, September 22, 2011

FAMILIA YA DR. REMMY ONGALA YAANDAA TAMASHA LA KUMUENZI BABA YAO

Mtoto wa Marehemu Dr Remmy Ongala, Aziza Ongala (kushoto)

Marehemu Dr. Remmy Ongala
Familia ya marehemu Dr. Remmy Ongala imeandaa sherehe Tamasha la kumbukumbu ya baba yao litakalofanyika Tar 10 Desemba katika viwanja vya Leaders jijini Dar Es Salaam
.
Akizungumza jijini London mtoto wa Dr. Remmy Aziza Ongala amesema wameamua kuandaa Tamasha hilo kwa ajili ya kumuenzi na kumkumbuka baba yao kwa kusherehekea Muziki wake kwa kuwa ingawa yeye(baba yao) ameondoka lakini kazi yake ya muziki bado upo na haina mwisho.

Aziza amesema kuwa kwa upande wake ni kazi ngumu sana kuandeaa Tamasha hilo kwa kuwa hajawahi kufanya kitu kama hicho na hii ni mara yake ya kwanza lakini kwa msaada wa mume wake na familia nzima ya Dr. Remmy anaamini jambo hilo litafanikiwa kwa kuwa Tamasha hilo linahusisha Familia nzima.

Hata hivyo baada ya Tamasha hilo wana mpango wa kuanzisha Dr. Remmy Ongala Foundation na ambapo wanatarajia kuianzisha mwaka ujao 2012 na wataanza kwa kutafuta na kusaidia watoto wenye vipaji na baadae wanawake kwa kuwa wanaamini kuwa ukimsaidia mwanamke umesaidia Taifa.

Source:Michuzi Blog!!

STEVE RNB AZIBA PENGO LA BOB RUDALA "INAFRIKA BAND"

Mwanamuziki ambaye anafanya vizuri kwenye gemu ya muziki wa Bongo Flava (Kulia)Steve Rnb ambae ametamba na vibao kadhaa kama vile One Love na Sogea karibu hatimaye ametua INAFRIKA Band ili kuziba pengo la Bob Rudala ambae ameihama bendi hiyo na kutimkia Kalunde Band. Akizungumza na blog hii Steve amesema ameamua kujiunga na bendi hiyo kwa kuwa ni bendi ya muda mrefu inayofanya vizuri hivyo anaamini atajifunza mengi sana kutoka kwa wanamuziki wa bendi hiyo, kwa kuwa sasa anafanya vitu vingi kama vile utumiaji wa vyombo mbalimbali tofauti na ilivyokuwa mwanzoni ambapo alikuwa akiimba tu.
Mmoja kati ya watunzi na waimbaji wa Bendi hiyo "Hamis" (pichani) amesema yeye binafsi anafurahia kufanya kazi na Steve kwa kuwa ni kijana anayejituma na ndio maana ameweza kuziba pengo la Bob Rudala, hivyo anatumai baada ya muda atakuwa mwanamuziki bora zaidi ya sasa kwa kuwa ameanza kupiga vyombo mbalimbali na anaendelea kujifunza kupiga vyombo vingine.
Akizungumzia kuhusu bendi kiongozi wa Bendi hiyo "Roy" amesema kwa sasa bendi yao imejipanga vizuri kulingana na soko la muziki kwa sasa na wanatarajia kutoa Album yao mpya itakayoitwa jina la Mbeleko wakati wowote kuanzia sasa hivyo mashabiki wakae tayari kuipokea Album hiyo.
Ukipenda kuiona kazi ya Steve Live fuatilia Afrobeat kila Jumamosi saa moja jioni, ili uone Steve Rnb anavyokung'uta Drums.

AFROKIJA YAZUNGUMZA NA KIDA WAZIRI


Naamini utakuwa unamkumbuka Mwanamama Kida Waziri (pichani) ambaye alitamba na Bendi ya Vijana Jazz na kujijengea heshima kubwa sana hasa kwa wanawake kutokana na vibao vyake vikali ambavyo vilibeba ujumbe mzito na wenye mafundisho, kama vile kibao Mawifi ambacho kimebeba ujumbe wa wanawake kuwanyanyasa wifi zao, kibao Penzi haligawanyiki ambacho kinazungumzia suala zima la mapenzi kama jina la wimbo linavyojieleza na vingine vingi tu.

Kida Waziri ambae kwa sasa amebadili dini na kutoka Uislam na kwenda Ukristo na kuokoka kabisaa ana Historia kubwa sana katika Muziki ambapo mpaka kufikia alipo sasa amepitia mambo mengi na kujifunza vitu vingi sana, mwenyewe anasema alikuwa akipenda Muziki tangu akiwa mdogo ila alikuwa muoga wa kupanda Stejini na kuimba mbele za watu na mara yake ya kwanza kufanya hivyo ilikuwa nchini Kenya ambapo alipata mshituko mkubwa sana na kushindwa kuendelea kuimba kutokana na watu kumshangilia sana kwa sauti yake na uimbaji wake kwa ujumla maana ndo ilikuwa mara yake ya kwanza kuimba na aliongopewa kuwa akiimba hatosikika hivyo yeye aliamini kuwa anaimba kwa kujifurahisha tu lakini si kwa kutoa burudani.

Na baada ya hapo akapewa moyo kuwa anaweza na ndo akapata moyo wa kuwa anaweza na kuamua Rasmi kuianza kazi hiyo ya Muziki, lakini aliporejea hapa Nchini Tanzania kutokea Kenya alipata mtihani mkubwa sana baada ya dada yake aliyekuwa akiishi nae kumzuia kuimba maana alikuwa akiishi jirani na na Mzee King Kikii hivyo akawa anamkaribisha mazoezini kwao ili aweze kuimba ila dada yake ndo hivyo akawa anamuwekea ngumu mpaka ikafikia wakatia akamfuata King Kikii na kumwambia kuwa akiendelea kufuatilia mdogo wake atamshtaki kwa wazazi wake kuwa anamfundisha tabia Mbaya Kida kwa kuwa alikuwa natumia muda mwingi mazoezini na hashiriki katika kazi za nyumbani, ila mwisho wa siku aliruhusiwa na ndo akaanza kuimba katika Bendi ya Jeshi hapa hapa jijini Dar Es Salaam na hatimaye akaangukia katika bendi ya Vijana Jazz na baadae akaachana kabisa na muziki mpaka mwaka huu alipoamua kurejea tena na kuamua kuzirekodi upya baadhi ya nyimbo zake za zamani na kutoa Album yake binafsi.

Ana Historia ndefu sana na yenye kuvutia ila hapa nimekupa kwa ufupi tu yale ambayo naamini wengi walikuwa hawayafahamu lakini kwa undani zaidi fuatilia Afrobeat ya Eatv ili upate kumsikia Livee!!!

Tuesday, September 20, 2011

PRINCE AMIGO ATOA SOMO KWA WANAMUZIKI WENYE TABIA YA KUHAMA HAMA BENDI ZAO

Mwimbaji mahiri wa kundi la Taarab la Jahazi Modern Taarab Prince Amigo amekanusha uvumi uliokuwa umeenea mitaani kuwa ana mpango wa kulihama kundi lake hilo la sasa na kuhamia kundi jipya la Tanzania Moto.

Akizungumza na Blog hii Prince Amigo amesema ni kweli alifuatwa na uongozi wa kundi hilo(Tanzania Motto) ili aweze kujiunga nao lakini yeye binafsi alikataa kwa kuwa hakuwa na sababu ya kuihama Jahazi na kujiunga na kundi hilo. "Ni kweli kundi hilo lilinifuata lakini mimi binafsi sikuona sababu ya kuhama Jahazi na kujiunga na kundi hilo"

Amigo aliongeza kuwa yeye kama msanii anayejitambua hawezi kuhamahama bila kuwa na mipango kwa sababu kuhama bendi kila siku kunamfanya msanii adharaulike na kuonekana hana msimamo na hajui anachokifanya. "Unajua mimi kama msanii ambae najitambua na kuelewa nini ninachofanya siwezi kuhamahama ovyo kwani ukiangalia wengi ambao wana tabia hiyo hawana mafanikio na wanapotea kimuziki lakini wale wanaotulia tunaona mafanikio yao, mfano dada yangu Luiza Mbutu yeye ana mafanikio makubwa kwa sababu ametulia sehemu moja na anajitambua yeye ni nani hivyo mimi naiga mfano wake.

Mengi zaidi usikose kuangalia Afrobeat ya EATV jumamosi hii saa moja usiku.

Wednesday, September 14, 2011

CHEZEA AFRIKA WEWEEEEEEEE!!!!

Miss Angola ambae ndiye Miss Universe 2011 Leila Lopes
 Miss Universe 2011 Leila Lopes akivishwa Taji na aliyekuwa akishikilia Taji hilo Miss Universe 2010 Ximena Navarette kutoka Mexico.


Hatimaye mashindano ya kumsaka Miss Universe yamefikia tamati ambapo mrembo kutoka Angola Leila Lopes ameibuka kidedea kwa kuwatupa kule wenzake 88 na kunyakua Taji hilo la Miss Universe 2011.

Mashindano hayo yamefanyika usiku wa kuamkia Leo huko Sao Paulo, nchini Brazil, ambapo Tanzania tuliwakilishwa na Mrembo Nelly Kamwelu.

KAMATI MISS TANZANIA YAWAOMBA RADHI WATANZANIA

Kamati ya mashindano ya urembo ya Miss Tanzania imewaomba Radhi watanzania na wale wote waliopatwa na maafa ya ajali ya kuzama kwa meli ya MV SPICE ISLANDER huko visiwani zanzibar, kwa kuendelea na shindano wakati Taifa likiwa kwenye majonzi mazito ya kuwapoteza watu zaidi ya 200.

Mratibu wa Shindano hilo Hashim Lundenga amesema kuwa kamati yake ililazimika kuendelea na Shindano hilo kutokana na kumalizika kwa muda wa kuwasilisha jina la mshindi kwenye shindano la Mrembo wa Dunia.

Lundenga aliongeza kuwa kamati yake ilipata taarifa hizo za Jumamosi saa 9:30 alasiri ambapo muda mfupi tu ulikuwa umebaki kabla ya shindano hilo kuanza, hata hivyo shindano hilo lilifanyika wakiwa latika maombolezo ambapo kabla ya kuanza shindano watu wote waliokuwepo ukumbini walisimama kimya kwa muda wa dakika moja kwa ajili ya kuomba na hata washiriki walipopita jukwaani kwa mara ya kwanza walikuwa wamevaa vitambaa vyeusi kuashiria maombolezo.

MWENYEKITI WA MAKAMPUNI YA IPP ATOA RAMBIRAMBI ZANZIBAR

Mwenyekiti wa makampuni ya IPP MEDIA LTD Bw. Reginald Mengi akikabidhi hundi ya Sh.mil. 40 kwa makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ally Idd kwa ajili ya Rambi rambi kutokana na ajili ya kuzama kwa Meli iliyotokea visiwani humo.

Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP MEDIA LTD Bw. Reginald Mengi akisaini kitabu cha Maombolezo katika ofisi ya makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar.

Tuesday, September 13, 2011

RWANDA VS TANZANIA

Huyu ni mwanafunzi wa Tanzania nchi ambayo mwaka huu inatimiza miaka 50 ya uhuru (akiingia darasani)

Na hawa ni wanafunzi wa Rwanda ambao wametoka kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka mitano iliyopita
Nimeweka hii post nikiamini unaweza kujifunza kitu katika hizi picha mbili, Tanzania yetu ndipo ilipo sasa na huo ni mfano mmoja tu lakini ukitembea katika maeneo mbalimbali hapa nchini utjionea mwenyewe jinsi wanafunzi wa kitanzania wanavyosoma na kuishi katika mazingira yasiyoridhisha.

 Pamoja na kelele zinazopigwa kila kukicha na baadhi ya vyombo vya habari lakini yanaingia sikio moja na kutokea la pili na hapo ndipo tunapodhihirisha ule usemi wa "kelele za mlango hazimzuii mwenye nyumba kulala"       TEMBEA UONE

Ahsante mdau ANDREW ZOMARI: Kwa picha

NAUNGANA NA WATANZANIA WENZANGU KUTOA SALAMU ZA POLE NA RAMBIRAMBI KWA WENZETU WALIOATHIRIKA NA AJALI YA MELI

MV Spice ikiwa inazama

Baadhi ya ndugu wakijaribu kutambua miili ya ndugu zao katika picha

Kwa kweli aliyepakia magodoro amekuwa msaada mkubwa sana kwa kuwa baadhi ya watu waliokosa life jackets waliyatumia magodoro hayo ili kujiokoa

Vyombo vya usalama na wasamaria wema wakisaidia zoezi la uokoaji
Naamini kila mmoja wetu atakuwa ameguswa na maafa makubwa yaliyotokea usiku wa kuamkia Tar 10, Septemba ya kuzama kwa meli ya MV Spice na kusababisha mamia ya ndugu zetu kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa, kama ambavyo tumeona na kusikia mengi yakizungumzwa na kufanyika hivyo basi nami kama mtanzania na binadamu ambae pia kwa namna moja au nyingine naguswa na matatizo mbalimbali yanayowakabili binadamu wenzangu napenda kutoa pole kwa wale wote ambao kwa namna yoyote ile wameguswa au kuathiriwa na maafa haya.

Huu si muda wa kuzungumza mengi sana ila la msingi ni kuwaombea ndugu zetu waliopoteza maisha walale mahali pema peponi na wale walionusurika kwenye ajali hiyo wapate nafuu mapema ili waweze kurejea katika shughuli zao za kila siku... AMEEN.

WASHIRIKI WA MAFUNZO YA HABARI ZINAZOHUSU UNYANYAPAA WAPEWA VYETI

Afisa Habari wa PACT TANZANIA, Bi. Leah Mwainyakule akiwa na mwezeshaji wa mafunzo bw.Wilbroad Manyama

Mdau Abdulaziz Ahmed kushoto, wa Channel Ten akipokea cheti cha kufuzu mafunzo ya unyanyapaa kwa watoto na watu wanaoishi na VVU, anayekabidhi ni bw. Wilbroad Manyama akishuhudiwa na bi. Leah Mwainyakule

Baadhi ya Waandishi waliopata mafunzo hayo
Mdau Abdulaziz wa pili kutoka kushoto akiwa na Mdau Frank kutoka Iringa (kushoto) na wakati wa mafunzo

Waandishi wa habari kutoka mikoa Tisa ya Lindi, Mtwara, Iringa, Rukwa, Mbeya, Tanga, Dodoma, Morogoro na Dar Es Salaam wamepatiwa mafunzo ya siku tano ya unyanyapaa kwa watoto na watu wanaoishi na VVU.
Mafunzo hayo yaliyofanyika mkoani morogoro yameandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la PACT TANZANIA kwa lengo la kuwawezesha waandishi wa habari nchini kufahamu namna ya kuandika habari za unyanyapaa wa watoto na watu waishio na VVU.
 
Sambamba na mafunzo hayo ya siku tano waandishi hao pia walipatiwa nyeti vya kufuzu mafunzo hayo.
HABARI NA: Mdau Abdulaziz- Lindi.

Thursday, September 8, 2011

MHINA PANDUKA AINGIA MATATANI KWA UDANGANYIFU

Mhina panduka
Panduka kushoto na Mangustino wa K- Mondo Sound
MWIMBAJI maarufu nchini Tanzania, Mhina Panduka ‘Toto Tundu’ ameingia matatani baada ya uongozi wa Bendi ya K-Mondo Sound kuamua kumfungulia kesi ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, baada ya kusaini mkataba wa kufanya kazi na Bendi hiyo kwa muda wa mwaka mmoja kuanzia Oktoba mwaka jana na badala yake alifanya kwa muda wa mwezi mmoja tu na kutimkia Visiwani Zanzibar na baadae kurejea Dar Es Salaam na kufanya kazi na TOT Band.
Taarifa iliyotolewa na Uongozi wa K-Mondo Sound imesema kuwa, wamefikia hatua hiyo ya kumshitaki Panduka baada ya kujaribu kumuita mara kadhaa tangu Aprili mwaka huu ili kumaliza suala lake lakini mwanamuziki huyo hakuonekana kujali.
“Tulimwita Panduka Aprili mwaka huu wakati wa sikukuu ya Pasaka aje kumaliza suala la mkataba wake,  tulipozungumza nae alisema hajasaini mkataba na TOT na atarudi, lakini akaomba afanye show ya Jumapili ya Pasaka pale Mango na TOT halafu atarudi K-Mondo lakini mpaka leo hajatokea,
Baada ya hapo tulimwandikia barua kupitia kampuni ya uwakili ya JM Attorney na akatakiwa kumaliza suala hili lakini mpaka leo hakuna alichojibu zaidi ya kuwatumia meseji viongozi kuwa watapambana mahakamani,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema wanamuziki wengine watatu ambao walikuwa wamechukua pesa na kukimbia wote waliamua kurudi kumalizia mikataba yao na mwingine ambaye ni mpiga rythim Fadhili aliamua kurudisha hela. Wengine waliokuwa wameondoka baada ya kuchukua hela lakini wakaamua kurudi kumalizia mikataba yao ni Joshua Bass ambaye alitimkia THT na Husein Said Tumba aliyekuwa Royal Band.
Taarifa hiyo  iliongeza kuwa baada ya kushauriana na wanasheria uamuzi uliofikiwa ni kumfungulia kesi hiyo ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu ili sheria ichukue mkondo wake kwani nyaraka zote za kusaini mkataba na jinsi alivyochukua pesa zipo.
Mbali na kuchukua pesa hizo Panduka pia ameitia K-Mondo Sound Band  hasara ya zaidi ya shilingi Milioni tatu kutokana na gharama ilizotumia kurekodi nyimbo tatu ambazo sauti yake ipo pamoja na Video hali iliyofanya nyimbo hizo zishindwe kurushwa hewani. Panduka alirekodi wimbo uitwao Kaumia, U Still Mine na Mpenzi Issa huku Video za Kaumia na U Still Mine zikiwa zimetengenezwa.

HALI ILIVYOKUWA LEO ASUBUHI PALE MOROCO HOTEL

Umati wa watu ulijaa kushuhudia kilichotokea
Kusimuliwa haifai, jamaa akapark gari yake ili ajionee nini kilichojiri

Magari yaliyogongana ndo hayo hapo
Jamaa sijui anafanya nini hapo


Kama ambavyo umeona hizo daladala mbili ndizo zilizohusisha hiyo ajali kwa kugongana ubavuni, daladala moja ikifanya safari za msasani - Gongo la mboto na nyingine Makumbusho- kariakoo, ila cha kumshukuru mungu ni kuwa hakuna aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa.

Wednesday, September 7, 2011

KIDA WAZIRI MBIONI KUTOA ALBUM YAKE

Kida Waziri katika pozi

Mwanamuziki wa enzi hizo wa bendi ya Vijana Jazz Kida Waziri (pichani) amejipanga kutoa Album yake binafsi ambayo itakuwa na nyimbo sita, ambapo nne kati ya hizo ni zile alizowahi kuziimba miaka ya 90 wakati akiwa na bendi yake hiyo.
Akizungumza jijini Dar Es Salaam Kida ambae ni mwanamke wa kwanza kuimbia Bendi ya Vijana Jazz amesema mpaka sasa anafikiria "wimbo wifi zangu" ndio utakaobeba jina la Album hiyo ambayo alianza kurekodi jijini Arusha kabla ya kuhamishia kazi hiyo jijini DSM ambapo anamalizia nyimbo zake zilizobaki.

Pamoja na wifi zangu Kida amesema nyimbo zingine za zamani zitakazokuwa kwenye Album hiyo ni Penzi haligawanyiki, Mary maria na Penzi haligawanyiki sehemu ya pili ambazo zote alishiriki kuziimba.
Amefafanua kuwa ameamua kurudia nyimbo hizo kwa kuwa anaamini watu wengi wangependa kuzisikiliza nyimbo hizo zikiwa zimerekodiwa kiustadi na sauti ya Kida kama ilivyokuwa ikisikika miaka ya nyuma.

Kida ameongeza kuwa kazi hiyo ya kurekodi ilikwishakamilika lakini baada ya kusikiliza alibaini baadhi ya mapungufu hivyo kulazimika kuzirudia baadhi ya nyimbo katika Studio za Dar Es Salaam.

MARIAM BSS AKIRI KURUDISHA PESA TANZANIA MOTO

Mariam katika Interview na Afrobeat
Mariam na Mutoto muzuri "Kijah"
Mshindi wa BSS 2010 Mariam Mohamed, amefunguka kuhusu uvumi kuwa alikuwa na mpango wa kulihama kundi lake la sasa la Five Stars Modern Taarab na kuhamia kundi jipya la Tanzania Moto ambalo limeanzishwa hivi karibuni.

Akizungumza na kipindi cha Afrobeat kinachorushwa na Eatv, Mariam amekiri kuwa ni kweli alipata ushawishi wa kujiunga na kundi hilo kutokana na ushawishi wa pesa na ahadi nyingi ambazo alizipata kutoka kwa viongozi wa kundi hilo. "Unajua pesa ni shetani sana na shetani wa pesa ndiye alinishawishi kutaka kulihama kundi langu lakini baada ya kukaa na viongozi wangu wa Five stars na mimi mwenyewe kutafakari nilibadilisha uamuzi na kuamua kurudisha pesa ambazo walinipatia viongozi wa Tanzania moto" alisema Mariam.

Mariam ameongeza kuwa viongozi wa Kundi hilo walimpatia pesa taslimu Shilingi laki nne na nusu (450,000) za kulipia nyumba ili aweze kuhama nyumba anaishi sasa.. Hata hivyo amedai kuwa hata baada ya kurudisha pesa hizo viongozi wa Tanzania Moto bado wanaendelea kumshawishi kuhamia kundi hilo ambapo amekiri kuwa hatoweza kuhamia kundia hilo na hayuko tayari kuafanya kazi na kundi l;olote kwa sasa zaidi ya Five Stars kwani anaamini kuwa yeye ni muhimu na anahitajika sana kwenye kundi hilo.  

Usikose kuangalia Afrobeat Jumamosi hii saa moja jioni kwa hayo na mengine mengi ambayo Mariam ameyazungumza.

MAMBO YALIVYOKUWA NDANI YA TRIZ MOTEL NA BURUDANI KUTOKA K-MONDO SOUND

Hapo nikifanya Interview na Mangustino a.k.a Teacher Mangu
Interview ikiendelea
Burudani kwa kwenda mbele
Nimekuonjesha tu hapo lakini kiukweli ilikuwa ni burudani ya nguvu mimi nilicheza na kuimba mpaka sauti ikaanza kukauka nikasema sasa imetosha nikaondoka nikawaacha wapenda burudani wakiendelea kuburudika, kama hujawahi kuwatembelea nakushauri uende ili ukonge roho yako, lakini pia usikose kupata burudani hiyo kupitia Afrobeat ya Eatv Jumamosi hii saa moja jioni.

SAMAHANI NDUGU ZANGU KWA UKIMYA WA MUDA MREFU

Ndugu zangu nilikuwa kimya kwa muda mrefu kidogo kutokana na matatizo ambayo yalikuwa nje ya uwezo wangu, lakini sasa mambo yamekaa sawa na tutaendelea kuwa pamoja kwa kufahamishana mambo mbalimbali.. Nawatakia siku njema na majukumu mema.